WHO yamteua Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, uchaguzi ukitajwa Mei

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza uteuzi wa Dk Chikwe Ihekweazu kama Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, huku likiweka wazi kuwa, Mkurugenzi mpya wa Kanda atachaguliwa Mei mwaka huu.

Uteuzi huo unakuja kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile aliyefariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kufuatia kifo hicho Desemba 2, 2024 Rais wa Tanzania, katika hafla ya kuaga mwili, Samia Suluhu Hassan alisema nafasi ya Dk Ndugulile itaelekezwa kwa Mtanzania mwingine mwenye sifa.

Katika salamu zake, Rais Samia alisema nchi ilimpata mwakilishi: “Wanadamu tunapanga yetu, lakini Mungu anatupangia, Dk Ndugulile ameiweka nchi pazuri lakini Mungu amechukua kilicho chake.

“Tutaingia tena kwenye mashindano tutatafuta Mtanzania mwenye sifa anayeweza kushindana na ulimwengu, tutaingia tena na tutaweka mtu mwenye sifa ileile kutuwakilisha,” alisema Rais Samia.

Desemba 10 akizungumza baada ya kuapisha viongozi mbalimbali akiwa katika Ikulu Ndogo Tunguu, Zanzibar Rais Samia alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi kujiandaa kugombea nafasi hiyo.

“Naomba nifichue siri hapa, tumepitia zaidi ya CV tano na tukaona Profesa Janabi anafaa kuchukua nafasi ya Dk Ndugulile. Hivyo, tunakundaa kwenda kugombea nafasi hiyo muda utakapofikia. Ujiandae,” alisema Rais Samia.

Dk Ndugulile aliyechaguliwa kwenye nafasi hiyo Agosti 2024, alifikwa na mauti ikiwa imesalia miezi michache kwenda kuanza kutumikia nafasi yake mpya WHO mapema Machi mwaka huu, akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania na mwana Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kwanza.

Uteuzi huu unakuja wakati ambapo Dk Matshidiso Moeti anamaliza kipindi chake cha uongozi kama Mkurugenzi wa Kanda, akihitimisha muongo mmoja (miaka 10) wa huduma yenye kujitoa kwa ustawi wa afya barani Afrika.

Kwa mujibu wa tovuti ya WHO, Dk Ihekweazu ni daktari wa magonjwa ya mlipuko, daktari wa afya ya umma na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO anayesimamia mifumo ya ujasusi na ufuatiliaji wa dharura za kiafya.

Kwa sasa, anaongoza kituo muhimu cha WHO cha Ujasusi wa Mlipuko na Janga kilichopo Berlin, ambacho kimeanzishwa ili kuimarisha maandalizi ya magonjwa ya mlipuko kupitia uchambuzi bora wa takwimu na uamuzi wa haraka.

Kabla ya uteuzi wake, Dk Ihekweazu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) kutoka Agosti 2016 hadi Oktoba 2021, baada ya kuteuliwa na Rais Muhammadu Buhari.

Wakati wa uongozi wake, alibadilisha NCDC kuwa taasisi bora ya afya ya umma, akiongoza Nigeria katika kukabiliana na milipuko mbalimbali ya magonjwa na kusimamia maendeleo makubwa ya shirika hilo.

Alihusika katika kuanzisha Maabara ya Taifa ya Marejeleo jijini Abuja, kuanzisha vituo vya kitaifa na kieneo vya dharura za afya ya umma na kupanua mpango wa mafunzo ya magonjwa ya mlipuko kwa wahudumu wa afya.

Uongozi wake ulikuwa muhimu katika kupitishwa kwa sheria ya NCDC mwaka 2018, ambayo iliipa taasisi hiyo mamlaka na uhuru zaidi.

Kazi yake ilipata kutambuliwa kimataifa, ikijumuisha ziara za Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Dharura ya WHO kuhusu Uviko19 na kuongoza juhudi za Nigeria dhidi ya janga hilo.

Dk Ihekweazu ana uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika nyadhifa za juu za afya ya umma na uongozi katika taasisi mbalimbali mashuhuri za afya duniani, ikiwa ni pamoja na NCDC, Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Afrika Kusini (NICD), Shirika la Ulinzi wa Afya la Uingereza na Taasisi ya Robert Koch (RKI) ya Ujerumani.

Amekuwa sehemu ya juhudi nyingi za WHO katika kukabiliana na milipuko mikubwa ya magonjwa duniani, akiwemo kwenye ujumbe wa pamoja wa WHO-China kuhusu ugonjwa wa Uviko-19.

Dk Ihekweazu alizaliwa na wazazi wa asili ya Nigeria na Ujerumani, hali ambayo imempa mtazamo wa kimataifa. Alikulia katika mji wa Nsukka, Nigeria, ambako alipata elimu yake ya msingi na sekondari. Ana shahada ya udaktari (MBBS) kutoka Chuo Kikuu cha Nigeria, Nsukka, Diploma ya tiba ya kitropiki kutoka Chuo Kikuu cha Heidelberg, Ujerumani, shahada ya uzamili ya afya ya umma kutoka Chuo Kikuu cha Heinrich Heine, Düsseldorf, Ujerumani, pamoja na ushirika wa mpango wa Ulaya wa mafunzo ya epidemiolojia ya uingiliaji na ushirika wa Kitivo cha Afya ya Umma cha Uingereza.

Alianza taaluma yake kwa kufanya mafunzo ya kitabibu na kutumikia Mpango wa huduma ya Kitaifa wa vijana wa Nigeria (NYSC), kisha akachukua nyadhifa katika Taasisi ya Robert Koch, Huduma ya Afya ya Taifa ya Uingereza (NHS) na Shirika la Ulinzi wa Afya la Uingereza.

Baadaye, alikuwa Mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Kifua Kikuu katika Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Mbali na taaluma yake, Dk Ihekweazu anahudumu kwenye bodi za mashirika kadhaa, yakiwemo Society for Family Health na Nigeria Health Watch.

Amepokea tuzo mbalimbali, zikiwemo National Productivity Order of Merit na Officer of the Order of the Niger kutoka serikali ya Nigeria, pamoja na Shahada ya Heshima ya Udaktari wa sayansi kutoka Shule ya Kitropiki ya Tiba ya Liverpool na Medali ya Clara Southmayd Ludlow kutoka Jumuiya ya Marekani ya Tiba ya Kitropiki na Afya.

Uteuzi wa Dk Ihekweazu kama Kaimu Mkurugenzi wa Kanda una hakikisha mabadiliko ya uongozi na kuendeleza kasi ya maendeleo.

Tovuti hiyo imeleeza utaalamu na uongozi wake, utakuwa muhimu katika kushughulikia changamoto zijazo na kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dk Moeti. Uchaguzi ujao wa mwezi Mei utaamua kiongozi atakayesimamia kazi muhimu ya WHO katika Kanda ya Afrika.

Related Posts