Mipango ya Ramovic yammaliza Gamondi

MOTO wa kocha Sead Ramovic bado unaendelea kuwachoma wapinzani wa Yanga katika Ligi Kuu Bara baada ya Gusa Achia Twende Kwao kumbeba tangu ajiunge na timu hiyo kutoka TS Galaxy ya Afrika Kusini, akimfunika hadi mtangulizi wake, Miguel Gamondi.

Kocha huyo Mjerumani, ameupindua ufalme wa Gamondi baada ya Gusa Achia yake kumlipa katika mechi sita za Ligi Kuu ikiwa ni nusu ya mtangulizi wake, akiwa ameshinda zote na kukusanya mabao ya kutosha hadi sasa.

Katika mechi sita za Ligi Kuu Bara tu zimetosha kuanza kuonyesha namba bora kutoka kwa Ramovic aliyevuna jumla ya pointi 18 na mabao 22 huku akiruhusu wavu wake kuguswa mara mbili tu hadi sasa akiwa ndio kwanza amecheza nusu ya mechi alizocheza Gamondi kabla ya kufurushwa klabuni.

Kwenye mechi 10 za kwanza msimu huu Yanga ikiwa chini ya Gamondi ilishinda mechi nane mfululizo kabla ya kupoteza mbili na huku kikosi hicho kikivuna pointi 24 na mabao 12 tu na yenyewe kufungwa manne. Yanga ya Gamondi ilianza kufungwa na Azam kwa bao 1-0 kisha kulala 3-1 mbele ya Tabora United na uzalendo ukawashinda mabosi wa klabu hiyo waliomfurusha na kumleta Ramovic.

Ramovic bado anaonekana mbabe dhidi ya Gamondi hata msimu wa kwanza ndani ya mechi sita za kwanza akianza na moto mkali lakini kikosi hicho cha msimu uliopita, kilifunga jumla ya mabao 18 huku akipoteza mchezo mmoja dhidi ya iliyokuwa inaitwa Ihefu (Singida Black Stars).

Ramovic namba zake bora hazijaishia hapo tu kwenye mabao ya kufunga bali hata katika kujilinda kwani ikmeruhusu mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa, lakini mechi nyingine tano Yanga ilipata ushindi bila nyavu zao kuguswa. Iliifunga Namungo 2-0, ikailaza Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Kagera Sugar kila moja kwa mabao 4-0, huku ikiinyosha Fountain Gate kwa mabao 5-0.

Kitu cha kushangaza ni kwamba makocha hao wawili wameutulia ukuta ule ule ulio chini ya kipa Diarra Djigui na mabeki wa kati Dickson Jon na Ibrahim Bacca, japo kwa mabeki wa pembeni wamekuwa wakibadilishana.

Kwenye mechi 10 ambazo Gamondi aliishia na Yanga msimu huu, alishinda tano ugenini na tano nyumbani wakati Ramovic akicheza mechi mbili pekee ugenini na nne nyumbani na mjerumani huyo bado anasubiriwa kwenye mechi zingine za ugenini.

Akizungumzia kiwango hicho ndani ya mechi hizo sita, Ramovic alisema furaha yake ni kuona maendeleo makubwa kwa wachezaji wake lakini akasema bado kikosi chake kina nafasi kubwa ya kufunga mabao mengi zaidi. Ramovic alisema kuhusu uimara wa safu yake ya ulinzi unatokana na jukumu la kukaba sio la watu wa ulinzi pekee na kuanzia washambuliaji, viungo na hata mabeki wote wanatakiwa kusumbuka kuutafuta mpira haraka wakati ukiwa kwenye miliki ya wapinzani.

“Nafurahi kuona wachezaji wanaimarika kadiri ya siku zinavyosogea, kasi, nguvu na juhudi uwanjani inazidi kuwa kubwa kwa kiwango kinachovutia, tunafunga mabao lakini najua hatuwezi kutumia kila nafasi ila tunaweza kufunga mabao zaidi,” alisema Ramovic na kuongeza;

“Ukitazama kama tuna safu ya ulinzi nzuri ni sawa mabeki wanafanya vizuri lakini hapa ningependa kuiangalia timu nzima namna tunavyopoteza mpira wote tunapambana kuuondoa kwenye umiliki wa wapinzani na hili limekuwa likifanyika vizuri.”

“Nawapongeza wachezaji wamecheza vizuri pamoja na kukutana na timu ambayo ilikuwa na mpango wa kujilinda zaidi na kutumia mipira ya kushtukiza wameweza kuwapita na kufunga mabao zaidi ya matatu,” alisema Ramovic.

Akizungumzia kumtumia Israel Mwenda eneo la winga alisema amefanya hivyo kutokana na kasi aliyonayo na alitamani kuona anawakimbiza wapinzani kwa kasi kupitia pembeni wakisaidiana na mabeki wa pembeni ambao wana uwezo wa kukimbia.

“Natamani kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, nikifanikiwa kwenye hilo nitakuwa na urahisi katika machaguo yangu, nampongeza Mwenda kwa dakika chache alizocheza kafanya vizuri.”

Akizungumzia mchezo ambao watakuwa wenyeji wa KenGold, Ramovic alisema mipango ni kuendeleza ubora walionao ili kuendelea kukusanya pointi kwa kila mchezo ulio mbele yao kwa lengo la kuhakikisha wanafikia lengo la kutetea taji.

Related Posts