Dodoma. Ikiwa leo ni maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mji wa Dodoma umekuwa na msongamano mkubwa wa magari kutokana na barabara zinazopita kwenye uwanja wa Jamhuri yanapofanyika maadhimisho hayo kuwa na msongamano wa watu na magari hivyo kusababisha foleni kubwa.
Mwananchi Digital imeshuhudia leo Jumatano Februari 5, 2025 msongamano na foleni kubwa ya magari ya mizigo, mafari ya shule na ya watu binafsi kwenye barabara zote zinazokatisha kwenye Uwanja wa Jamhuri na hivyo kusababisha kero kwa watumiaji wa barabara hizo.
Miongoni mwa barabara zenye msongamano mkubwa wa magari na watu ni Dodoma Inn ambayo inatoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) hadi kwenye mataa ya Chako ni Chako Bar inayopitisha magari ya mizigo ambapo kuna foleni kubwa ya magari ya mizigo na watu binafsi ambao wameshindwa kuendelea na safari kutokana na barabara inayokwenda uwanja wa Jamhuri kuwa na msongamano mkubwa.
Barabara hiyo pia inaunganisha kutoka Uwanja wa Jamhuri hadi mzunguko wa Bahi Road na kwenda Singida ambapo pia kuna msongamano mkubwa wa watu na magari hali inayosabaisha foleni.
Kutokana na msongamano huo baadhi ya madereva wa magari ya mizigo na magari binafsi waliamua kutumia barabara nyingine katikati ya mjna kuendelea na safari zao ili kupisha msongamano huo.
Mmoja wa dereva wa magari ya mizigo Ahmed Kanno amesema hakutegemea kukutana na msongamano mkubwa kiasi hicho kwani amezoea kupita njia hiyo ikiwa haina msongamano wowote.
“Kwa kweli Dodoma leo hapafai, nimekaa kwa nusu saa nzima kusubiri foleni iishe niondoke lakini naona hakuna dalili, wenzetu wenye magari binafsi wanachepuka kuingia katikati ya mji lakini sisi hatuwezi kwa sababu uzito wa magari yetu hauturuhusu kupita barabara nyingine zaidi ya hii,” amesema Kanno.
Wakati magari yakiwa yamesimama kwenye foleni baadhi ya wanachama wa CCM waliamua kushuka kwenye magari yaliyowabeba kuwapelekea uwanjani na kuanza kutembea kwa miguu ili kuwahi kufika.
Ili kupunguza msongamano huo, askari wa usalama barabarani walikuwa wanaongoza magari kupita kwa utaratibu bila kuleta madhara kwa wananchi na kwa watumiaji wengine wa barabara.