UWT Mufindi yaonya wanaojipitisha kutia nia kabla ya wakati

Mufindi. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Mufindi, Marceline Mkini amewaonya baadhi ya wanachama wanaoanza kujipitisha kabla ya utaratibu rasmi wa chama kutangazwa.

Amewataka kuacha mara moja, la sivyo chama kitachukua hatua dhidi yao.

Onyo hilo amelitoa leo Jumamosi, Februari Mosi, 2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika viwanja vya Kata ya Changarawe, sambamba na utoaji wa msaada kwa kituo cha kulea watoto yatima cha Yerusalemu kilichopo Mafinga mjini.

Mkini amesema tayari wanazo taarifa kuna baadhi ya wanachama wameanza kupitapita kwenye kata zenye madiwani wa viti maalumu na kuanza kutangaza kwamba wanataka kuwania kabla ya wakati.

Mwenyekiti huyo amesema hali hiyo inasababisha kushuka kwa ufanisi wa kazi kwa madiwani waliopo kutokana na kuhamasisha ushindani usio wa lazima.

“Madiwani wa viti maalum bado ni viongozi wetu, hivyo tunapaswa kuwaenzi na kuwaheshimu kwa sababu muda wao bado haujaisha. Tabia ya wanachama kujitokeza kabla ya wakati inaleta mtazamo hasi kwa chama, kwani CCM haina sera ya kutangaza nia kabla ya muda wake kufika,” amesema Mkini.

Ameongeza kuwa wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali wanapaswa kusubiri mpaka chama kitangaze rasmi utaratibu wa kuchukua fomu.

Katika hatua nyingine, Mkini amesema katika maadhimisho hayo, UWT imetembelea kituo cha watoto yatima cha Yerusalemu na kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh500,000 ikiwa ni sehemu ya kujali na kusaidia jamii.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Saadani, Rozana Nzogo amepongeza kauli ya Mwenyekiti Mkini kwa kulaani vitendo hivyo, akisema vinaleta hofu kwa madiwani waliopo.

“Sisi madiwani bado tupo kazini na tunaendelea kutekeleza majukumu yetu. Uongozi wetu unamalizika Juni mwaka huu, hivyo wanachama wanapaswa kusubiri mpaka chama kitakapotangaza rasmi mchakato huo,” amesema Nzogo.

Related Posts