Watu 700 Wameuawa DRC Ndani Ya Siku 5 – Global Publishers

 

Umoja wa Mataifa (UN) umetoa wito wa kukomesha vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 yamesababisha watu zaidi ya 700 kuuawa huku wengine wasiopungua 2,800 wakijeruhiwa katika kipindi cha siku tano.

Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na washirika wa serikali, wamefanya tathmini ambayo ilifichua hali ya kuogofya ya mgogoro huo wa eneo la mashariki mwa DRC. Maafisa wameonya kwamba, idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri habari zaidi zinavyopatikana.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia zinazoongezeka katika eneo hilo, na kuonya kuhusu hali mbaya zaidi katika mji wa Goma, ambao ni makazi ya takriban watu milioni 3.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa tahadhari kuhusu kupungua kwa usambazaji wa chakula, maji safi na matibabu.

“Watu wanakosa chakula, maji safi, vifaa vya matibabu, na kwa msingi huo tuna wasiwasi mkubwa,” msemaji wa WFP, Shelley Thakral amesema na kuongez kuwa, “Mgogoro huo unachangiwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”

Angalau kambi mbili za wakimbizi wa ndani (IDP) zilishambuliwa kwa mabomu, kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR). Shirika hilo la haki la UN pia limeleza habari ya kuuawa kinyume cha sheria watu wasiopungua 12 na waasi wa M23 kati ya Januari 26 na 28.

Tayari waasi wa kundi la M23 la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeteka mji mkubwa zaidi mashariki mwa nchi hiyo, Goma, wametangaza nia yao ya kuelekeza vita katika mji mkuu, Kinshasa, huku Rais Félix Tshisekedi akitoa wito wa kuandaliwa jeshi kubwa kukabiliana na mashambulizi hayo.

Related Posts