Yanga yatua Maniema ikimsaka mbadala wa Aziz KI

MISIMU miwili iliyopita, mashabiki wa Yanga walidhani ni ndoto kuuzwa kwa mshambuliaji Fiston Mayele. Lakini Pyramids wakaweka mzigo mezani mwamba akasepa kiroho safi.

Na sasa kituo kinachofuata ni kwa Azizi Ki. Presha ya kumuuza kiungo huyo imeanza kukolea ndani ya Yanga na Mwanaspoti limeambiwa kwamba mezani kuna jina la mbadala wake ambaye limeonyeshwa.

Yanga imevuta waya pale DR Congo kwa kiungo mmoja ambaye alikuwa pacha uwanjani wa staa wa Jangwani, Maxi Nzengeli wakati anaichezea Maniema.

Mabosi wa Jangwani wanajipanga kumuuza Aziz KI baada ya msimu huu kumalizika ikitajwa klabu moja ya Algeria imefika bei kutaka kumnunua na sasa zimeanza hesabu za kupata mbadala wake kwani tayari wameshajua ni kiasi gani watalipwa na wameanza kukipigia bajeti.

Mabosi wa Yanga wamerudi Union Maniema ya DR Congo wakionyesha kuvutiwa na huduma ya kiungo wa timu hiyo, Agee Basiala.

Yanga iliwahi kumtaka Basiala msimu mmoja uliopita ikivutiwa wakati huo akicheza kama kiungo wa pembeni, lakini baadaye akabadilishiwa nafasi na kuchezeshwa kiungo wa kati mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho. Hapo Maniema ndipo alipotoka Nzengeli na wakati akiwa hapo, alichukuliwa kama pacha wa Basiala wote wakiifanya Maniema kuwa tishio kabla ya Yanga kumnyakua fundi huyo na sasa inataka kumbeba na mwingine.

Basiala anajua kutoa pasi za mwisho na kuchezesha timu, lakini pia anatupia sana mipira ya adhabu kama Aziz KI.

Mwanaspoti linafahamu kwamba bosi wa Yanga alipokuwa Morocco hivi karibuni kwa majukumu yake kama mwenyekiti wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA), alikutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Maniema, Guy Kilongozi na wawili hao waliteta juu ya Basiala.

Hatua rahisi kwa Yanga ni kuwa, haihitaji kutumia nguvu kubwa kumpata mchezaji ndani ya Maniema kwa kuwa tayari ilishatengeneza uhusiano mzuri kutokana na ukaribu wa viongozi wa timu hizo.

Endapo Yanga itampata Basiala itakuwa imefanya usajili mzuri kwani kiungo huyo ana nguvu ya kumudu kukimbia eneo kubwa uwanjani kama alivyo Nzengeli.

Chanzo cha ndani Maniema kimeliambia Mwanaspoti: “Yanga wanamtaka Agee (Basiala) kweli. Tupo nao kwenye mazungumzo na bado hayajakamilika. Lakini, unajua wale ni rafiki zetu wakati wowote kitu kutoka kwao kinaweza kumalizika kwa haraka hakuna shida.

“Unajua sio mara ya kwanza Yanga kumtaka Agee wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu, hata wakati rais wao, Said (Hersi) alipokuja hapa Congo (DRC) alimuangalia sana na kuuliza mengi. Naona sasa hivi wanasema tena wanamtaka.”

Related Posts