TIMU ya Junguni United imeilaza Chipukizi United ya Mjini Chake Chake kwa kichapo cha mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Zanzibar uliopigwa kwenye Uwanja wa FFU.
Junguni ndio iliyokuwa ya kwanza kuliona lango la Chipukizi lililofungwa na Salim Othuman Chubi katika dakika ya 22 kipindi cha kwanza kwa pigo la moja kwa moja (free kick) baada ya mchezaji mmoja wa Junguni kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari nje kidogo ya 18 ya lango la Chipukizi.
Iliwachukua dakika tatu Junguni kupata bao la pili kwa shuti kali la mguu wa kulia lililomshinda mlinda mlango ambalo liliwekwa wavuni na Sharif Mohammed Rashid katika dakika 25.
Mabao hayo hayakuwakatisha tamaa Chipukizi na katika dakika ya 36 ilijipatia bao lililofungwa na Abdullah Mahmud Nassor baada ya kumalizia mpira uliowaacha mabeki wa Junguni kujisahau na kumuachia Abdullah kuujaza mpira huo kimiani.
Na kwa kuwa jitihada haiondoi kudra, Chipukizi walijipatia bao la pili na la kusawazisha lililofungwa na Haroun Thomas Soko katika dakika ya 54.
Junguni ilipata bao la tatu katika dakika za jioni lililofungwa na Salim Othman Chubi baada ya kuwalamba chenga mabeki na kipa wao.
Mchezo huo umekuwa ni kama wa kulipa kisasi baada ya mechi ya awali baina yao, Junguni kulala kwa bao 1-0.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha wa Chipukizi, Mohamed Ayoub alisema ni matokeo ya mchezo kufungwa na watajipanga kwa ajili ya mchezo mwengine.
Alisema bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata na kuondosha upungufu uliojitokeza katika mchezo huo.
“Tukubali tumefungwa. Kikubwa ni kuangalia upungufu uliojitokeza na kwenda kuufanyia kazi ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo ujao,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Junguni, Sultan Issa alisema ushindi huo ulitokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kwenye kikosi chao.
Alisema wakati ligi ikiwa imesimama walikuwa wanafanya mazoezi ya haja ili kuona mzunguko huu hawafanyi makosa kwa vile mzunguko uliopita hawakufanya vizuri.
Alisema huo ni mkakati waliojiwekea kuwa kila timu watakayokutana nayo washinde waweze kujiweka kwenye mazingira salama ya kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
“Sisi tulidhamiria tufanye vyema kwenye mzunguko huu wa pili baada ya kufanya vibaya mzunguko uliopita, tumejipanga vizuri, hatutaki tufanye makosa, tunataka kila mchezo tushinde,” alisema Sultani.