Aliyeua bila kukusudia jela miaka mitatu

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Tabora, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, Hussein Warioba baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Hamis Okelo bila kukusudia.

Hussein alishtakiwa kwa kumuua Hamis kwa kumchoma na kisu upande wa kushoto wa kifua baada ya kutokea ugomvi baina yao walipokuwa wakinywa pombe ya kienyeji.

Jaji Dk Adam Mambi ametoa hukumu hiyo Februari 3, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya mahakama, ambapo Jaji huyo amesema baa Hussein alikiri kusababisha kifo bila kukusudia ambapo alitiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia chini ya kifungu cha 195 cha Kanuni ya Adhabu.

 Kwa mujibu wa mashtaka, tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba 8, 2024 ambapo mshtakiwa na marehemu walikuwa wakinywa pombe ya kienyeji kwa Regina Kasani, ambapo ilidaiwa baada ya kunywa kwa muda mrefu Hussein na Hamis walianza kugombana.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili jaji amesema baada ya kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, suala kuu kwa mtazamo wake ni kuzingatia hukumu inayofaa.

“Nimezingatia kwa makini mawasilisho kutoka kwa pande zote mbili ikiwa ni pamoja na kupunguza kutoka kwa utetezi, ili nifikirie hukumu inayofaa kwa mtuhumiwa, pia nimesoma ukweli na mazingira ya kifo cha marehemu ili kuniwezesha kuamua hukumu inayofaa,”amesema.

Jaji huyo amesema kwa ujumla kosa la kuua bila kukusudia ambalo mshtakiwa anashtakiwa chini yake linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha juu ambacho ni kufungwa maisha jela chini ya kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu lakini mahakma ina hiari ya kuweka kosa dogo kulingana na mazingira ya kesi.

Amesema kutokana na ukweli kwamba kifo hicho kilitokana na ugomvi uliosababishwa na pombe na lilikuwa ni kosa la kwanza kwa mshitakiwa kama ilivyokubaliwa na upande wa mashtaka chini ya kumbukumbu za kesi, mahakama imeona ni vyema kuzingatia adhabu ndogo.

“Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na mgogoro, na marehemu lakini kwa bahati mbaya ugomvi huo ulisababisha kifo chake. Hii inaonyesha mtuhumiwa hakuwa na chuki,”amesema

“Maamuzi mbalimbali ya mahakama yanaonesha kuwa pale inapothibitika kuwa kifo hicho kilitokana na kupigana au ugomvi, mahakama inapaswa kuzingatia kuchagua kosa la kuua bila kukusudia, kwa kuzingatia mambo hayo na mazingira ya kifo cha marehemu, naona ni sahihi kwa mtuhumiwa kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela,” amehitimisha Jaji Mambi

Awali ilidaiwa kuwa licha ya kusuluhishwa, Hussein alichomoa kisu kutoka kwenye koti lake na kumchoma Hamis upande wa kushoto wa kifua, ambapo alianguka chini huku akivuja damu.

Ilidaiwa mshtakiwa aliamua kukimbia eneo la tukio kuelekea Bwawa la Ibaku huku mashuhuda wa tukio hilo wakimkimbiza hadi walipomkamata na kusubiri askari polisi wafike kwa ajili ya hatua zaidi.

Tukio hilo liliripotiwa katika uongozi wa kijiji na polisi na katika muda mfupi askari polisi wa Kituo cha Nzega walifika eneo la tukio ambapo uchunguzi ulianza ikiwemo mashuhuda wa tukio hulo kuhojiwa na baadhi yao walieleza Hussein alimchoma kisu Hamisi baada ya kutokea ugomvi kati yao.

Wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo bila kukusudia ambapo akiwakilishwa na Wakili Saikon Justine, aliomba kupunguziwa adhabu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na nia ya kutenda kosa hilo na ugomvi uliotokea baina yao ulisababishwa na unywaji pombe.

Amesisitiza kuwa mshtakiwa anasumbuliwa na macho hivyo kuiomba mahakama kuzingatia adhabu ndogo.

Related Posts