Wafanyabiashara wa Kariakoo waanza kuchukua fomu za kurejea sokoni

Dar es Salaam. Mamia ya wafanyabiashara waliokidhi vigezo vya kurejea soko la Kariakoo wamejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuanza tena biashara sokoni hapo, huku baadhi yao wakitaja changamoto ya kutojua kodi wanayotakiwa kulipa.

Hatua ya kurejeshwa kwa wafanyabiashara hao inakuja baada ya kukamilika kwa ukarabati wa soko hilo lililoungua Julai 10, 2021 na kuteketeza mali.

Ukarabati wa soko hilo ulianza Januari 2022 na Serikali ilitoa Sh28.03 bilioni ikihusisha pia ujenzi mpya wa soko dogo lenye ghorofa sita.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2025, Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia, alisema soko hilo hadi sasa limekamilika kwa kiasi kikubwa na vitu vichache vilivyobaki haviwezi kuwa kikwazo kwa watu kuanza kufanya biashara.

Leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, Mwananchi imeshuhudia wafanyabiashara wakichukua fomu zilizokuwa zikitolewa na shirika hilo, zikiwa zimepita siku tatu tangu walipoweka hadharani orodha ya majina ya wenye vigezo vya kurejea. Fomu hizo zilianza kutolewa saa 3 asubuhi katika ukumbi wa Anaurtoglou, jijini Dar es Salaam.

Katika orodha hiyo, wafanyabiashara 1,520 ndio wenye sifa ya kurejea sokoni kati ya wafanyabiashara 1,670 waliokuwepo awali kabla ya soko kuungua. Kigezo kimoja ni kuwa na kitambulisho cha uraia au namba ya mlipakodi au vyote kwa pamoja.

Akieleza malengo ya utoaji fomu hizo, Ofisa Uhusiano wa Shirika hilo, Revocatus Kasimba, amesema ni kupata taarifa sahihi za wafanyabiashara na kuziweka kwenye kanzi data ya shirika kwa kuwa za awali ziliteketea na moto.

Pia kujua mtu anaweza kulipa kiasi gani, jambo litakalowasaidia shirika kujua linafanya biashara na watu wa uwezo wa kiasi gani.

Ofisa huyo amesema kazi ya utoaji fomu inafanyika kwa siku tano (Jumatatu hadi Ijumaa) na wiki ijayo itawapa nafasi kuwasikiliza wale ambao hawajaona majina yao kwenye orodha iliyotolewa.

“Kinachofanyika hapa ni wafanyabiashara kuchukua fomu kujaza taarifa zao binafsi za aina ya biashara waliokuwa wanaifanya pale mwaka 2021 kabla ya tukio la moto kutokea, taarifa ambazo pia zitasaidia katika kuliendesha soko,” amesema Kasimba.

Baadhi ya wafanyabiashara wakizungumzia mchakato huo wamesema ni mzuri ila shida ipo kwenye yanayotakiwa kujazwa kwenye fomu, ambapo sahemu ya kodi haijataja kiwango gani.

“Katika hiyo fomu kuna sehemu unaulizwa upo tayari kulipa kodi ambayo shirika imepanga, sasa unajiuliza unajibu nini hapo kwani hujajua hata kiasi cha kodi yenyewe, walau wangeweka tukajipima kama tunaweza au la,” amesema Ashura Daudi, Mwenyekiti wa Wanawake Soko la Kariakoo.

Akitoa ufafanuzi kwa changamoto hiyo, Kasimba amesema kuna kiasi cha kodi kinachotakiwa kulipwa na kueleza wamefanya hivyo kwa kusudi kwanza kutowapa faida washindani wao ambao nao wanafanya biashara ya kupangisha majengo.

“Mbali na kutowapa faida washindani wetu, lingine ni kutaka kujua aina ya biashara atakayokuwa anaifanya mfanyabiashara, ambapo baada ya kujaza fomu hiyo, ataingia moja kwa moja kwenye mfumo wa Tausi na huko ndio atakuta na kiasi gani cha fedha anapaswa kulipa,” amesema Kasimba.

Amewaondoa hofu kuhusu kipengele hicho cha kodi akisema hata mwenyekiti wa bodi alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika soko hilo, hivyo si rahisi viwango vya mwaka 2021 ndivyo vitumike kwa sasa.

Mfanyabiashara Ziada Kindimba amelalamikia muda mfupi waliopewa kurejesha fomu hizo, yaani siku moja, akisema wanakosa muda wa kutosha kutafakari mikataba hiyo.

Hata hivyo, Kasimba amesema sio lazima warudishe kesho, kwani ndani ya wiki hii nzima watakuwa wakishughulika na mambo ya fomu, hivyo mtu anaweza kurudisha muda wowote ndani ya siku hizo.

Bakari Mitole, aliyeachwa katika orodha hiyo, amesema kabla ya kuungua sokoni alikuwa na meza mbili katika soko la wazi.

Hata hivyo, amesema wakati wa uhakiki wa awali walielezwa watapatiwa meza moja moja hata kama mtu alikuwa na meza tano, jambo ambalo walilikubali na kufuata taratibu zote ambazo walielekezwa na mamlaka.

“Sasa ni jambo la kushangaza ndugu mwandishi, uhakiki wa kwanza ulivyofanyika na majina kutolewa, jina langu halikuwepo. Nikajipa matumaini kwa uhakiki wa pili nako hola.

“Ninaomba Serikali isikilizie kilio chetu hiki kwa kuwa tulivumilia wakati wote soko likiwa kwenye ujenzi na wengine mitaji hadi kukata, leo hii linarejea tunachwa. Ni jambo la kusikitisha,” amesema mfanyabiashara huyo.

Akijibu hilo, ofisa uhusiano wa soko amesema wametoa nafasi ya kuwasikiliza wafanyabiashara waliokosa kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo.

Related Posts