ZEC yashtuka, yaonya makarani uandikishaji daftari la mpigakura

Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Aziza Iddi Suweid, amesisitiza kuwa tume haitarajii kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliokosa kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura iwapo wanakidhi vigezo. Amewataka wakuu wa vituo na makarani wa uandikishaji kuhakikisha kila mwenye sifa anapata haki yake ya kuandikishwa.

Akizungumza leo Jumamosi, Februari 1, 2025, wakati wa kufunga mafunzo kwa wakuu wa vituo na makarani wa uandikishaji wa awamu ya pili kisiwani Pemba, Jaji Suweid amesema ni wajibu wa makarani kuhakikisha wanaowaandikisha ni wale wanaokidhi vigezo, huku wale wasio na sifa wakipewa fomu maalum kwa mujibu wa utaratibu.

“Viapo mlivyoapa vya kufanya kazi kwa maadili mviheshimu kwa kuhakikisha kila mwenye haki ya kuandikishwa anapata fursa hiyo ili aweze kushiriki kupiga kura uchaguzi utakapofika,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa Tume ya Uchaguzi ni chombo huru kinachotoa haki kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Hivyo, amekemea uwepo wa tofauti zozote zinazoweza kumyima mtu haki yake ya kupiga kura.

Pia, amehimiza kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, akiwataka makarani kuwa mfano wa maadili kazini.

“Tumia lugha nzuri, na hata pale inapobainika kuwa mtu hana sifa za kuandikishwa, mueleze kwa ustaarabu na kauli yenye staha,” amesema.

Mratibu wa Tume ya Uchaguzi Pemba Ali Said amesema kuna matumaini makubwa kwamba mafunzo haya yatawaandaa watendaji kwa kazi zenye ubora na ufanisi.

Baadhi ya wakuu wa vituo vya uandikishaji, akiwemo Asha Abdalla Omar, amesema kutokana na mafunzo hayo, changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza, kama tatizo la kutosoma kwa alama za vidole, hazitajirudia kwa kuwa tayari zimeptiwa ufumbuzi.

Mohamed Salim Mohamed pia amesisitiza kuwa kupitia mafunzo haya, matatizo yaliyotokea awamu ya kwanza yamepatiwa suluhisho, hivyo wananchi wanapaswa kufuata taratibu, ikiwemo kuangalia mabango yanayoonyesha shehia zao, ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina amewataka makarani wa uandikishaji kushirikiana kwa karibu na wananchi wanaofika vituoni kwa kutumia lugha nzuri na staha.

Amesema ni muhimu kwa watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi kwa kuzingatia miongozo, maelekezo, kanuni, na sheria zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi.

Aidha, amesisitiza kuwa kazi wanayoifanya ni jukumu la kitaifa linalohitaji ustadi ili kuhakikisha wapigakura wanapata fursa ya kuamua hatima ya demokrasia ya taifa katika uchaguzi ujao wa Zanzibar na Tanzania.

Mkurugenzi huyo amesema Tume ya Uchaguzi Zanzibar inaendelea na maandalizi ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kuwaandikisha wapigakura wapya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Katika kipindi hiki, tume ina jukumu la kusimamia na kuendeleza daftari kwa kufuata utaratibu, ikiwa ni pamoja na kuandaa ratiba ya uandikishaji wa wapiga kura,” amesema Faina.

Amesema tume itatumia watendaji wa uandikishaji walioteuliwa kisheria baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Mratibu wa Ofisi ya ZEC Pemba, Ali Said Ali, amesema kuwa mafunzo haya yanawajengea uwezo wa utendaji, hivyo ni muhimu kwa washiriki kuwa makini ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Almesema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya mafanikio katika uendeshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

“Nina imani kuwa mafunzo haya yatawajenga vyema na kuwawezesha kufanya kazi zenu kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Related Posts