Unguja. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imesema lazima iwepo sheria mpya itakayotoa adhabu kwa wanaosingizia makosa ya ukatili, ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pia, watendaji wanaozorotesha, uchukuaji wa hatua katika masuala hayo pamoja na adhabu kwa wazee au walezi wanaotelekeza familia zao.
Mapendekezo hayo yametolewa na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi hiyo, Dk Mahfoudha Masoud Ali wakati alipokuwa akiwasilisha mada kwa wadau wa sheria leo, Februari 5, 2025, Mjini Zanzibar.
Bila ya kutaja tafiti Wakili huyo amesema, mapendekezo hayo yametokana na utafiti uliofanywa katika maeneo yaliotumika kuangalia sheria na uzoefu wa nchi mbalimbali, mikataba ya kimataifa, sheria za ndani, sera, miongozo na maoni ya wadau.
“Uwepo wa sheria mpya utasaidia kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na kupunguza vitendo hivyo endapo sheria hiyo itasimamiwa na kutekelezwa inavyotakiwa,” amesema Dk
Pia, Dk Mahfoudha amesema ofisi hiyo imependekeza kuanzishwa kwa vituo vya waathirika wa ukatili wa kijinsia, kuwafanyia tathmini, kuwarekebisha (rehabilitation of victim) pamoja na kuwepo kwa wajibu wa kuwajulisha haki zao ili kukabiliana na janga hilo.
Wakili Mkuu wa Serikali kutoka ofisi hiyo, Dk Abdul Nasser Hikmany amesema hatua hiyo imekuja baada ya kufanyika utafiti ulionesha kuwa vitendo vya ukatili vimekosa sheria na miongozo ya moja kwa moja ya kuvidhibiti na ndio sababu ya kuongezeka kwa matukio hayo.
Amesema, utafiti huo uliangalia mifumo ya sheria inayohusiana na udhibiti wa masuala ya ukatili wa kijinsia, umebaini changamoto mbalimbali ndio maana ofisi hiyo imekuja na mapendekezo ya kisheria na kiutendaji ili kudhibiti vitendo hivyo, ikiwemo kuwawajibisha wanaokosa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahalifu.
“Ofisi hii inapendekeza kuanzishwa sheria maalumu itakayosimamia masuala ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ukiwemo wa kimwili, akili na hata kingono ambao utasababisha ukatili wa kijinsia kwa muathirika,” amesema Dk Abdul
Hata hivyo, Dk Hikmany amewataka wadau wa udhalilishaji kutoa michango yao katika mapendekezo hayo ili kuona haja ya kuja na sheria mpya au kuzifanyia maboresho sheria zilizopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Zanzibar, Tabia Makame Mohammed amesema uzoefu unaonesha kuwa hakuna usimamizi katika sheria zilizopo jambo linalochangia vitendo hivyo kuendelea kutokea na kushauri kuzitekeleza ipasavyo sheria hizo, wakati wakisubiria sheria yenye nguvu dhidi ya janga hilo.
Amesema uwepo wa sheria na sera inayoendana na matakwa ya jamii ni jambo zuri lakini sheria hizo zinapaswa kuzingatia jinsia zote mbili kwani wote ni waathirika hivyo cha umuhimu ni kuzingatia jinsia zote mbili kwani zinaathirika kwa namna moja ama nyengine.
Mtabibu wa saikolojia Kitengo cha Afya ya Akili, Mohammed Sharif Haji amesema sheria zilizopo zilijikita kuwafikisha waathirika katika vyombo vya sheria na kupata haki zao bila kuzingatia matibabu ya afya ya akili ambayo huathirika zaidi kutokana na matendo hayo.
Hivyo, ameshauri sheria ambazo zinatengenezwa zinatakiwa kuzingatia hilo ili kumuweka muathirika sehemu salama. Pia, ameshauri adhabu ya anayesingizia iende sambamba kutoa haki ili kurudisha heshima yake katika kuimarisha uchunguzi, upelelezi na kuepusha kutoa hukumu kwa wasiokuwa na hatia.