Siku moja yampa jeuri Minziro

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’ amesema kusogezwa mbele siku moja kwa mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji kumempa nafasi ya kuendelea kuijenga timu kisaikolojia baada ya kukamilisha maandalizi ya kimbinu.

Pamba Jiji itakuwa ugenini Alhamisi hii kuikabili Dodoma Jiji mchezo ambao awali ulipangwa upigwe kesho Jumatano na timu hiyo ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 16, ikishinda mbili, sare sita na vipigo nane ikikusanya pointi 12.

Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro alisema kimbinu amekamilisha kila kitu na ana matumaini makubwa na kikosi chake kufanya vizuri mzunguko wa pili kutokana na maingizo mapya na yupo tayari kwa ushindani baada ya kufanyia kazi mapungufu.

“Unajua mpira unamambo mengi ukiondoa mbinu za uwanjani nje ya uwanja mambo ni mengi pia hivyo nakaa na wachezaji wangu kwaajili ya kuwajenga ili wafanye kazi yao ya uwanjani zaidi na kuachana na mambo ya nje ya uwanja huku tukielekezana mambo madogo madogo kuelekea kumkabili mpinzani wetu,” alisema Minziro, nyota wa zamani wa Polisi Zanzibar na Yanga aliyeongeza;

“Tunarudi kwenye ushindani kupambania nafasi ya kucheza tena msimu ujao wachezaji wangu kwa asilimia kubwa wapo tayari na ninamatumaini makubwa na wachezaji wangu sambamba na maingizo mapya baada ya kufanyia marekebisho makosa waliyoyafanya mzunguko wa kwanza.”

“Tunarudi mzunguko wa lala salama tukiikabiri Dodoma Jiji ugenini tunatarajia mchezo mgumu na wa ushindani kutokana na wapinzani wetu pia kuhitaji matokeo ili waweze kujiweka kwenye nafasi nzuri,” alisema Minziro na kuongeza;

“Sisi pia tunazihitaji pointi tatu muhimu kutokana na nafasi tuliyopo na tayari nimefanyia kazi mapungufu na kuongeza wachezaji kwenye nafasi ambazo zilipelea mzunguko wa kwanza, naamini tutakuwa bora.”

Minziro akizungumzia maandalizi kwa jumla alisema yalikwenda vizuri walifanya kwa vitendo wakicheza mechi moja ya kirafiki na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na wachezaji wangu wanaendelea kuimarika siku hadi siku matarajio kuanzia benchi ya ufundi na wachezaji ni makubwa malengo ni kuhakikisha msimu ujao tunacheza tena ligi kuu na haturudi tulipotoka.” alisema.

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa CCM Kirumba, jijini Mwanza Agosti 24 mwaka jana zilishindwa kufungana kwa kutoka suluhu.

Related Posts