MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamerejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar na kuishusha Simba.
Kurejea kwa Yanga kileleni kumetokana na kufikisha pointi 42, zikiwa mbili zaidi ya Simba yenye 40 ambayo kesho itacheza dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Yanga imerejea kileleni baada ya kupita takribani siku 86 kwani tangu mara ya mwisho iliposhushwa Novemba 7, 2024 wakati ikifungwa 3-1 na Tabora United, ilikuwa haijarejea kileleni ikiziacha Azam na Simba zikipishana kabla ya Simba kuishikilia kwa muda mrefu hadi jana Yanga ilipokaa tena hapo juu.
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ulianza kwa Yanga kuonyesha kuhitaji bao la kuongoza wakipasiana kwa usahihi pasi kuelekea lango la wapinzani lakini Kagera Sugar walikuwa imara zaidi kujilinda huku wakitumia mashambulizi ya kushitukiza.
Uimara wa safu ya kiungo ya Kagera Sugar ambayo ilimtumia Nasoro Kapama ulisaidia kupunguza mahambulizi mengi kupitia eneo la kati kutokana na viungo wao kutopitika kirahisi wakizuia mipira mingi kuelekea langoni mwao.
Wenyeji wa mchezo Yanga walitumia dakika 32 kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao Clement Mzize ambaye alikwamisha shuti kali nyavuni akipokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki.
Bao la Yanga lilianza kusukwa na ukuta wa Kagera Sugar ambao ulikuwa unapasiana pasi fupifupi eneo lao la hatari ndipo viungo wa Yanga wakaunasa mpira ambao uliguswa na nyota watatu wa timu hiyo kabla ya kutikisa nyavu.
Baada ya Yanga kupata bao la kuongoza, waliendeleza mashambulizi langoni mwa Kagera Sugar wakitumia dakika tatu kupata shambulizi lililozaa penalti baada ya kiungo wake Mudathir Yahya kuangushwa ndani ya 18.
Kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda aliibuka shujaa dhidi ya Stephane Aziz Ki baada ya kupangua mkwaju huo wa penalti uliopigwa dakika ya 35.
Hii ni mara ya pili kwa kiungo huyo kukosa penalti katika ligi msimu huu baada ya kufanya hivyo Novemba 7, 2024 dhidi ya Tabora United timu yake ikiambulia kichapo cha mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wakati kipindi cha pili kinataka kuanza, Kocha wa Yanga, Sead Ramovic alifanya mabadiliko akimtoa Israel Mwenda aliyekuwa akichezeshwa winga, nafasi yake akachukua Pacome Zouzoua.
Kuingia kwa Pacome, Yanga iliwafanya kuongeza mashambulizi ambayo yalikuja kuazaa matunda dakika ya 60 baada ya Mudathir Yahya kufunga bao akiwa eneo la boksi akimalizia pasi ya Prince Dube, kisha Pacome akaongeza bao la tatu dakika ya 78 kwa mkwaju wa penalti ulitokana na Maxi Nzengeli kufanyiwa faulo eneo la hatari.
Maxi alifanikiwa kutengeneza bao la nne lililofungwa na Kennedy Musonda dakika ya 87 kwa kichwa baada ya kuanzishiana kona fupi kati ya Kibwana Shomari na Maxi.
Hata hivyo, Kagera ilionekana inashindwa kutengeneza nafasi nyingi hali iliyowafanya Yanga eneo lao la ulinzi muda mwingi kucheza bila ya wasiwasi mkubwa.
Kipigo hicho kimeifanya Kagera Sugar kuendelea kushika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu 16 ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi 16 ikishinda mbili, sare tano na kupoteza tisa.
Yanga yenyewe imekaa kileleni ikiwa imeshuka dimbani mara 16, imeshinda mechi 14 na kupoteza mbili, haina sare ikifunga mabao 36 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.
Baada ya mchezo huo, Februari 5 mwaka huu Yanga itaikaribisha KenGold wakati Februari 6 Kagera Sugar ikiifuata Singida Black Stars katika mwendelezo wa ligi hiyo.