Watu 67 Wauawa Katika Shambulizi Sudan – Global Publishers



 

Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa, takriban watu 67 wameuawa Jumapili katika shambulizi la mizinga lililofanywa na Vikosi vya RSF huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini- magharibi mwa Sudan.

Taarifa ya ya jeshi la Sudan imeongeza kuwa miongoni mwa waliouawa kwenye shambulio hilo ni wanawake 30, watoto 17 na wanaume 20.

Taarifa hiyo imesema: “Mapigano yalitokea kati ya SAF na RSF katika sehemu ya mashariki ya mji wa El Fasher Jumapili na Jumatatu, ambapo SAF iliharibu magari kadhaa ya kivita ya RSF.”

Mapigano ya silaha kati ya SAF na RSF yameongezeka hivi karibuni katika maeneo matatu ya mji mkuu Khartoum, Jimbo la Gezira katikati mwa Sudan, na karibu na mji wa El Fasher wa magharibi mwa Sudan.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, Jeshi la Anga la Sudan lilianzisha mashambulizi ya anga Jumatatu likilenga eneo la kusini mwa Khartoum linalodhibitiwa na vikosi vya RSF.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa, Jeshi la Sudan( SAF) hivi karibuni limepata mafanikio na ushindi kubwa katika Jimbo la Khartoum baada ya kuteka maeneo kadhaa muhimu kutoka mikononi mwa vikosi vya RSF. Lakini RSF bado inashikilia ngome muhimu huko Nile Mashariki.

Tovuti ya habari ya Sudan Tribune imeripoti kwamba Abdallah Hussein, kamanda mkuu wa RSF katika jimbo la Gezira, aliuawa Jumatatu pamoja na askari wenzake kadhaa katika mashambulizi ya anga nje kidogo ya mji wa Al Kamlin, kaskazini mwa jimbo la Gezira. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, SAF inasonga mbele kuelekea Al Kamlin, ngome ya mwisho ya RSF huko Gezira.


Related Posts