Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Subira Mwaifunga, ametaja masharti magumu katika sheria ya kuasili watoto kuwa chanzo cha kuendelea kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto mtaani.
Mwaifunga ametoa kauli hiyo bungeni leo, Februari 3, 2025, wakati akiuliza swali la nyongeza, ambapo ameeleza kuwa watu wengi wanashindwa kuwaasili watoto kutokana na mlolongo wa sheria.
Katika swali la msingi, Mwaifunga ameuliza ni lini Serikali itapeleka mabadiliko ya Sheria ya Kuasili Watoto bungeni, kwani iliyopo imepitwa na wakati.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamisi, amesema Serikali imefanya mabadiliko ya Sheria ya Mtoto kuhusu masuala ya uasili wa mtoto kwa kuboresha mifumo na kuimarisha taratibu za kuasili nchini kupitia Sheria ya Ulinzi wa Mtoto ya Mwaka 2024.
“Mabadiliko hayo yamepitishwa kupitia kikao cha 16 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa sasa yanatumika katika baadhi ya vituo vya kulelea watoto, ikiwemo kile cha Makao ya Watoto Kikombo (Dodoma),” amesema Mwanaidi.
Naibu waziri huyo amesema Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sera na sheria mbalimbali kwa kadri itakavyohitajika, kwa lengo la kuimarisha ulinzi na ustawi wa mtoto, huku ikitoa nafasi zaidi kwa watu wanaotaka kuwaasili watoto.
Endelea kufuatilia Mwananchi.