Othman: Mabadiliko ni lazima, tupambane kuingia Ikulu 2025

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud, amesema mabadiliko ni lazima, hivyo amewataka wanachama, wafuasi na wananchi wanaokiunga mkono chama hicho kupambana katika uchaguzi mkuu ujao ili kuhakikisha wanakiweka madarakani na kuikomboa Zanzibar kutoka katika janga la umasikini.

Amesema licha ya kufanyiwa vitimbwi katika chaguzi zilizopita, havijawakatisha tamaa, na kuwataka wanachama na wafuasi wake kupambana kuhakikisha katika uchaguzi wa madiwani, wabunge, wawakilishi na rais, chama chao kinaingia madarakani.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, huko Mkajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja, alipozungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kukiimarisha.

“Ndugu zangu, katika uchaguzi unaokuja lazima tupambane sana. Walidhani (bila kuwataja) tumevunjika moyo, tumeanguka na hatuwezi kuamka tena, lakini tunawaambia nguvu tunazo. Wanachokitafuta wao ni madaraka tu, lakini hawana dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi na changamoto zao,” amesema.

Amesema, licha ya kujipambanua kwa kujenga miradi na maghorofa makubwa, bado hali ya maisha ya wananchi haijabadilika.

“Lakini mtu mwenye njaa, kusoma ghorofani unamsaidia nini?” amehoji.

Amesema bado kuna nia ya kuwadhulumu wananchi kama ilivyoshuhudiwa katika miaka iliyopita, na kwamba baadhi ya watu wanataka kuingia madarakani kwa nguvu.

Hata hivyo, Othman, ambaye ameweka nia ya kuwania urais iwapo ACT-Wazalendo itampitisha, amesema hawataweza kufanikisha dhamira yao ya kuingia madarakani iwapo wananchi hawatajitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.

“Safari inaanza sasa kwenye uandikishaji wa daftari la mpiga kura. Usipochukua hatua sasa, tutateseka maisha yetu yote,” amesema.

Hata hivyo, Katibu wa Kamati Maalumu ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Khamis Mbeto, amejibu kauli za chama hicho akisema utekelezaji wa ilani wa CCM umewafanya wapinzani wao wakose hoja za msingi, hivyo wanatafuta huruma ya wananchi.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, maarufu kama Babu Duni, amesema Wazanzibari ‘wananuka’ njaa.

“Ndugu zangu, tatizo la Wazanzibari ni moja tu – njaa. Kuna umasikini unanuka hapa. Mnahitaji kubadilika angalau mpate shibe. Zanzibar hatujawahi kushiba. Shida yetu ni shibe, hayo mengine yanafuata, haya majengo na shule,” amesema.

Duni amesema, “Ndugu zangu, tunahitaji mabadiliko. Mkikosea mwaka 2025, tumekwisha.”

Amehoji ni kwa jinsi gani amani inaweza kupatikana bila haki, akisema kuwa mnyonge akinyanyaswa, inafika wakati anataka kujilinda.

“Siku zote mwenye nguvu ndiye anayeanzisha fujo. Mnyonge, kama Babu Duni, yeye anajitetea tu. Kwa hiyo, wenye nguvu ndio wanataka fujo. Sisi ACT tutajitetea tu,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, ambaye pia ni Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui, amewataka wananchi waache woga na washirikiane kuinusuru Zanzibar.

Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, amesema chama hicho kinaposema kinataka kuinusuru Zanzibar, maana yake ni kuiondoa kwenye ufisadi na unyang’anyi wa rasilimali.

“Maana nyingine ni kuondoa mawakala na madalali wa kushikilia mamlaka kamili ya Zanzibar, kwani mfumo uliowekwa na kulindwa ni kwa ajili ya kuwanufaisha wachache,” amesema.

Related Posts