Shirika la Kimataifa lajitosa usafiri mwendokasi Dar

Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) umeingia makubaliano na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) ili kuusaidia wakala huo kuwapata watoa huduma watakaofanya kazi katika awamu ya tatu na ya nne ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia akizungumza na The Citizen jana Jumanne, Februari 4, 2025 amesema taasisi hizo mbili zimeingia makubaliano ili kuwezesha mchakato wa mazungumzo ya kupata watoa huduma katika awamu hizo mbili.

Ujenzi wa awamu ya tatu ya BRT inaanzia katikati ya Jiji hadi Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere na ya nne inaanzia katikati ya Jiji hadi Bunju kando ya Barabara ya Bagamoyo.

Ujenzi wa BRT awamu ya tatu kwa sasa unakadiriwa kufikia asilimia 75 na utakamilika Juni 2025 wakati BRT awamu ya nne ambayo kwa sasa ni asilimia 20 itakamilika mwishoni mwa 2025 kwa mujibu wa Dk Kihamia.

Usafiri wa BRT ulianza na awamu ya kwanza ambayo inaunganisha Kimara, Mbezi hadi Kibaha mkoani Pwani hadi katikati ya Jiji kupitia barabara ya Morogoro ambayo ilianza kazi mwaka 2016.

Ujenzi wa miundombinu ya awamu ya pili inayoanzia katikati ya jiji hadi Mbagala pia umekamilika, lakini inasubiri mchakato wa upatikanaji mabasi.

Dk Kihamia amesema tayari IFC imeanza kutafuta watoa huduma kwa mujibu wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) na kanuni zake.

“Serikali tayari imetoa fedha za kulipa IFC ili itusaidie katika mazungumzo na wasimamizi wa mabasi, wasimamizi wa hazina, watoza nauli na watoa huduma wa Mfumo wa Usafiri wa Kiakili (ITS),” amesema.

Amefafanua kuwa IFC hutumia vitambuzi, uchanganuzi na teknolojia ya mawasiliano ili kuimarisha usalama na ufanisi wa mfumo wa BRT.

Dk Kihamia amesema ushirikiano wa IFC unafanyika ili kuhakikisha watoa huduma wote muhimu wanakuwa tayari wakati ujenzi unakamilika na kuwezesha shughuli kuanza kama ilivyopangwa.

Dk Kihamia amesema ikiwa kila kitu kitaendelea sawa, IFC itahitaji miezi 21 kukamilisha mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kupata huduma muhimu.

“Miradi ya namna hii inatuhitaji kushirikisha washauri ili kusaidia katika kazi mbalimbali, kuhakikisha tunaepuka kuingia katika mikataba mibovu ambayo inaweza kusababisha hasara kwa Serikali,” amesema.

Dart ambayo ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kuanzisha na kuendesha mfumo wa BRT jijini Dar es Salaam, imesema ushirikiano na IFC unalenga kuhakikisha unaleta ufumbuzi endelevu wa tatizo la usafiri mijini.

Januari 20, 2025, Dart iliwakutanisha wataalam mbalimbali, wakiwemo washauri wa masuala ya sheria, kiufundi, mazingira na kijamii ili kujadili jinsi ya kuboresha usafiri wa mijini na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kuendesha BRT.

“Tuko tayari kufanya kazi na IFC na wadau wote muhimu ili kuhakikisha mfumo thabiti wa biashara ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kwa awamu zijazo za mradi,” alisema.

Timu ya IFC iliongozwa na Ofisa mkuu wa uwekezaji na kiongozi wa timu iliyoko nchini Kenya, Jacques Bleindou.

Bleindou alielezea malengo muhimu ya mchakato wa ushauri wa kitaalamu, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau mbalimbali ili kukusanya maarifa ya kina kuhusu mradi wa BRT.

“Mchakato huu wa ushauri wa kitaalamu utatuwezesha kutengeneza mtindo bora, endelevu na wa gharama nafuu wa ununuzi wa watoa huduma kwa watumiaji wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam,” alisema

Related Posts