Dar es Salaam. Karakana ya mbao na samani mbalimbali iliyopo Mtaa wa Kibangu, Kata ya Makuburi, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam imeteketea kwa moto.
Moto huo ambao umetokea asubuhi ya leo Jumatano, Februari 5, 2025 umeelezwa na mashuhuda umesababishwa kwa hitilafu kwenye nguzo ya umeme iliyopo pembezoni mwa jengo hilo kisha kudondokea kwenye samani hizo na kuwaka.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Peter Mtui amesema walipokea taarifa kwa simu kutoka kwa wananchi.
“Tulipokea wito wa moto majira ya saa nne na dakika 12 asubuhi Mtaa wa Makuburi, ndipo timu yetu imetoka haraka kufika kwenye sehemu ya tukio na kukuta moto unawaka kwenye kiwanda kidogo cha samani ndipo tukaanza kuzima,” amesema Mtui.
Amesema walipata usumbufu kuzima moto huo kwa sababu ni mbao zilizokuwa zinaungua ukichangiwa na upepo hadi kusababisha hofu kwa wananchi waliopo jirani.
Mmiliki wa Karakana hiyo, George Charles amesema moto huo ulianzia kwenye nguzo ya umeme ambapo cheche ya moto ilidondokea kwenye eneo la juu la karakana na yeye alikuwa chini ya banda hilo hivyo alichelewa kuugundua moto huo.
“Ofisi hii imejengwa kwa mbao kuanzia chini hadi juu ikigharimu kiasi cha Sh27 milioni lakini pia kulikuwa na makochi ya wateja yalipaswa kuondoka yenye thamani ya Sh8 milioni, bado kuna mashine na mbao zote zimeungua,” amesema Charles.
Shuhuda wa tukio hilo Jackson Joseph, amesema moto ulianzia sehemu ya juu ya karakana hilo ambapo sofa lilishika moto na kueneza kwingine.
“Moto ulianzia kule juu ndipo mafundi sofa na mafundi gereji tukaanza kuuzima kwa kutumia maji na mchanga Ingawaje hatukuweza kuuzima, lakini tuliupunguza kasi ya kuenea kwani endapo tungetegemea Jeshi la Zimamoto nyumba nyingi zingeathirika kwani walikuja kwa kuchelewa,” amesema Joseph.
Jirani wa karakana hiyo, Maria Oleti anayefanya kazi ya kuuza genge, amesema mteja aliyekuja kununua bidha gengeni hapo ndiye alimuonyesha moto huo ulipoibuka.
“Alikuwepo mteja wangu ananua bidhaa ndipo alipoanza kushangaa kwa sauti kubwa jamani moto moto, ndipo na mimi kuanza kutoka kuangalia na kuuanza kukimbia,” amesema Maria.