Dar es Salaam. Licha ya ukubwa wa hadhi na heshima ya Global Gates Goalkeeper Award aliyotunukiwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ukweli ni kwamba hiyo siyo tuzo yake ya kwanza katika maisha yake ya urais.
Mkuu huyo wa nchi amewahi kutunukiwa tuzo lukuki za ndani na nje ya nchi, zinazotambua mchango wake katika uendelezaji wa sekta mbalimbali na uongozi wake tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021.
Samia aliyekuwa Makamu wa Rais kuanzia Novemba 5, 2015, aliapishwa kuwa Rais kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Tangu ameingia madarakani, tuzo mbalimbali zimemiminika kwa Rais Samia kwenye sekta za utalii, miundombinu, utawala bora na demokrasia kitaifa na kimataifa, zote hizo zikionyesha kutambua uwezo na uongozi wake.
Kubwa zaidi ni ile aliyokabidhiwa jana Jumanne, Februari 4, 2025 ya Global Gates Goalkeepers inayotambua uongozi na mchango wake katika kuimarisha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.
Kwa mujibu wa Rais wa Dawati la Usawa wa Jinsia la Gates Foundation, Dk Anita Zaidi, chini ya uongozi wake Tanzania imepunguza vifo vya wazazi kwa zaidi ya robo tatu na watoto kwa asilimia 80.
Tuzo ya Gates Goalkeeper imeasisiwa na Taasisi ya Bill and Mellinda Gate mwaka 2017 (sasa Gates Foundations) ikilenga kuchochea na kuonyesha juhudi za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) kwa watu mbalimbali.
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva ni miongoni mwa viongozi waliowahi kupokea tuzo hiyo mwaka 2024, huku Ursula von der Leyen Rais wa Umoja wa Ulaya akiwa kiongozi mwingine aliyewahi kuipokea.
Tuzo hiyo pia aliwahi kupewa Waziri Mkuu wa India, Narendra Mondi, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN-Women), Phumzile Mlambo-Ngcuka.
Dk Anita amesema Rais Samia ameonesha kuguswa na athari za afya ya uzazi na kuzitafutia ufumbuzi wake kwa vitendo.
Amesema ulipofika mwaka 2021, Rais Samia akaapishwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke na ameonyesha anafahamu kwa undani madhara ya kupuuza masuala ya uzazi.
Katika uongozi wake, amesema Serikali ilianza kufanya juhudi mbalimbali ikiwamo kuongeza miundombinu na vifaa kwa ajili ya uzazi katika vituo vya afya na kutoa suluhisho kwa wazazi.
Rais Samia alikabidhiwa tuzo hiyo jijini Dar es Salaam kisha akapanda ndege kwenda Dodoma ambako alipokewa na mamia ya wananchi waliojipanga kando ya barabara ya uwanja wa ndege wakiwa na mabango kadha wa kadha.
Baadhi ya mabango hayo yaliyokuwa na picha ya Rais Samia yalikuwa yameandikwa ‘hongera bimkubwa’, tulilolitaka wajumbe wamelifanya mwaka 2025 ni wako mama, kazi umemaliza hatudai, tunakuahidi ushindi wa kishindo.
Rais Samia amesema tuzo hiyo ina maana kubwa kwa sababu anadhani dunia imefahamu juhudi za Tanzania katika huduma za afya na anaitoa kwa wahudumu wa sekta ya afya na Watanzania kwa ujumla.
Mwaka mmoja baada ya kushika wadhifa huo, Mei 25, 2022, Rais Samia alitunukiwa Tuzo ya Babacar Ndiaye. Hatua hiyo ilitokana na maelezo kuwa, dunia imetambua jitihada anazozifanya katika ujenzi wa miundombinu bora nchini.
Aghalabu Tuzo ya Babacar Ndiaye, hutolewa kwa watu mashuhuri duniani walioonyesha dhamira ya kuendeleza sekta ya miundombinu ya usafiri.
Mwaka huohuo baadaye, Rais Samia alipokea tuzo nyingine kutoka Taasisi ya Afrimma ya Dallas nchini Marekani. Tuzo hiyo ilitambulishwa kuwa ya uongozi wa kimageuzi Afrika 2022, ikilenga kutambua mchango wake katika uendelezaji wa sanaa nchini.
Mwaka 2022 ulikuwa wa baraka kwa Rais Samia, kwani alipokea tuzo nyingine nchini Nigeria ya Pyne Africa Award, akitambuliwa kuwa kiongozi bora, muwajibikaji katika kuendeleza sekta ya utalii.
Tuzo hiyo ilifuatiwa na aliyopewa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi siku hiyohiyo, kutambua mchango wake katika kukuza sekta ya utalii visiwani humo.
Bado tuzo ziliendelea kumiminika ndani ya mwaka huo wa 2022, akipokea Tuzo ya Mani iliyoambatana na ile ya Rais wa Dhahabu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Desemba 11, 2022 taasisi ya International Iconic ilimtunuku Rais Samia kuwa mshindi wa Tuzo ya Muongoza Watalii Bora.
Tuzo hiyo ilitokana na kutambua na kuthamini mchango wake na kuwa mhusika mkuu kwenye filamu ya The Royal Tour iliyotangaza vivutio vya utalii vya Tanzania hivyo kuchochea ongezeko la idadi ya watalii nchini. Itakumbukwa Tanzania ilivuna idadi kubwa ya watalii wakati huo dunia ikitoka kwenye maumivu ya Uviko-19.
Mwaka huohuo, Rais Samia alitunukiwa tuzo ya heshima katika kutambua mchango wake wa utekelezaji wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira ya ‘Nyumba ni Choo’.
Mwaka 2023 ulikuwa wa pekee kwa Rais Samia, baada ya kukabidhiwa tuzo ya pongezi kwa maridhiano ya kuboresha na kuimarisha demokrasia yenye amani, upendo na mshikamano nchini.
Upekee wa tuzo hiyo siyo kwa sababu ilitolewa 2023, bali aliyeitoa ni Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) na aliyekabidhi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Katika mazingira ya kawaida isingetarajiwa kwa chama kikuu cha upinzani ambacho aghalabu huikosoa Serikali, kumpa tuzo mkuu wa nchi anayetokana chama cha siasa.
Lakini, hatua hiyo ilifanyika miezi michache baada ya uamuzi wa Rais Samia kuunda kwa tume mbalimbali za maridhiano na kuridhia kuketi na vyama vya upinzani kujadili uendeshaji wa siasa kwa namna ya kuheshimiana, kutoaminiana na kudumisha demokrasia.
Katika nyakati hizo hizo, ndipo zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa liliondolewa na hatimaye vyama vyote vikawa na uhuru sawa wa kufanya mikutano ya kisiasa.
Ndani ya mwaka huo pia, Rais Samia alitunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kutetea, kulinda na kuimarisha haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Tuzo hiyo alitunukiwa na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Pia, alipokea tuzo maalumu kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere aliyeikabidhi kwa niaba ya wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Tuzo hiyo alikabidhiwa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nane Nane ambayo Kitaifa yalifanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti, 2023.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pia, ilimzawadia Rais Samia tuzo maalumu ya kutambua mchango, maono na uongozi wake katika kuifanya elimu kama nguzo kuu ya maendeleo ya nchi.
Baadaye mwaka 2024 alitunukiwa Tuzo ya Ubinadamu na Shirika la Msalaba Mwekundu, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuthamini haki muhimu za binadamu ikiwemo afya.
Rais Samia pia, alikabidhiwa Tuzo ya Care Impact, nchini Marekani iliyolenga kutambua uongozi wake unaoleta mabadiliko chanya kwenye jamii.