Mwabukusi: Kushirikiana na Serikali sio kulamba asali

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema ushirikiano wa chama hicho na Serikali hauna maana kuwa amelamba asali, bali wanatekeleza wajibu wa kuwahudumia Watanzania.

Kauli ya Mwabukusi inajibu mitazamo tofauti inayoibuliwa katika mitandao ya kijamii, baadhi wakikosoa hatua ya TLS kushirikiana na Serikali katika utoaji huduma za kisheria kupitia Msaada wa Kisheria wa Samia (Samia Legal Aid).

Kadhalika, ukosoaji mwingine uliohusisha madai ya kulamba asali ni hatua ya chama hicho kupewa gari na Wizara ya Katiba na Sheria.

Akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini leo, Jumatatu Februari 3, 2025, jijini Dodoma, Mwabukusi amesema wanaposhirikiana na Serikali si kwamba wanalamba asali, kwa sababu TLS ni bodi ya kisheria na haki.

Katika maadhimisho hayo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ni mgeni rasmi, Mwabukusi amesema kupongeza kwa haki na kushiriki kwa pamoja kutalijenga Taifa kwa kuwahudumia Watanzania.

“Tunaposhirikiana na Serikali hatulambi asali, kwa sababu tunapata changamoto watu wanapoona tunashirikiana na Serikali wanafikiri tunalamba asali.

“TLS sio kikundi cha magaidi, ni bodi ya kisheria, kwa hiyo sehemu ya kuonya tutaonya kwa haki, sehemu ya kupongeza tutapongeza kwa haki, na sehemu ya kushiriki pamoja tutashiriki kulijenga Taifa letu na kumhudumia Mtanzania,” amesema.

Kuhusu gari walilopewa na Wizara ya Katiba na Sheria, amesema linawasaidia kuwafikia Watanzania na wapo tayari kupokea msaada mwingine wowote kutoka kwa yeyote ili kuwawezesha kuwafikia wananchi.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, chama hicho hakina fedha za kutosha kuwahudumia wananchi, hivyo kinahitaji kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kinatekeleza wajibu wake.

“Yeyote anayetuletea msaada tutaendelea kupokea. Popote tutakapohitaji kwenda kushirikiana na mtu kufanya kazi tutaenda kushirikiana, sio rushwa, sio kutuziba mdomo, tutajitambua. TLS ina wajibu, haifanyi biashara.”

Amewajibu pia wale wanaohoji kwanini siku hizi haongei kama alivyokuwa kabla ya urais wake wa TLS akisema; “Watu wanauliza Mwabukusi huongei tena, umelamba. Ukishakuwa kiongozi huongei tena, unatenda. Kiongozi huongei, unatenda.”

Awali, Mwabukusi ametaja changamoto zinazoathiri taaluma hiyo nchini kuwa ni pale wanaposimamia kesi za watu wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa, zikiwamo za mauaji, akisema uwakili ni kazi kama kazi nyingine.

“Unakuta malipo yanaanza Sh100,000 hadi Sh300,000, ambayo haitoshi hata kuandaa shajara tu, lakini mtu anatakiwa kumtetea mtu anayepaswa kunyongwa au aachiwe.

“Kwa hiyo, wakili anakuwa kwenye dilemma (njiapanda) kiasi cha kushindwa kufanya kazi yake kwa weledi,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni wananchi kutoelewa taaluma yao.

“Hata kama mtu hapendwi na kijiji kizima, kama mimi ni wakili, yule mtu ana haki ya kuwakilishwa nami… Mawakili wamekuwa wakiunganishwa na wateja wao na kuwekwa lockup (mahabusu),” amesema Mwabukusi.

Related Posts