Pacome amuangukia Gamondi, kocha amgomea

SAA chache kabla ya Yanga kuanza safari ya kuja uwanjani kiungo wa timu hiyo amewasilisha maombi kwa kocha wake ampe hata dakika 20 za mchezo huo.

Taarifa kutoka ndani ya Kambi ya Yanga ni kwamba baada ya kiungo huyo kufanya mazoezi vizuri ya siku tatu na kikosi hicho, akawasilisha maombi hayo kwa Gamondi, lakini akagoma.

Pacome tangu aumie dakika 20 za kwanza kwenye mchezo dhidi ya Azam amekosa mechi nne za mashindano zikiwemo mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns za Ligi ya Mabingwa,  moja ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Dodoma Jiji na ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate.

Mmoja wa mabosi wa Yanga ameeleza kuwa baada Pacome kuwasilisha maombi hayo Gamondi hakuonekana kuyakubali.

Wakati Yanga ikiingia baada ya kuwasili Uwanja wa Benjamin Mkapa, Pacome alikuwa mmoja wa wachezaji ambao waliukagua uwanja huo lakini kwenye kikosi hayupo hata kwenye benchi.

Kiungo huyo ameonekana akiwa mchangamfu huku akicheza muziki unaopigwa uwanjani hapo, ilhali mashabiki wa Yanga wakimshangilia kwa nguvu.

Pamoja na Pacome, kushindwa kuingia kwenye mchezo huu, beki Kouassi Attohoula 
Yao alikuwa mmoja wa wachezaji ambao wameukagua uwanja na ameanza mechi ya leo baada ya kukaa nje kwa muda akisumbuliwa na majeraha.

Related Posts