Waitara aliamsha bungeni, adai TRA Sirari wanatembeza vipigo

Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (Mara), Mwita Waitara amedai gari la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) limemsukuma mtaroni kijana ambaye amefariki dunia na kwamba maofisa mamlaka hiyo wanadai kodi kwa kupiga watu.

Waitara ametoa madai hayo leo bungeni Jumatano Mei 15, 2024 kwa kuomba mwongozo wa Spika, akitumia kanuni ya 76, akidai TRA Sirari inadai kodi kwa kupiga vijana.

Hata hivyo, mwongozo wa kiti cha Spika umesema hauna nyaraka wala maelezo yoyote kuhusu madai hayo ya Waitara na kwambakimepokea na kitarudi kwake.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kikao cha Bunge , Deo Mwanyika amemshauri Waitara kuwa anaweza kupeleka swali hilo kwa Serikali bungeni.

“Natumia kanuni ya 76, naomba mwongozo wa kiti chako, wakati napata majibu ya Serikali ya swali namba 344, nilisema utaratibu unaotumika kukusanya kodi kule Sirari umeleta madhara makubwa kwa vijana wetu na kuna mauaji.

“Nimesema Jumamosi watu wa TRA wakiwa wanamfukuza kijana mwenye bidhaa za mifuko ya plastiki ‘ilimpushi’ (sukuma) kijana na akaingia kwenye mtaro na amefariki dunia, lakini tumeshuhudia mpaka watu wanapigwa risasi.

“Sasa kama tunatoa taarifa za mauaji kwa watu wetu, na vizuri tukisema watu wa Tarime tupewe uzito wa pekee kwa sababu inaweza ikafikia mahali watu wakaanza kuchukua sheria mkononi.

‘Je, ni sahihi kutafuta kodi ya Serikali kwa njia ya damu? Kwamba unakusanya kodi kwa kuua watu na sio mara moja watu wetu wa TRA kule Sirari, kwenye magari yao wana mipini ya jembe, wanapiga vijana wa Tarime, mheshimiwa Mwenyekiti.

“Kwa hiyo nataka Serikali itoe kauli juu ya hili jambo, ili tuone kwamba wanachukua hatua. Wanachukua kodi kistaarabu, na kama kuna mtu ana magendo akamatwe na achukuliwe hatu za kisheria bila kuleta madhara kwa watu wetu na kujenga chuki dhidi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, lakini pia na TRA. Naomba mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti,” alisema Waitara.

Mwenyekiti wa Bunge Mwanyika amesema “Mheshimiwa Waitara hapa kiti hakina ‘document’ (nyaraka) yoyote na maelezo yoyote ya kuweza kuthibitisha hilo jambo unalolisema, kwa hiyo nalipokea na tutarudi kwenu au kwako kadiri kanuni zinavyoturuhusu. Na nakushauri ungeleta swali la msingi ili upate majibu ya Serikali.”

Related Posts