Kocha mpya Yanga alivyotua Dar

WAKATI maswali yakiwa mengi kuhusu kuondoka kwa kocha wa Yanga, Sead Ramovic aliyekuwa kocha wa Singida Black Stars, Hamdi Miloud na msaidizi wake Nassim Anisse wametua kwenye Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, mapema asubuhi hii ili kutua Jangwani.

Ikumbukwe kuwa, makocha hao wote ni wageni katika Ligi ya Tanzania, huku Ramovic akitua Yanga Novemba mwaka jana, ilihali Hamdi akiingia Singida Desemba pia mwaka jana.

Ramovic aliyeagana na wachezaji wa Yanga jana baada ya mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara unaopigwa leo dhidi ya KenGold na kuondoka kwake ndiko kumempa shavu Mfaransa huyo ndani ya kikosi cha Yanga.

Kwa msimu huu pekee, Hamdi anakuwa kocha mkuu wa tatu kuifundisha Yanga, huku ikianza msimu na Miguel Gamondi na kufuatiwa na Ramovic.

Mjerumani huyo atakayekumbukwa kwa uchezaji wake wa Gusa Achia Twende Kwao, anadaiwa kutua katika kikosi cha CR Beloiuzdad ya Algeria inayoshika nafasi ya pili katika ligi ya nchini humo (Ligue 1), huku akiiongzoa Yanga katika mechi sita za Ligi Kuu na kushinda zote, timu hiyo ikifunga jumla ya mabao 22 na kufungwa mawili tu na kuvuna pointi 24, akiiacha timu nafasi ya pili ikiwa na pointi 42.

Kocha huyo anaondoka Yanga akiwa na rekodi mpya binafsi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi akiwa na timu hiyo, huku Hamdi akitua kikosi humo akiwa amecheza mechi mbili tu za kirafiki kabla kutangazwa kutua Yanga inayotetea taji la Ligi Kuu inayolishikilia misimu mitatu mfululizo.

Related Posts