Dar es Salaam. Mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) yametajwa kuathiri biashara kati ya Tanzania na nchi hiyo huku Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) kikiiomba Serikali kuwapatia ulinzi waweze kushusha mizigo na kurudisha magari yaliyokwama nchini humo.
Inaelezwa kuwa malori karibu 100 yakiwa na shehena za mizigo yaliyotoka hapa nchini yamekwama DRC huku mengine yakishindwa kuvuka mpaka kutokana na hali ya usalama ilivyo.
Akizungumza na Mwananchi Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dossa amesema mapigano hayo yameathiri usafirishaji wa mizigo kwa kiasi kikubwa kwani DRC ndiyo uti wa mgongo wa shughuli zao kwa asilimia 70.
“Tumeathirika sana na kinachoendelea sasa, kwa mfano, magari yanayokwenda mashariki mwa Congo yameegeshwa Rwanda kwa sababu hawawezi kuendelea upande wa pili mpaka hali iwe shwari,” amesema Dossa.
Amesema hali hiyo inasababisha hasara kwa sababu magari yanaegeshwa yakiwa na mizigo bila kuendelea na safari hadi sehemu ambayo wanatakiwa kushusha, huku wakiwa hawajui jambo hili litachukua muda gani.
“Tunaomba Serikali ituangalie na ikiwezekana tupate hata ulinzi wa kwenda kushusha hiyo mizigo ya watu halafu tuone hili jambo linashughulikiwa vipi, lakini kiukweli tumeathirika sana, sana, sana na huu mgogoro unaoendelea,” amesema.
Amesema mpaka sasa magari yameegeshwa maeneo tofauti, ambapo katika mji wa Goma madereva kati ya 40 hadi 45 waliokuwa wamekwama, waliruhusiwa kuondoka na kuyaacha bila ulinzi wowote.
“Tunategemea tutakuwa na hasara kubwa sana kwa sababu umeacha mzigo kwenye yadi ya mtu hujui usalama wake ukoje, kwa sababu kuna magari mengine walivamiwa na watu na kuanza kuiba mizigo ya wateja, jambo ambalo lilifanya tuwaruhusu madereva watoke ili, wawe salama lakini mali ipo kule,” amesema Dossa.
Amesema kwa upande wa Rwanda takribani magari 45 yako katika mpaka huo, hali iliyofanya baadhi ya madereva kuruhusiwa kushusha mizigo katika maghala ya mpakani.
Japhet John, mmoja wa madereva wa malori amesema wiki iliyopita alilazimika kushusha mzigo mjini Kigali baada ya kuambiwa DRC hakuendeki, badala Goma alikokuwa anaupeleka.
“Uzuri mwenye mzigo alifanya utaratibu nikashusha pale Kigali, lakini kwa wenzangu mpaka sasa wamekwama huko, maana bao hawajashusha mzigo,” anasema John.
Anasema kwa sasa kazi za kwenda DRC zinapungua hususani za mashariki mwa nchi hiyo, lakini maeneo mengine kunaendeka lakini tayari matajiri wana wasiwasi wa kupeleka magari yao huko.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara nchini, Khamis Livembe amesema Dar es Salaam ni kama Dubai ya watu wa DRC na wamekuwa wakifanya manunuzi yao kwa kiasi kikubwa, lakini sasa mambo ni tofauti.
“Kinachoendelea kinatuathiri sana kama wafanyabiashara, kwani wao ni wateja wetu wakubwa, Dar es Salaam ndiyo kama Dubai yao, mizigo yao mingi inanunuliwa Kariakoo na hata kwenye maghala yetu na viwandani,” amesema Livembe.
Amesema hata wafanyabiashara wa Tanzania wengine wamewekeza DRC, akiwemo Bakhresa ambaye alifungua kiwanda.
“Mbali na kununua kutoka Dar es Salaam kuna wengine wanaagiza mizigo kutoka nje wanapitishia kwetu bandarini, hali hii itaathiri biashara zetu kwa kiasi kikubwa na uchumi kwa ujumla,” amesema.
HaIi hiyo imemwibua Dk Donath Olomi, mtaalamu wa uchumi na biashara, akisema katika kipindi kama hiki ni vyema kuangaliwa njia mbadala ambayo inaweza kutumika kufikisha bidhaa nchini DRC.
Akitolea mfano kwa wasafirishaji, amesema ni vyema kuangalia uwezekano wa kuwa wanashusha bidhaa mipakani, ili wale wanaohusika wawe wanazichukua katika eneo hilo kwenda nchini kwao.
“Lakini pia kama nchi ni lazima tuwe na taarifa sahihi ya kile kinachoendelea kule na kujua vihatarishi vilivyopo katika ufanyaji wa biashara. Kama nchi pia tunatakiwa kushiriki katika kutafuta suluhu au njia yoyote ambayo itarudisha amani ili biashara ziweze kuendelea,” amesema Dk Olomi.
Hata hivyo, mchumi mwingine Oscar Mkude amesema jambo hili si jipya kwa kuwa mara zote biashara zinazofanyika katika nchi hiyo zimekuwa zikifanyika kwa tahadhari.
Vilevile, amesema ni vyema katika kipindi hiki njia nyingine za kuingia DRC, ikiwemo inayopitia Zambia zitumike zaidi, akishauri kuongezwa kwa tahadhari kwani wahalifu wengine wanaweza kutumia machafuko hayo kutekeleza azma zao.
“Wahalifu wanaweza kutumia muda huu kupora mali na kuharibu mali na kwa njia hii wasafirishaji wanaweza kuathiriwa zaidi,” amesema Mkude.
Kufuatilia suala hili, Mkude ameshauri taasisi za kibiashara ikiwemo jumuiya ya wafanyabiashara wa malori kufutilia kwa karibu kujua jambo hilo litaathiri vyombo vyao kwa kiwango gani.
“Ikiwezekana waombe ulinzi wa kusindikizwa hadi eneo fulani ili walioagiza wachukue mizigo yao katika eneo hilo na wao warudi ili kuepusha athari zinazoweza kutokea, hili litasaidia usafirishaji mizigo kutoathirika kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Vilevile, Mkude amesema hali hii pia inaweza kuathiri kwa kiasi utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwani huenda wafanyabiashara ambao walikuwua wakiagiza mizigo yao nje kwasimama kwa muda, jambo ambalo linaloweza kuathiri matumizi ya bandari.
“Hili ni jambo la kawaida katika biashara kwani kuna kupanda na kushuka lakini jambo hili pia linaweza kuangaliwa na bandari kwa namna nyingine, ambayo inaweza kuimarisha huduma zake katika nchi nyingine wanazohudumia,” amesisitiza Mkude.
Taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) zinaeleza zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mapigano nchini DRC.
Pia, mashirika ya misaada yalisema kuwa hospitali zimefurika mamia ya watu waliojeruhiwa katika mapigano, wakiwemo watoto huku Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likisema usambazaji wa misaada ya chakula umesitishwa kwa muda ndani na karibu na mji wa Goma kutokana na mapigano hayo.
Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), uliofanyika juzi jijini Harare, Zimbabwe, viongozi hao walitoa salamu za pole kwa mataifa yaliyopoteza wanajeshi wake kwenye misheni ya kulinda amani (SAMIDRC) nchini DRC.
“Mkutano huo ulitoa salamu za rambirambi kwa nchi za DRC, Malawi, Afrika Kusini na Tanzania kwa wanajeshi waliopoteza maisha katika mashambulizi ya hivi karibuni huko Sake, Mashariki mwa DRC, wakiwa kwenye misheni ya SAMIDRC na wamewatakia waliojeruhiwa kupona haraka,” ilieleza taarifa rasmi ya viongozi hao baada ya mkutano wao juzi.
Alipotafutwa ili kuzungumzia salamu hizo kwa Tanzania, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alisema: “Naomba ongea na Waziri wa Mambo ya Nje.”
Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo hakupatikana mara moja wala kujibu ujumbe mfupi aliotumiwa.
Mwananchi lilimtafuta pia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mindi Kasiga ambaye pia alisema swali hilo aulizwe Waziri. Hata hivyo, Kasiga hakuwa na uhakika kama waziri huyo alikuwa amerejea nchini baada ya mkutano wa Harare.
Hata hivyo, Balozi Kasiga ameahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kuwasiliana na viongozi wake kuhusu suala hilo.
Baada ya kuuteka mji muhimu wa Goma, waasi wanaotajwa kuungwa mkono na Rwanda wanaendelea kusonga mbele kuelekea kusini, katika hatua inayotishia makabiliano kati ya Rwanda na Burundi. Huko Bukavu, raia wanaandikishwa kulinda mji.
Jeshi la DRC kwa msaada wa Jeshi la Burundi lilionekana likidhibiti shinikizo la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wanaotaka kupanua udhibiti wao wa mikoa ya mashariki mwa DRC katika mashambulizi ya wiki chache yaliyosababisha hofu ya mgogoro mpana wa kikanda.
Kwa mujibu wa Shirkika la Habari la Ujerumani (DW), waasi wa M23 waliiteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC ambao ni nyumbani kwa migodi ya dhahabu, coltan na madini ya shaba.
Waasi hao sasa wanaelekeza macho yao Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini na wanapiga hatua kuelekea lengo hilo huku matamanio yao yakiwa kuikamata Kinshasa.
Hata hivyo, Jeshi la DRC (FARDC) na washirika wake wamefanikiwa kuwadhibiti waasi hao, vyanzo vitatu, akiwemo Gavana wa Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi Sadiki waliliambia shirika la habari la Reuters.
Mmoja wa watu waliokuwa na taarifa za moja kwa moja kuhusu mapigano hayo, alisema kikosi cha takribani wanajeshi 1,500 wakiwemo wa DRC, Burundi na wapiganaji wanamgambo wa ndani kilitumwa kulinda mji wa Nyabibwe ulioko kilometa 50 kaskazini mwa Bukavu.
Wakazi wa Bukavu, ambao mara ya mwisho uliangukia mikononi mwa waasi mwaka 2004, walisema watu walikuwa wanajitayarisha kwa chakula, tochi na betri au kukimbilia mpakani mwa Burundi.
Raia walioajiriwa na mamlaka kutetea mji huo walikuwa wakifanya mazoezi kuzunguka uwanja wa michezo na kujipanga kwa ajili ya salamu za kijeshi.
“Tumeumia kwa muda mrefu kwa sababu ya wavamizi ambao ni majirani zetu,” alisema mwalimu wa hesabu Habamungu Mushagalusa, mmoja wa kundi la watu takribani 200 walioajiriwa.
“Tuko hapa kulinda ardhi yetu hadi kifo. Rwanda imepinga matokeo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba imetuma maelfu ya wanajeshi na vifaa nchini DRC kuisaidia M23.
Umoja wa Mataifa ulisema Alhamisi iliyopita kwamba kulikuwa na taarifa za vikosi vya Rwanda kuvuka mpaka na kuelekea Bukavu. Rwanda haikujibu mara moja ombi la kuzungumzia kauli ripoti hizo.