LIGI Kuu Bara inazidi kupaa na kuonekana kuwa mojawapo ya ligi zenye nguvu katika Afrika. Kwa sasa Ligi hiyo inashika nafasi ya sita kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na ipo nafasi ya nne kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS).
Shirikisho hilo limeipanga ligi hiyo nafasi ya 57 duniani mwaka 2024 na kwa Afrika ikiwa imepitwa na Ligi Kuu ya Misri (Nile Premier League), Batola Pro ya Morocco na Ligue 1 ya Algeria tu.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, huku kukiwa na wimbi kubwa la makocha na wachezaji wa kigeni kukimbilia kuja kucheza Tanzania, bado kumekuwapo na ubabaishaji mkubwa katika klabu zinazoshiriki mashindano haya.
Utafiti uliofanywa na Mwanaspoti umeonyesha kuwa ni klabu tatu tu kati ya 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zinayokidhi matakwa ya kanuni za Leseni za Klabu, na hii inatia wasiwasi kuhusu mustakabali wa soka la vijana nchini.
Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kifungu cha 26 kimeweka wazi kwamba, “Kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara au Mashindano ya Kimataifa inatakiwa iwe na angalau, timu mbili za vijana ya kwanza kuanzia miaka 15-21 na 10-14.”
Aidha, kifungu cha nne cha Sera ya Maendeleo ya Michezo Tanzania kinasisitiza kuwa: “Kila chama cha mchezo ambao unashindaniwa kitaifa na kimataifa lazima kiwe na timu mbili za kudumu ambazo ni za vijana na timu za wakubwa. Mtiririko huu lazima uanzie kwenye klabu mbalimbali, vyama vya wilaya, mikoa hadi ngazi za taifa.”
Licha ya msisitizo huo wa kanuni na sera lakini bado klabu 13 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimeshindwa kuzingatia hilo kwa unyoofu wake.
Klabu tatu ambazo zimeonyesha kufuata kanuni na sera hizo ni Azam FC, Mashujaa na Fountain Gate zikionyesha mfano mzuri wa uwekezaji wa soka la vijana kwa kuzalisha vijana wapya kuanzia chini.
Azam FC imeonyesha mfano mzuri wa uwekezaji wa soka la vijana ikiwa klabu iliyofuata vyema kanuni na sera hiyo ya kuzalisha vijana ikiwa na timu ya vijana kuanzia miaka 10-14, ambayo ni hatua muhimu katika kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.
Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Omar Kuwe anasema kuwa uwekezaji katika soka la vijana ni muhimu, na klabu inahitaji nguvu ya kiuchumi ili kuendesha programu hizo.
“Kuwa na timu za vijana ni biashara inayohitaji muda mrefu ili kupata faida. Iwapo tutafanikiwa kumuuza mchezaji mmoja, inaweza kulipa gharama za kikosi kwa mwaka mzima lakini kwanza lazima upitie njia ndefu ya kumtengeneza vizuri huyo kijana kuanzia chini na kumuendeleza kuanzia chini mpaka kufika juu,” anasema Kuwe.
Mashujaa nayo ipo nyuma ya Azam FC, inaweka wazi kwamba inamiliki timu za vijana chini ya miaka 10 mpaka 20 ikizalisha wachezaji hadi maofisa wa michezo wakiwamo waamuzi wa soka kupitia kituo chao cha Twalipo kilichopo jijini Dar es Salaaam.
Ofisa habari wa timu hiyo, Khamis Malyango anasema hatua ya kuzalisha vijana hao ni mpango ulioanza muda mrefu hata kabla hawajapanda Ligi Kuu Bara huku akikiri kuwa ili mpango huo uwe na mafanikio na endelevu unahitaji rasilimali fedha na uthubutu.
“Sisi Mashujaa hizo timu za vijana zote na hii program naweza kusema tulikuwa nazo hata kabla hatujapanda Ligi Kuu, kazi kubwa imekuwa ikifanywa pale kwenye kituo chetu maarufu cha Twalipo na tumekuwa tu sio tunazalisha wachezaji wapo pia hadi waamuzi tukiwatengeneza kuanzia chini kabisa,” anasema Malyango.
“Hii ni programu ambayo inahitaji uthubutu mkubwa kama unakusudia kutaka kuona matunda yanayostahiki, lakini kikubwa kinahitaji sana rasilimali fedha ili uweze kufanikisha haya kwa manufaa ya soka la Tanzania.”
Fountain Gate iliyonunua timu iliyokuwa Singida Big Stars ipo kwenye kundi hili ikiwa na timu za vijana chini ya miaka 20, 17, 10 zikilelewa kwenye makundi mawili tofauti.
Ofisa Habari wa Fountain, Issa Liponda anasema timu hizo mbili za U 20 na U 17 hizo zinasimamiwa na timu ya Ligi Kuu, huku zile za vijana chini ya miaka 15 na 10 zikiwa chini ya usimamizi wa shule zao za Msingi na Sekondari za Fountain Gate.
“Tuna timu nne za vijana zile za chini ya miaka 20, 17, 15 na 10 lakini hizo mbili za miaka 20 na 17 zinasimamiwa na uongozi wa timu wa Fountain Gate, ila hayo makundi mawili ya chini utaona ni vijana wadogo zaidi ambao wanahitaji usimamizi mkubwa, tuliamua zikibaki kwenye usimamizi wa uongozi wa shule zetu za Fountain Gate,” anasema Liponda.
Baada ya kuziangalia timu tatu pekee zilizofuata kanuni hiyo kwa usahihi, klabu 13 zilizobaki zimeshindwa kuwa na ukamilifu huo huku, kati ya hizo, ni sita pekee zenye timu moja ya vijana, ambayo ni U20.
Hali hii inadhihirisha changamoto kubwa zinazokabili soka la vijana nchini. Katika makala hii, tutaangazia kila klabu na changamoto zinazowakabili, huku Tabora United FC ikieleza kuwa haijajipanga katika soka la vijana. Hii inaonyesha kuwa hata klabu zenye historia ndefu zinashindwa kuwekeza katika timu za vijana kwa sababu ya gharama kubwa za uendeshaji.
Klabu nyingi zinafahamu umuhimu wa kuanzisha programu za vijana, lakini gharama za vifaa, safari za mashindano, na ukosefu wa wadhamini vinazifanya zipate ugumu kuanzisha timu za vijana.
Aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaaya, kabla ya kuondoka kwenye nafasi hiyo alisema walikuwa na kikosi kimoja cha U20 ambacho kiko chini ya kocha Samweli Galafao mwenye leseni B ya CAF. Hata hivyo, klabu hii inakabiliwa na changamoto nyingi.
“Changamoto kwa timu hii imeshindwa kuwa na programu maalum ya kukuza vipaji vya vijana kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa licha ya kujitahidi lakini ukosefu wa rasilimali fedha unawazuia kuweza kuendeleza vijana kwa njia bora,” alisema Kaaya ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa Singida Black Stars.
Tabora United FC kupitia msemaji, Christina Mwagala anasema hawajajipanga vizuri katika soka la vijana ingawa wana kikosi kimoja cha U20 ambacho wanapambana kuhakikisha kinakuwa endelevu.
“Tunafahamu umuhimu wa soka la vijana, huu ni mpango ambao unahitaji muda na nguvu lakini kwetu Tabora kama mnavyofahamu huu ni msimu wetu wa pili Ligi Kuu, baada ya kucheza play off msimu uliopita tulihitaji kuweka nguvu zaidi kuhakikisha kwanza timu yetu mama inasimama imara lakini wakati huo basi tusiache kabisa kuweka nguvu kwenye soka la vijana tukasimama imara na hii timu ya chini ya miaka 20,” anasema Mwagala.
Pamba kupitia mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mohammed Bitegeko anathitisha kwamba, timu yao ina kikosi kimoja cha U20, wakiamua kuanza na kikosi hicho huku wakijipanga kutanua wigo wa kuwa na timu nyingine.
Anazungumzia changamoto kwenye eneo la soka la vijana kwa timu yao iliyorejea Ligi Kuu msimu huu anasema: “Timu za vijana zinahitaji makocha wenye uzoefu mkubwa.”
Pia, gharama za uendeshaji ni kubwa, na ukosefu wa rasilimali unawanyima nafasi ya kukuza vipaji vya vijana.
KenGold FC nayo kupitia Katibu Mkuu wake, Benson Mkocha imethibitisha kuwa ina kikosi kimoja cha U20 pekee, pamoja na ile ya wakubwa ikiwa kwenye msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara tangu ipande.
“Huu ndio msimu wetu wa kwanza kwenye ligi, tunafahamu kwamba kanuni inatutaka kuwa na timu zaidi lakini kipaumbele chetu kikubwa cha kwanza ni timu kubwa kwa kuwa ili uwe sawa kwenye soka la vijana unahitaji nguvu kubwa ya fedha,” anasema Mkocha.
Kagera Sugar FC inatumia kanuni zinazowataka wawe na timu ya vijana, ingawa kwa sasa wana kikosi kimoja tu cha U20.
Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Thabity Kandoro anasema: “Ukosefu wa wadhamini unafanya timu nyingi, ikiwamo yetu, kushindwa kuanzisha timu za vijana kuanzia miaka 10-14.”
Coastal Union, iliyoko Tanga, Ofisa Mtendaji wake mkuu Omar Ayoub anathibitisha kwamba timu yao ina vikosi viwili vya vijana: U20 na U17, ambapo timu hizo zote zinashiriki michuano ya ligi ya vijana, na zinafanya vizuri katika kuandaa wachezaji kwa ajili ya hatua za juu.
Ingawa klabu ina timu mbili, Ayoub anasema, wanakabiliana na changamoto za kifedha na uendeshaji, kwenye kuwalea vijana hao kuwagharamia vifaa na mahitaji mengine ya msingi.
KMC nayo inamiliki timu mbili za vijana, U17 na U20, lakini haina timu ya vijana kuanzia miaka 10-14.
Ofisa Mtendaji wa KMC, Mkuu Daniel Mwakasungula anasema sababu ya ukosefu wa timu hizo ni changamoto za kiuchumi.
“Hatuna timu ya vijana kuanzia miaka 10-14 kutokana na gharama kubwa ambazo kwa sasa hatuwezi kuzimudu,” anasema Mwakasungula.
Tanzania Prisons ina timu mbili za vijana, U20 na U17, lakini haina timu za vijana kuanzia miaka 10-14. Katibu wa klabu hiyo, Ajabu Kifukwe anabainisha kuwa, changamoto ya fedha na kupata wachezaji sahihi kwa umri wa chini ambao muda mrefu wako masomoni ni kati ya changamoto wanazokabiliana nazo katika kuwa na timu za umri wa chini zaidi.
“Hakuna timu za watoto kwa sababu wengi wao wako shuleni lakini kubwa zaidi ni gharama za uendeshaji katika kuzilea hizi timu zote sio kitu rahisi kwa kuwa hakuna mashindano makubwa juu ya hawa vijana,” anasema Kifukwe.
Klabu kongwe na mabingwa wa kihistoria, Yanga yenyewe ina vikosi viwili vya vijana kuanzia miaka 17 na 20 tu. Clement Mzize, ambaye tetesi zinasema anatakiwa na klabu mbalimbali Afrika na nje ya bara hili kwa ada ya uhamisho inayofikia Sh3 bilioni, ni mfano wa matunda ya timu za vijana, akipikwa Jangwani kabla ya kupandishwa katika timu ya wakubwa ya Yanga akiwa ndio kwanza ameitumikia kwa misimu miwili na nusu tu sasa. Dili hili likitimia, hii ni pesa ambayo inaweza kuendesha timu zote za vijana za Yanga kwa miaka kadhaa.
Mkurugenzi wa mashindano wa timu hiyo, Ibrahim Mohamed anasema timu inaendelea na maboresho ya soka la vijana wakianza na timu hizo.
“Tupo kwenye maboresho makubwa ya kuhakikisha hili eneo la soka la vijana linakuwa na mafanikio, kwasasa tuna hizo timu mbili za umri chini ya miaka 17 na 20 lakini huko mbele tutakuwa na nafasi ya kuziongeza za chini zaidi. Changamoto kubwa ni watoto wadogo wana ratiba za masomo, kuna ugumu wa kufanikisha kufanya kile mnachokikusudia,” anasema Mohammed.
Simba ni kama ilivyo kwa watani wao Yanga, ina timu hizo hizo mbili za vijana chini ya miaka 17 na 20 huku ikiweka wazi kwamba nguvu ya uwekezaji inahitajika ili kuweza kufika kwa vijana wa chini zaidi.
Mkuu wa kitengo cha soka la vijana ambaye pia ni meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Kazi ya kulea watoto na kuwakuza inakuwa sahihi kufanywa na akademi lakini sisi Simba tulitaka kwa kuanza tuwe na kitu tofauti ndio maana tulizunguka sana mikoa mbalimbali kutafuta watoto sahihi kwa umri sahihi na kama unavyojua ukitaka kuwa na timu ya umri wa chini zaidi tukumbuke hakuna ligi za watoto kuanzia 10-14, kuna gharama za uendeshaji zinawafanya wachezaji wa umri mdogo kukosa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao,” alisema Rweyemamu.
Singida Black Stars ina timu mbili za vijana, U17 na U20, lakini kupitia Ofisa Habari, Hussein Masanza anataja changamoto ya kifedha ndio inakwamisha mpango mkubwa wa kwenda chini zaidi.
Masanza anasema, “Tumeshindwa kuwa na timu kamili za vijana kuanzia miaka 10-14 kwa sababu inahitaji uwekezaji mkubwa hasa kifedha.”
Dodoma Jiji kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu, Fortunatus Johnson alisema timu yao ina kikosi kimoja tu cha vijana chini ya miaka 20 akitaja ukosefu wa fedha ndio unaowalazimu kuwa na kikosi hicho kimoja pekee cha vijana.
“Kuendesha soka la vijana kunahitaji nguvu kubwa ya fedha sisi Dodoma tuliona kwanza tuwe na hii timu ya chini ya miaka 20, nguvu kubwa tumeipeleka kwenye timu kubwa ya Ligi Kuu lakini tunaendelea kupiga hesabu ni namna gani tutatanua zaidi kuwa na vikosi vingine vya vijana.
“Ili soka la Tanzania liweze kufanikiwa, ni lazima kuwe na mikakati ya muda mrefu na uwekezaji wa kutosha katika programu za vijana. Hii ni njia pekee ya kuhakikisha kwamba tunapata wachezaji wenye viwango vya juu kwa siku zijazo.”
CHANGAMOTO NA MWELEKEO WA SERIKALI
Katika muktadha wa soka la Tanzania, Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msita, anatoa maoni kwamba soka sasa ni biashara inayohitaji uwekezaji mkubwa kutoka kwa klabu.
Klabu nyingi zinajitahidi kufanya usajili wa wachezaji ili kujijenga kiuchumi na kiushindani, lakini hali hiyo ina madhara makubwa kwa ukuaji wa vipaji vya wazawa, hasa vijana wadogo walioko shuleni.
Msita anabainisha kuwa, licha ya kwamba kuimarika kwa soka la Tanzania kunasaidia kuleta maendeleo, changamoto za kiuchumi zinafanya iwe vigumu kwa klabu nyingi kuwekeza katika timu za watoto. Kuanzisha na kuendesha timu za vijana kuanzia miaka 10-14 ni jukumu kubwa linalohitaji muda, fedha na ari ya kujitolea.
“Ni muhimu klabu zisiangalie tu changamoto za leo, bali pia ziangalie kesho,” anasema Msita. Anasisitiza kuwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) lina jukumu kubwa katika kusimamia kanuni na sera zinazohusiana na soka, hivyo inapaswa kuchukua hatua za kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Katibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, anasema kwamba bado kuna umuhimu wa uwekezaji mkubwa ili kuleta maendeleo katika soka la Tanzania na kufikia viwango vya nchi zilizoendelea.
Anasema viongozi wanajitahidi kuandaa mipango itakayosaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kuanzia ngazi ya chini.
“Mipango ambayo tunaandaa itakuwa wazi katika muda mfupi ujao, lakini pia tunajifunza kutoka nchi zilizoendelea jinsi wanavyoweza kukuza vipaji,” anasema Msigwa.
Msigwa anaeleza kuwa, ingawa uwekezaji katika timu za watoto ni muhimu, kuna changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa wadhamini.
Hali hii inafanya kuwa ngumu kwa klabu nyingi kuweza kuanzisha timu za vijana. Kutokana na ukosefu wa rasilimali, klabu nyingi hazina uwezo wa kuwafundisha na kuwapa vifaa wachezaji wa umri mdogo.
Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu wa kuanzisha mashindano kama UMISSETA na UMITASHUMTA, ambayo yanatoa nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao. Ni hatua muhimu katika kukuza soka la vijana nchini.
Ligi ya Tanzania inahitaji kujenga msingi imara wa soka la vijana ili kuweza kutoa wachezaji wenye viwango vya juu. Kukuza vipaji vya vijana ni mchakato wa muda mrefu, lakini unahitaji uwekezaji wa kutosha na msaada wa kifedha kutoka kwa wadhamini na serikali.
Kama klabu zitaweza kuwekeza katika timu za vijana kuanzia umri mdogo, soka la Tanzania litakuwa na mustakabali mzuri. Huu ni wakati wa kutafakari na kuwekeza kwa ajili ya siku zijazo. Lakini kwanini ligi zinaendelea kuchezwa licha ya klabu kukiuka kanuni hii? Ni kwa sababu FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) linataka soka lichezwe duniani kwa kadri iwezekanavyo. Kwa Afrika ambako klabu nyingi hazina uwezo kifedha na hazina udhamini wa kutosha, kuzilazimisha kuwa na timu za vijana ilhali za wakubwa zenyewe hazijimudu kiuchumi, kunaweza kufanya ligi zisimame ama zichezwe na timu chache mno. Kupanga ni kuchagua.