HAKUNA ubishi juu ya kiwango bora kilichoonyeshwa na Yanga msimu huu na kufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ambao umechagizwa na wachezaji mbalimbali katika kikosi hicho akiwemo Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, aliyerithi mikoba ya Nasrreddine Nabi aliyetimka baada ya msimu uliopita kumalizika.
Gamondi, raia wa Argentina huu ni msimu wake wa kwanza kuifundisha Yanga na imefanikiwa kubeba ubingwa ukiwa ni wa tatu mfululizo kwa Wananchi wakifikisha makombe 30 tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza mwaka 1965.
Wakati kocha huyo anatua Jangwani aliikuta timu hiyo ipo kwenye kilele cha furaha ya kuchukua ubingwa wa ligi, Kombe la Shirikisho (FA) na kufika fanali Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya mtangulizi wake kuipatia mataji sita Yanga katika misimu miwili aliyodumu Jangwani, lakini kuna rekodi zinambeba Gamondi mbele ya Nabi katika kipindi alichodumu klabuni hapo, huku Nabi pia upande mwingine katesa. Mwanaspoti inakuletea utamu wa rekodi zao.
UBINGWA BILA STRAIKA TEGEMEO
Ndani ya misimu miwili ambayo Yanga imebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa na Nabi yaani 2021/2022 na 2022/23 ilikuwa na idadi kubwa ya washambuliaji ambao uwezo ulikuwa unafanana, ukimuondoa Fiston Mayele aliyekuwa juu ya wenzake.
Yanga ilikuwa na Heritier Makambo, Yacouba Sogne, Wazir Junior na Mayele na kila mmoja alitoa mchango wake kikosini.
Baadaye iliachana na wachezaji wengi kikosini na kubaki na Mayele, kisha ikamuongezea Kennedy Musonda na kumpandisha Clement Mzize kutoka kikosi cha vijana, lakini pale alipokosekana Mayele mashabiki waliingiwa na hofu kwa kuwa ndiye aliyekuwa nyota tegemeo katika utupiaji nyavuni.
Hata hivyo, Gamondi alipotua Jangwani msimu huu licha ya kuwakuta Mzize, Kennedy Musonda na kumsajili Hafiz Kounkon kisha Joseph Guede waliotegemewa kuziba nafasi ya Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri, matarajio hayakwenda ilivyopangwa na hivyo kocha huyo akageuzia matumaini kwa viungo ambao wamembeba.
Hivyo Gamondi amempindua Nabi kwa kugeuza matumaini ya timu kuwategemea wachezaji wa eneo la kiungo badala ya ushambuliaji kukiwa na Maxi Nzengeli, Aziz KI, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua wanaoibeba timu katika utupiaji mabao nyavuni
MATUMIZI YA AZIZ KI
Katika msimu wake wa pili kufundisha Yanga, Nabi alikuwa akimtumia zaidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ eneo la kiungo mshambuliaji na Aziz KI hakuwa bora kama ilivyo sasa ambapo anaisadia timu hiyo kufunga mabao.
Gamondi aliwahi kusema kwenye moja ya mahojiano yake kuwa ni muumini wa kuwatumia viungo jambo ambalo limemfanya kumpa muda mwingi wa kucheza KI na kuonyesha kiwango bora.
Msimu uliopita Aziz alimaliza na mabao tisa kwenye michezo 30, lakini msimu huu umeonekana kuwa bora zaidi kwake chini ya Gamondi baada ya kutupia kambani mabao 15 na asisti nane Ligi Kuu Bara.
USAJILI MPYA
Msimu huu Yanga imesajili wachezaji sita ikiwa ni wanne wa kigeni na wawili wa ndani na wote wamekuwa wakicheza na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Pacome, Yao Kouassi, Gift Fred na Joseph Guede ni nyota wa kigeni waliotua Jangwani ambao wanafanya vizuri Ligi Kuu, huku wazawa Nickson Kibabage na Shekhan Hamis wamekuwa wakipata nafasi za kucheza pia.
Nabi alikuwa na viungo wawili wenye asili moja ya kiuchezaji Aziz na Fei Toto ambao hakuwatumia vizuri jambo ambalo lilimfanya kumchezesha mmoja na mwingine kukaa benchi au kumbadilisha eneo.
KUIFUNGA SIMBA 7-2
Kama kuna msimu wa furaha zaidi kwa Wananchi, basi ni huu wa 2023/24 baada ya kuchukua ubingwa na kuwafunga watani wao, Simba mabao 7-2 nyumbani na ugenini.
Gamondi pia amefanikiwa kuzifunga baadhi ya timu mabao mengi ikiwemo Simba sababu iliyoifanya kuachana na makocha wake wawili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akiondoka baada ya kichapo cha mabao 5-1, huku Abdelhak Benchikha akisepa alipofungwa tu mabao 2-1.
Kwa Nabi ndani ya misimu miwili aliyofundisha Jangwani ilishuhudia Simba kwenye ligi akishinda mara moja kwa bao 1-0 lililofungwa na Zawadi Mauya, Julai 03, 2021 kisha akatoka sare mbili na kufungwa mara moja Aprili 16, 2023 na Wekundu hao kwa mabao ya Henock Inonga na Kibu Denis.
MASHINDANO YA CAF
Katika mashindano ya kimataifa Nabi alishindwa kuipeleka Yanga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ilikotolewa hatua za awali na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1 na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambako alifanikiwa kuifkisha fainali na kuondoshwa na USM Algier iliyobeba ubingwa.
Chini ya Gamondi, Yanga imecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kutolewa na Mamelodi Sundown kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.
Ingawa Nabi aliiwezesha Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, pia kwa kuiwezesha Yanga kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Gamondi amefanikiwa kuvunja rekodi ya miaka 25 ya Yanga kutocheza makundi kwenye michuano hiyo baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho 1998.
POINTI NA MABAO
Hadi ligi inamalizika Yanga chini ya Nabi katika msimu wake wa pili ambao alianza na kikosi hicho tangu mwanzo wa msimu ilikusanya pointi 78 ikifunga mabao 61 na kuruhusu 18, ikishinda michezo 25 sare tatu na kupoteza miwili dhidi ya Simba na Ihefu.
Lakini, msimu huu zikiwa zimesalia mechi tatu, Yanga imekusanya pointi 71 ikifunga mabao 60 na kuruhusu 13 ikishinda mechi 23, sare mbili na kupoteza mbili dhidi ya Ihefu na Azam zote kwa vichapo vya mabao 2-1.