Unguja. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdallah amesaini mpango wa Taifa wa kushughulikia utekelezazi wa ajenda ya masuala ya wanawake, kuhusu amani na usalama ulioandaliwa mahususi kwa ajili ya kutekeleza azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akizungumza wakati wa kusaini mpango huo leo Jumatano Januari 5, 2025 Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Abeida katika ofisi za wizara hiyo Kinazini Unguja, amesema mpango huo ni heshima kwa Tanzania kwani imeonesha wazi kukubali na kutekeleza azimio hilo la Umoja wa Mataifa la kuhakikisha wanawake wanakuwa katika amani na usalama wakati wote.
Ameeleza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Tanzania Bara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta zingine za umma na binafsi wameshirikiana katika kuandaa mpango huo ili kuleta ufanisi katika utekelezaji.
“Katika uandaaji wa mpango huu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto ndio waratibu wakuu waliosimamia lakini sekta zingine zinazoshughulika na masuala ya wanawake zimehusihwa kwa ajili ya kutoa maoni yao,” amesema Katibu Mkuu huyo.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abbas Ali amesema mpango huo utasaidia katika kuongeza nguvu ya utetezi wa masuala ya wanawake ili wabaki salama katika harakati zao zakujitafutia kipato.
Amefahamisha kwamba mbali na suala la amani, mpango huo pia unaelekeza namna ya kulinda amani na kuleta suluhisho wakati wa migogoro kwani mwanamke akikosa amani hatoweza kufanya shughuli zake za kujiletea maendeleo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Timotheo Mgonja amesema mchakato wa kuandaa mpango huo ulinza mwaka 2020 na sasa upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.