Dar es Salaam. Ukiwa umetimia mwezi mmoja tangu Bunge la Bajeti lianze vikao vyake, hoja tano za wabunge zimeibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na watu tofauti wamezizungumzia ama kwa kuzikosoa, kuzishangaa na wengine kuziunga mkono.
Hoja hizo ni pamoja na kuondolewa kwa fedha za kujikimu (boom) kwa wanafunzi wa elimu ya juu, tozo za bima ya afya, mawaziri kumpiga majungu mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na wito wa wabakaji wote kuhasiwa.
Hoja ya ongezeko la tozo kwenye laini za simu iliyotolewa na mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby kuwa Serikali ikate Sh2, 000 kila mwezi kama chanzo ya mapato ya Bima ya Afya kwa Wote, iliamsha mjadala mzito, ikipingwa vikali na wananchi.
Katika mchango wake, mbunge huyo alishauri wabunge na wafanyabiashara wakatwe Sh10, 000 kila mwezi kufanikisha lengo hilo.
Shabiby aliyasema hayo Aprili, mwaka huu wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, akitaka bima hiyo iwe na uhakika wa vyanzo vyake vya mapato.
Akitoa maoni yake kuhusu kauli hiyo, Dk Godfrey Malisa amesema ni masikitiko kwamba wabunge waliopo bungeni hawapo kutetea masilahi ya wananchi na mambo mengi wanayoyafanya ni usanii.
“Niliwahi kugombea uspika na nilipata nafasi ya kuzungumza na mbunge mmoja baada ya mwingine, nilitoka nikiwa na huzuni, kila kinachoonekana bungeni ni usanii, wabunge wa CCM na upinzani ukiwakuta wamekaa pamoja huwezi kujua ni wale waliopo bungeni,” anasema.
Mhadhiri huyo mstaafu amesema aliamini wabunge wa vyama vya upinzani wangelipinga suala la wabunge kutokatwa kodi, lakini nao wamekaa kimya jambo ambalo linadhihirisha nao wamewaacha wananchi.
Dk Malisa amehoji inawezekanaje mwakilishi wa wananchi kupendekeza ongezeko la kodi wakati nafasi ya ubunge wanayopambania ni kuwa na uwezo wa kuwatetea wananchi.
Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alishauri mikopo ya fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu maarufu kama ‘boom’ iondolewe kwa sababu wanafunzi wanaoipata hawasomi, wana nidhamu mbovu na wanalewa pombe.
Mbunge huyo alipendekeza kuwa badala yake wanafunzi wa vyuo walipiwe ada moja kwa moja kwa sababu wenye uhitaji wa kusoma ni wengi, lakini wanakosa nafasi hiyo kutokana na kukosa ada.
Kauli hiyo ya Getere imechambuliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie akisema wakati mwingine wabunge wakati wanazungumza wanakuwa na hamasa kupitiliza.
“Wanahamasika kiasi kwamba ule ujumbe wanaotaka kuufikisha unakosa manufaa. Unaposema ‘boom’ liondolewe, huwezi kueleweka na hicho kitu hakina manufaa kwa wanafunzi wengi,” anaeleza mchambuzi huyo wa siasa.
Amesema ujumbe ambao mbunge huyo alishindwa kuufikisha ni jinsi gani suala la maadili kumomonyoka linavyochangiwa na boom.
Hoja nyingine ni iliyoibuliwa na mbunge wa Konde, Mohamed Sais Issa ya kutaka kurejeshwa kwa utaratibu wa kuingia Zanzibar kwa pasipoti ili kudhibiti uingiaji wa watu visiwani humo wanaochukua ardhi ya Wazanzibari.
“Sasa hivi ukienda Zanzibar utakuta viwanja vimechukuliwa, miti imekatwa kulikuwa na zao la mikarafuu haliko tena, imebakia Pemba, nako linakwenda kuisha, minazi hakuna, tunaagiza nazi kutoka Mafia,” alisema na kuongeza kuwa hata ajira za watalii hawapati tena Wazanzibari, bali wageni, hivyo alitaka iwepo mkakati kuwalinda Wazanzibari.
Kutokana na mapendekezo hayo, Dk Loisulie amesema ujumbe wake ni shida iliyopo kwenye Muungano, hivyo amewachokoza walionyamaza.
Anasema mbunge huyo alitaka kuchochea hasira kwa watu ili Muungano uwe sawa kwa sababu upande mmoja ulinyamaza, lakini ameshindwa kutumia maneno sahihi kufikisha ujumbe wake na hatimaye kusababisha hamaki kwa watu.
Naye Abbas Mwalimu, alipozungumzia hoja hiyo, amesema mchango wa mbunge huyo ulijikita kwenye hoja ambayo imepitwa na wakati.
“Inawezekana aliyetoa hoja hiyo hakusoma mwongozo wa Agenda ya Afrika 2063 inayolenga kutoka nchi moja kwenda nyingine kusiwe na pasipoti, sasa iweje ndani ya nchi kuwe na pasipoti?” amehoji Mwalimu.
Mwalimu ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa, amesema hoja ya mbunge huyo pia inakinzana na maono ya waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hoja nyingine ni ya kuitaka Serikali ipeleke bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ili kuweka adhabu ya kuhasiwa kwa wanaume wanakutwa na hatia ya kulawiti au kubaka watoto, iliyotolewa na mbunge wa viti maalumu kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Shally Raymond wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Akizungumzia hoja ya mbunge huyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza amesema jukumu la kwanza la wabunge wanapaswa kuakisi matakwa na matamanio ya wananchi.
Amesema jukumu lao la pili ni utunzi wa sheria na kuisimamia Serikali, hivyo kama mbunge anapeleka bungeni jambo linalotoka kwenye misingi, anapaswa kupuuzwa.
“Mbunge akileta hoja inayoakisi udhaifu wa sheria, udhibiti na usimamizi wa Serikali, hatuwezi kumpuuza,” anasema kaiza akiongeza kwamba mbunge huyo ameonyesha kukata tamaa licha ya kuwepo kwa sheria.
“Jambo la kujiuliza kwa nini sheria hazitekelezwi, si kusema kuhasi watu hakuna sheria yake, kama mtu amefanya kosa anapaswa kusahihishwa,” anasema Kaiza.
Suala jingine lililochukua nafasi ni vita vya Luhaga Mpina, mbunge wa Kisesa na mawaziri, akiwatuhumu kwa kumpikia majungu kwa kuwa wameshindwa kujibu maswali au hoja anazozitoa bungeni.
Mpina alieleza hayo Mei 10 wakati akichangia mjadala wa kupitisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Nataka kuwaambia kwamba hakuna jambo loote ambalo ninalo ila tuna jambo moja la Watanzania kupata maendeleo, hakuna hiyana yeyote na huko wanakopeleka majungu wegine wajue ndiko tumekulia,” alieleza Mpina.
Akizungumzia hoja ya Mpina, Kaiza amesema hapaswi kupuuzwa kwa kuwa kila hoja anayoitoa ina vielelezo. Anasema anachozungumza mbunge huyo kijibiwe kwa hoja na si kupewa vijembe kama anavyodai, vinginevyo kutojibiwa kwake kwa hoja ni kumkosea.
“Kama anachozungumza Mpina ni mawazo ya watu wengi, kujibu hoja zake kwa kejeli hakusaidii, wanaomkejeli wanawaimarisha wanaowatuhumu,” anasema Kaiza.