Barabara mpya kuzingatia njia ya waenda kwa miguu

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema barabara zote mpya zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinahusisha ujenzi wa njia za waenda kwa miguu katika maeneo ya majiji, miji na maeneo mengine.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya ameyasema hayo leo Jumatano Februari 5, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko.

Mbunge huyo amehoji ni kwa nini Serikali isiboresha barabara zote nchini kwa kuongeza Barabara za waenda kwa miguu na pikipiki.

Akijibu swali hilo, Kasekenya amesema Serikali inahakikisha kuwa barabara zote mpya zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinahusisha ujenzi wa njia za waenda kwa miguu katika maeneo ya majiji, miji na maeneo mengine.

“Kwa barabara ambazo zilijengwa bila kuweka njia za waenda kwa miguu maboresho yamekuwa yanafanyika kwa kujenga njia za waenda kwa miguu kulingana na upatikanaji wa fedha,” amesema.

Katika swali la nyongeza, Matiko amesema majibu ya Serikali yanasikitisha sana kwa kuwa wameendelea kupoteza Watanzania, waenda kwa miguu na waendesha pikipiki.

“Hata jana tu tumeshuhudia ajali mbaya sana hapo Meriwa na watu wawili wamepoteza maisha. Unapokuwa unakwenda Dar es Saalam wabeba mikaa wanabeba mikaa mingi ambayo inaziba hata uoni inaweza kusababisha ajali,” amesema.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya akijibu maswali ya wabunge leo Februari 5,2025, bungeni Jijini Dodoma

Amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa Sheria za Usalama wa Barabarani inatekelezeka na waendesha pikipiki wanafuata sheria hizo ili wasipoteze maisha.

Aidha, amesema kumekuwa na mwingiliano katika barabara kuu ambapo madereva wamekuwa wakikutana na wanyama mbalimbali.

“Wizara hii inashirikianaje na wizara nyingine kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kuhakikisha raia wenye mifugo wanahakikisha kuwa wanyama hao hawaingii barabarani na kusababisha ajali,” amehoji.

Akijibu maswali hayo, Kasekenya amesema changamoto iko katika barabara za zamani lakini zinazojengwa sasa njia ya waenda kwa miguu zipo.

Amesema wanasheria ambazo kila mtumiaji wa barabara anatakiwa kufuata na kuwa suala la waendesha pikipiki kuvunja sheria liko katika vyombo vingine.

“Kwa hiyo tunasheria ambazo zinahakikisha kila anayetumia barabara hizi afuate sheria ambazo zipo na zoinatumika. Suala la waendesha pikipiki ambao wanavunja sheria viko vyombo vingine wanashughulika nalo na ndio maana wanachukuliwa hatua kwa sababu sheria hizo ziko,”amesema.

Related Posts