Mbeya. Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ikipitisha rasimu ya bajeti ya zaidi ya Sh 66.6 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, madiwani wamependekeza stendi ya mabasi ya Mji wa Mbalizi kufanyiwa maboresho na kilimo cha viazi kuwa zao la mkakati.
Wakizungumza leo Januari 31 katika kikao cha bajeti, baadhi ya madiwani wamesema stendi ya mabasi ya Mji wa Mbalizi haifanani na hadhi ya wilaya hiyo licha ya kuwa sehemu ya kuingiza fedha na kuchangia pato la ndani.
Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, Yona Ntunjilwa amesema stendi hiyo haiendani na hadhi ya wilaya hiyo, akieleza kuwa wakati wa mvua hali huwa mbaya ikiwamo maeneo ya vyoo.
“Stendi ile inaingiza fedha, lakini hali yake wakati wa mvua hali huwa ni mbaya hata sehemu ya vyoo, kuwepo njia maalumu ya kuweza kuiboresha” amesema Ntunjilwa.
Naye Diwani wa Kata ya Maendeleo, Daniel Nyamwale amependekeza kufanyiwa marekebisho ya bajeti ya zao la viazi kutoka Sh 800,000 na kupanda zaidi kutokana na uzalishaji ulivyo.
Pia ameshauri katika bajeti hiyo itengwe japo Sh 10 milioni kwa ajili ya maboresho kila shule iliyochakaa ili kuleta mabadiliko na ufanisi katika mwaka wa fedha wa 2025/26.
“Tunawapongeza wataalamu na ofisi ya mkurugenzi kwa bajeti nzuri, lakini upande wa kilimo cha viazi ifanyiwe mabadiliko na itengwe sh 10 milioni kwa kila shule iliyochakaa kufanyiwa maboresho” amesema Nyamwale.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ijombe, Mary Mbengale ameshauri bajeti inayogusa masuala ya vijana kutoegemea upande wa wasichana pekee akieleza kuwa hata watoto wa kiume wapo katika hatari.
“Katika bajeti hii inaonesha kutaja upande wa watoto wa kike kama ambao ndio wapo kwenye hatari, lakini tunasahau upande wa watoto wa kiume, ningeshauri watoto wote wajumuishwe pamoja” amesema Mary.
Akifafanua hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gidion Mapunda amesema kilimo cha viazi kitaboreshwa kuwa zao la kimkakati, huku kuhusu stendi ya Mbalizi akieleza kuwa wanaenda kulifanyia kazi kwakuwa bajeti haikutosheleza.
Mkuu wa Idara ya mipango na uratibu wa halmashauri hiyo, Fransisca Nzota amesema katika bajeti hiyo wamezingatia vipaumbele ikiwamo mishahara itakayotumia Sh 46 bilioni, Sh 12 bilioni kwenye miradi ya maendeleo na sh 6.6 mapato ya ndani.
Amesema katika vipaumbele hivyo kupitia mapato ya ndani, Sh 1.8 bilioni itaenda katika elimu, afya na miradi ya kiuchumi ikiwamo kuendeleza shamba la parachichi ambalo litawekewa vifaa ikiwamo lori na trekta.
Akifunga kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa Halmashauri hiyo, Devotha Chacha amesema kipindi hiki wakiendelea kuandikisha watoto, shule zote zisifukuze wanafunzi kwa sababu ya sare akibainisha kuwa mwanafunzi apokelewe.
“Nisisitize umuhimu wa chakula shuleni kwakuwa afya ni muhimu katika kukabiliana na magonjwa yoyote, mzazi akija na mtoto bila sare apokelewe hadi atakapopata sare” amesema.