Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kesho, Jumanne, Februari 4, 2025 anatarajiwa kupokea tuzo ya ‘The Gates Goalkeepers Award’ kama kielelezo cha matokeo makubwa ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 nchini.
Matokeo hayo yamepatikana chini ya uongozi wake, kutokana na ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022.
Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, wakati akitoa taarifa ya upokeaji wa tuzo hiyo ya Rais, iliyoandaliwa na Taasisi ya The Gates Foundation, mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za wizara, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mhagama amesema tukio hilo linafanyika nje ya Marekani, nchini Tanzania kwa mara ya kwanza, na Rais Samia ndiye kiongozi wa kwanza kupokea tuzo hiyo kwa Bara la Afrika, jambo lililochochewa na uongozi wake mahiri ulioleta mafanikio makubwa nchini, hususan katika sekta ya afya.
Amesema kuwa mafanikio hayo yamesababisha mataifa makubwa duniani kutambua mchango wake.
Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na mikakati iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kutokana na utashi wa kisiasa chini ya uongozi wake, kuweka mazingira wezeshi ya kisera pamoja na kuimarisha huduma za rufaa kwa akina mama na watoto.
“Rais Samia ameongeza bajeti ya kuimarisha huduma, ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kusogeza huduma za dharura za uzazi karibu na wananchi kwa kujenga vituo zaidi ya 530 vya upasuaji wa kutoa mtoto tumboni,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama ameipongeza Taasisi ya The Gates Foundation kwa kutambua na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
“Kwa namna ya kipekee, tunatambua jitihada za Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan, katika mapambano dhidi ya vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
“Hivyo, tuna kila sababu ya kumpongeza na kutembea kifua mbele kwa jinsi Rais anavyotung’arisha nje ya mipaka ya nchi yetu,” amesema Waziri Mhagama.
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa mwaka 2012 vifo vitokanavyo na uzazi vilikuwa 432 kwa kila vizazi hai 100,000. Hata hivyo, takwimu za mwaka 2015/16 zilionyesha kuongezeka kwa idadi hiyo hadi 556 kwa kila vizazi hai 100,000.
Lengo la Serikali lilikuwa kupunguza vifo hivyo kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 292 ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo, ilifanikiwa kuvishusha zaidi na kufikia 104 mwaka 2022.