Rwanda Yaikubalia SADC Kujadili Mzozo Wa DRC – Global Publishers



 

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rwanda Jumapili imekubaliana na pendekezo la kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku Tanzania ikitangaza pia kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa katika mapigano ya hivi karibuni.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma wiki iliyopita na kutishia kusonga mbele hadi mji mkuu wa Kinshasa.

Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) siku ya Ijumaa ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki “kuamua juu ya suluhu la hali ya usalama nchini DRC.”

Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda “imekubaliana na pendekezo hilo” na kuongeza katika taarifa kwamba “imekuwa ikiunga mkono kila mara suluhisho la kisiasa kwa mzozo unaoendelea huko DRC.”

Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria mkutano wa dharura wa SADC, lakini Rais wa DRC Felix Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya mtandao. Rwanda sio mwanachama wa SADC.

Viongozi wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali pamoja na wawakilishi wao wakati wa Mkutano Maalum wa SADC kuhusu hali ya usalama katika sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo Januari 31, 2025.

Mkutano wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi wa Afrika Kusini na Malawi kuuawa katika mapigano karibu na Goma, ambako walikuwa wanahudumu katika kikosi cha nchi wanachama wa SADC (SAMIDRC). Kikosi hicho kilikuwa na jukumu la kuisaidia DRC kupata amani na usalama wa kudumu.

Jumapili, Tanzania ilitangaza kwamba wanajeshi wake wawili katika kikosi cha SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya hivi karibuni. Msemaji wa jeshi Gaudentius Ilonda alisema wanajeshi wengine wanne walijeruhiwa na wanapewa matibabu huko Goma.

Wanajeshi 13 wa Afrika Kusini, raia watatu wa Malawi na mmoja wa Uruguay waliokuwa wanahudumu katika kikosi cha MONUSCO na SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya DRC.


Related Posts