Mitazamo tofauti wanaorejea sokoni Kariakoo, mamia walizwa na madeni

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Shirika la Masoko Kariakoo kutoa orodha ya majina ya wafanyabiashara 1,520 wanaotakiwa kurejea kwenye Soko la Kariakoo, wafanyabiashara hao wametoa maoni tofauti, huku wengi wao wakifurahi kurejea. Hatua hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa ukarabati na ujenzi wa soko hilo lililoungua Julai 10, 2021 na kuteketeza mali na uharibifu mkubwa.

Baada ya tukio hilo, Serikali ilitoa Sh28.03 bilioni kwa ajili ya ukarabati na ujenzi mpya wa soko dogo, jumla likiwa na uwezo kubeba wafanyabiashara 1,906 kwa wakati mmoja.

Katika maandalizi ya kurejea kuanzia mwezi huu, Shirika la Masoko Kariakoo ambalo ndilo linalosimamia soko hilo, jana Januari 31, 2025, lilitoa orodha ya wafanyabiashara wanaostahili kurejea.

Kabla ya hapo, mchakato wa awali ulipingwa na baadhi ya wafanyabiashara waliodai kuwa viongozi wao hawakushirikishwa katika uhakiki wa majina ya wafanyabiashara hao na kuwa baadhi yalikuwa yameachwa huku mengine yakijirudia.

Julai 13, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza nao, pamoja na mambo mengine, aliamuru majina zaidi ya 819 yaliyokuw yamepitishwa kati ya wafanyabiashra 1,670 waliokuwepo kabla ya soko kuungua yaondolewe kwenye mfumo na kufanyike uhakiki.

Januari 30, 2025, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Hawa Ghasia alisema uhakiki huo mpya umekamilika na orodha ya majina ingetolewa kabla ya mwishoni mwa juma.

Jana Januari 31 orodha ya majina ya walio sifa na vigezo vya kurejea sokoni hapo iliwekwa hadharani ikionyesha waliachwa ni takriban 80.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Uhusiano Mkuu wa shirika hilo, Revocutus Kasimba ilisema orodha ya majina hayo yanapatikana kwenye tovuti ya Shirika <www.kariakoomarket.co.tz> na iIe ya Ofisi ya Rais-Tamisemi <www.tamisemi go tz>.

Katika taarifa shirika, Kasimba amesisitiza kwa wafanyabiashara 366 wanaodaiwa na shirika zaidi ya Sh358 bilioni, watapaswa kulipa madeni yao kabla hawajapatiwa nafasi za biashara.

Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao akiwemo Mwenyekiti wa Vigoli, Abdul Karim amesema anashukuru watu wake wote wamerudi kwa sababu ingewaumiza kama wangeachwa na kuingizwa wengine wapya.

Kuhusu suala la madeni, amesema ni vema Serikali ikafirikia kuwasamehe na “iwe kama wamelipwa fidia kutokana na ajali waliyoipata”.

 Amesema katika ajali hiyo, wengi walipoteza fedha na mali na wengine kwa miaka yote mitatu wakati soko linafanyiwa ukarabati, hawakuwa na shughuli yoyote wanayoifanya ya kuwaingizia kipato.

Mwenyekiti Soko Mzunguko, Rashid Kabwali amesema katika kitengo chao wafanyabaiashra wengi wamerudi na kuwa kati ya 297 waliokuwepo, saba pekee ndio majina yao hayajaonekana.

Hata hivyo, amesema moja ya makosa yaliyofanyika ni waliokuwa wanamiliki maeneo kutoandikisha wasaidizi wao badala yake wakaweka majina mapya ya ndugu zao.

“Hivyo kwa kuandikisha jina mtu ambaye hana analojua kuhusu Karikaoo, alipohojiwa na timu ya uhakiki, hakuweza kutoa majibu ya usahihi na kuonekana ni muongo,” amesema.

Kabwali ameomba sharti la kuwa na kitambulisho cha taifa kurudi sokoni hapo liangaliwe upya kwa kuwa wengi wao hawana, badala yake waruhusiwe kuendelea na biashara huku wakishughulikia suala hilo.

Kwa upande wake Hussein Rajab, mwenyekiti wa soko dogo, ameshauri majina hayo yachapishwe na kubandikwa kwenye mbao za matangazo ya masoko walikohamishiwa baada ya ajali kutokea.

Maeneo hayo ni masoko ya Karume, Kisutu na Machinga Complex.

“Hii ni kwa sababu kuna watu hawana simu janja wala hawawezi kuingia kwenye mfumo kupitia kompyuta, lakini pia itasaidia kuondoa usumbufu kwa viongozi kupigiwa simu mara kwa mara kuulizwa kama mtu jina lake lipo,” amesema.

Katibu wa soko kubwa, Juma Lusunga amesema hawezi kutoa maoni yake sasa akidai kuwa utaratibu waliokubaliana wa kurejesha majina hayo umekiukwa.

Anadai awali walikubaliana kabla ya orodha hiyo haijawekwa hadharani, viongozi wangeyahakiki kwanza, jambo alilodai kwamba halijazingatiwa.

Kutokana na hilo, Lusunga amesema kamati kuu ya soko inakutana kujadili hilo na watatoka na azimio.

Related Posts