Mahamat Deby anavyobeba mustakabali wa Chad

Kishindo cha Mei 10, mwaka huu kimewaacha wananchi wa Chad midomo wazi baada ya kutangazwa kwa Mahamat Idriss Deby Itno, maarufu kama Mahamat Kaka kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitarajiwa kutangazwa Mei 21, hata hivyo yametangazwa mapema kuliko ilivyotarajiwa, jambo ambalo limeibua maswali na kuwafanya wananchi kuingia barabarani kupinga ushindi huo.

Mahamat ni ofisa wa jeshi aliyegeuka kuwa mwanasiasa nchini Chad na sasa ndiye Rais wa saba wa Taifa hilo la Afrika Magharibi kuanzia mwaka huu. Ni mmoja wa watoto wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Idriss Deby.

Alizaliwa Aprili 4, 1984 huko N’Djamena, Chad. Yeye ni mwanasiasa na ofisa wa kijeshi. Chad imekuwa na marais saba tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1960, marais hao ni François Tombalbaye (1960–1975), Felix Malloum (1975–1979), Goukouni Oueddei (1979–1982), Hissene Habre (1982–1990), Idriss Deby (1990–2021), Albert Pahimi Padacke (Kaimu Rais wa muda mfupi kufuatia kifo cha Idriss Deby, mwaka 2021) na Mahamat Deby.

Mahamat alitwaa madaraka kama Rais wa Baraza la Kijeshi la Mpito (TMC) Aprili 20, 2021, wakati baba yake, Idriss Deby, alipouawa vitani akiwaongoza wanajeshi katika mashambulizi ya Kaskazini mwa Chad.

Rais Deby alifariki kutokana na majeraha aliyopata katika mapigano na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Hii ilitokea mwishoni mwa wiki na tangazo la kifo chake lilitolewa siku moja baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi kuonyesha kuwa angechaguliwa kwa muhula wa sita madarakani.

Idriss, ambaye alikuwa na umri wa miaka 68 wakati wa kufa kwake, alikaa zaidi ya miongo mitatu madarakani na alikuwa mmoja wa viongozi waliotawala kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Alifika mstari wa mbele, umbali wa mamia ya kilomita Kaskazini mwa mji mkuu, N’Djamena, kutembelea wanajeshi waliokuwa wakipigana na waasi wanaojulikana kama Fact (the Front for Change and Concord in Chad).

Uteuzi wa Mahamat Deby ulisababisha hisia tofauti ndani na nje ya Chad. Baadhi ya watu walipokea habari hiyo kwa furaha, wakiona fursa ya mabadiliko chanya na uongozi mpya. Hata hivyo, wengine, walionyesha wasiwasi wao kuhusu mchakato wa uchaguzi na mamlaka ya familia ya Deby.

Mahamat alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 61 ya kura zote zilizopigwa. Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa mpinzani wake, Succes Masra, ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 18 ya kura. Masra na chama chake, Les Transformateurs, walipinga matokeo hayo na kuwasilisha rufaa kwenye Baraza la Katiba.

Chama cha Les Transformateurs kilibainisha idadi kubwa ya dosari wakati wa upigaji kura, hususan kukataliwa kuingia katika vituo vya kupigia kura au kushiriki katika shughuli za kuhesabu kura, ukosefu wa vifaa vya uchaguzi na masanduku ya kura yaliyochukuliwa na wanajeshi. Mahamat alitangazwa mshindi rasmi wa uchaguzi wa urais.

Hata hivyo, ghasia na maswali kuhusu udanganyifu wa uchaguzi yaliharibu hesabu ya kura, ambayo ilitangazwa mapema kuliko ilivyotarajiwa. Ghasia zimeendelea huko Chad, na jeshi lilipelekwa mitaani kutuliza ghasia hizo.

Hali ya sasa nchini Chad iliendelea kuwa tete, na vikosi vya usalama vilipelekwa mitaani na huduma za mtandao wa intaneti zilikatwa sehemu nyingi za nchi.

Uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya hofu na kulikuwa na ripoti kuhusu udanganyifu siku ya uchaguzi.

Wanasiasa 10 ambao walikuwa wakigombea urais waliondolewa na Baraza la Katiba kwa sababu ya kile kilichotajwa kuwa ni “udanganyifu”.

Kuapishwa kwa Mahamat kulifanyika kwa haraka baada ya kifo cha baba yake na kuzua maswali mengi kuhusu uhalali wake na mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Serikali ya Chad iliona hatua hii kama njia ya kudumisha utulivu katika muktadha wa mgogoro uliokuwapo kuhusiana na mashambulizi ya makundi ya waasi pamoja na hali tete ya kisiasa katika eneo la Sahel.

Mahamat, kama kiongozi mpya, amejaribu kujiweka katika hali ya kuungwa mkono ndani ya nchi yake na kimataifa kwa Serikali yake mpya.

Ametoa ahadi za kufanya mageuzi ya kisiasa na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Chad. Hata hivyo, wakosoaji wameeleza shaka yao kuhusu uhalali wa utawala wake na ikiwa ataweza kushughulikia changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi zilizokita mizizi nchini humo.

Mahamat ana wake watatu, wa kwanza ni wa kabila la Zaghawa nchini humo. Mwaka 2010, Mahamat alioa mke wa pili kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na binti wa Abakar Sabone ambaye ni waziri wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, mshauri wa Michel Djotodia ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la waasi la Wapiganaji wa Haki za Afrika ya Kati.

Inaaminika kuwa Mahamat na mke wake wa pili wana watoto watano. Mke wa tatu, Dahabaya Oumar Souni, ni mwandishi wa habari na mshauri wa vyombo vya habari ambaye sasa anachukuliwa kuwa mke wa Rais wa Chad.

Kwa miongo kadhaa, familia ya Deby imekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Chad na historia yao imejaa matukio ya kisiasa, mafanikio na changamoto.

Kuanzia utawala wa Rais Idriss Deby ambaye alitawala nchi kwa miongo mitatu, hadi uteuzi wa mwanaye, Mahamat kama rais wa mpito, familia hii imekuwa kitovu cha nguvu za kisiasa nchini humo.

Rais Deby alipata umaarufu kama kiongozi aliyepindua Serikali ya Hissene Habre mwaka 1990. Baada ya kupata madaraka, aliendelea kuongoza nchi hiyo kwa miaka 30, akipambana na changamoto za kisiasa na kijamii kando na kutetea usalama wa nchi yake katika eneo la Sahel.

Wakati wa utawala wake, familia yake ilijitokeza kama moja ya zenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Chad.

Watoto wake walipewa nyadhifa muhimu katika Serikali, jeshi na taasisi za umma wakati ndugu zake na marafiki walipata nafasi kubwa za uongozi. Familia ya Deby imekuwa ikishikilia madaraka muhimu katika taasisi za Serikali na Jeshi la Chad. Hii imesababisha madai ya ukoo wa kifamilia katika siasa za nchi hiyo huku baadhi wakilalamika juu ya ukosefu wa uwazi na demokrasia.

Hata hivyo, wakati mwingine familia ya Deby imekuwa ikichukua hatua za kushirikisha sehemu zingine za jamii, ikiwa ni pamoja na makabila mbalimbali na vyama vya kisiasa. Hii imekuwa njia ya kudumisha utulivu wa kisiasa na kuzuia upinzani mkali dhidi ya utawala wao.

Chad inakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa zinazoweza kumkwamisha Mahamat katika juhudi zake za kudumisha utawala. Mojawapo ni jinsi ya kuunda Serikali inayojumuisha makundi mbalimbali ya kikabila na kisiasa ili kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Pia, kuna haja ya kushughulikia mgogoro wa kibinadamu unaosababishwa na vita na ukosefu wa usalama katika eneo la Sahel ambalo limeathiri maisha ya raia wa Chad. Serikali inahitaji kufanya kazi na jamii za kimataifa ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Hata baada ya kifo cha Rais Deby, familia yake bado inaonekana kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Chad.

Kutangazwa kwa Mahamat kuwa Rais kumekuwa na athari kubwa katika mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo, na hii imezua mjadala mkali kuhusu demokrasia na uwazi.

Changamoto kubwa zinazokabiliwa na familia ya Deby ni pamoja na kukabiliana na madai ya upinzani na kuungwa mkono na umma na kushughulikia masuala ya maendeleo na usalama nchini Chad.

Mustakabali wa familia hii na ushawishi wake katika siasa za nchi utategemea jinsi wanavyoshughulikia changamoto hizi na kujenga mifumo imara ya utawala.

Mustakabali wa Chad unaonekana kuwa na changamoto nyingi, lakini pia kuna fursa za kujenga msingi imara wa utawala wenye ufanisi na wa kidemokrasi.

Kwa kujenga mifumo imara ya utawala na kushirikiana na jamii za kimataifa, Chad inaweza kufanikiwa kuleta utulivu na maendeleo kwa wananchi wake.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa Mahamat Deby na Serikali yake kuchukua hatua madhubuti za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kuimarisha misingi ya utawala bora na kuhakikisha maendeleo ya nchi hiyo.

Wakati huohuo, jumuiya ya kimataifa inahitaji kusaidia Chad katika juhudi zake za kujenga utawala imara na wenye ufanisi.

Chad imekuwa na historia ya siasa iliyogawanyika na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi. Baada ya kupata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1960, Chad ilianza kushuhudia machafuko ya kisiasa na mizozo ya kikabila.

Mwaka 1975, Hissene Habre aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi na baadaye kuendesha utawala wa ukandamizaji mkubwa wa kisiasa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Habre aliondolewa madarakani kwa mapinduzi uasi yaliyoongozwa na Idriss Deby mwaka 1990 ambaye aliendelea kuwa Rais hadi kifo chake Aprili 2021.

Wakati wa utawala wake, Chad iliendelea kujihusisha katika migogoro ya ndani na ya kikanda, pamoja na kupambana na makundi ya waasi na ugaidi.

Mahamat ameendeleza utawala wa familia ya Deby ambao umedumu kwa miaka 34.

Hata hivyo, Chad inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na miundombinu duni, migogoro ya ndani na waasi kaskazini mwa nchi na ugaidi unaosababishwa na makundi ya Waislamu wenye msimamo mkali katika eneo la Sahel na Bonde la Ziwa Chad.

Related Posts