Magugu maji bado kikwazo usafiri wa vivuko Kigongo-Busisi

Mwanza. Wingi wa magugu maji ndani ya Ziwa Victoria umeendelea kukwamisha shughuli za usafirishaji wa abiria na magari katika eneo la kivuko cha Kigongo-Busisi, kutokana na injini za vivuko kupata hitilafu.

Kutokana na tatizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kwa mara nyingine jana, Februari 2, 2025, alilazimika kuwaruhusu watembea kwa miguu na magari kupita juu ya daraja la muda linalotumiwa na mkandarasi anayeujenga daraja la JPM.

Uamuzi huo ulitokana na vivuko vya MV Mwanza na MV Misungwi vilivyokuwa vinatoa huduma kutembea taratibu, hivyo kusababisha foleni ya magari, abiria, na mizigo.

Hii ni mara ya pili kwa mamlaka za Serikali kuruhusu watembea kwa miguu na magari kutumia daraja hilo la muda, baada ya kulazimika kufanya hivyo Januari 26, 2025.

Eneo la kivuko cha Kigongo-Busisi ni lango kuu la usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Kigoma, na nchi jirani za Rwanda, Burundi, na Uganda.

Akizungumza na Mwananchi jana, Februari 2, 2025, alipofika kwenye kivuko hicho mara baada ya kupigiwa simu na abiria waliokaa zaidi ya saa sita wakisubiri kuvuka, Mtanda amesema uongozi wa Serikali Mkoa wa Mwanza umewasiliana na Wizara ya Ujenzi kuomba injini mpya itakayofungwa kwenye vivuko vipya vinavyojengwa.

Mtanda amesema ofisi yake pia imewasiliana na wizara inayohusika na masuala ya mazingira kuleta wataalamu kufanya utafiti wa namna ya kumaliza tatizo la magugu maji katika eneo hilo.

“Poleni kwa usumbufu ndugu zangu wananchi, tuwe na subira kidogo hali itatengemaa, tayari hatua za msingi nimefanya,” amesisitiza mkuu huyo wa mkoa alipozungumza na wananchi hao.

Huku akisimamia upitaji wa abiria na magari, mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa, “Haya magugu maji yanakuja… yanaingia kwenye injini, kwa hiyo ule mchanganyiko unatokea unaingiza maji na mafuta kwenye injini. Vivuko vinashindwa kufanya kazi na injini zake zinaharibika, ndio changamoto iliyoko hapa.”

Mmoja wa abiria aliyekuwa akielekea mkoani Geita, Richard Mahizo, amesema alikata tamaa ya kuvuka kutokana na wingi wa watu na magari, hivyo kuruhusiwa kupita kwenye daraja la muda lililowapa ahueni.

Magugu maji yameendelea kuwa changamoto katika Ziwa Victoria, ambapo Februari 2017, nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Sudan, Rwanda, Ethiopia, na Burundi kupitia makatibu wake wa wizara za maji walitia saini maazimio 23 yatakayosaidia kutunza na kulinda ziwa hilo, likiwemo azimio la kuondoa magugu maji.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza alipozungumza bungeni Januari 31, 2025, Serikali imeanza kudhibiti magugu maji ziwani humo, ikiwemo ofisi ya Makamu wa Rais kuandaa na kutekeleza Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka 2019-2029.

Related Posts