Alichokisema Rais Mwinyi miaka 48 ya CCM

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema mafanikio ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tangu kuasisiwa kwake ni kielelezo muhimu cha kujipambanua ubora wake kwa vyama vingine vya siasa vya ndani na nje ya nchi.

Amesema jijini Dodoma leo Jumatano, Februari 5, 2025 wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa CCM.

Katika maadhimisho hayo yaliyoudhuriwa na wakereketwa, wanachama wa chama hicho, viongozi mbalimbali wa Serikali na wastaafu, yaliambatana na kuwatambulisha wagombea wateule kwa nafasi ya urais kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar na kusoma wasifu wao.

Rais Samia ni mgombea urais Tanzania, Dk Mwinyi mgombea urais Zanzibar huku Dk Emmanuel Nchimbi akiwa mgombea mwenza wa Samia.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais Mwinyi amesema: “CCM imeonyesha ukomavu wa kiuongozi na demokrasia, ni dhahiri wote tunawajibu wa kudumisha mafanikio yetu kwa kuzidi kuimarisha umoja na mshikamano ambayo ni misingi mikuu ya mafanikio tunayoendelea kuyapata.”

Dk Mwinyi amesema kwa kuzingatia wanakabiliwa na uchaguzi wa dola baadaye mwaka huu, wanachama wa chama hicho hawana budi kuendelea kudumisha misingi hiyo ili kukiimarisha chama hicho kishike dola pande zote Tanganyika na Zanzibar.

“Ili kufanikisha azma hii, tunao wajibu wa kuhakikisha wanachama wetu wanajiandikisha katika daftari la wapiga kura na wakati ukifika wahakikishe wanakwenda kukipigia kura chama chetu,” amesema.

Katika hotuba yake, Dk Mwinyi amesema mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2020/25, kwa pande zote ni dhawabu tosha ya kuwafanya Watanzania kuendelea kukiamini na kukichagua chama hicho kiendelee kuongoza nchi.

“Nitoe wito kwa wana-CCM, kila mmoja kwa nafasi yake kuyatangaza mafanikio na kuwashawishi Watanzania wote kuendelea kukiiunga mkono chama chetu ili nchi yetu ipige hatua kimaendeleo,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema chama hicho kiliasisiwa katika uwanja wa Amani Visiwani Zanzibar mwaka 1977, baada ya kuungana vyama viwili, Tanu na ASP, vilivyofanya kazi kubwa kufikia demokrasia ya kweli.

“Baada ya kazi nzuri tangu mwaka 1961, 1964 hadi 1977, vyama hivi viliona havina sababu ya kuwa na vyama viwili ila tuwe na chama kimoja kitakacholiunganisha Taifa nzima,” amesema.

Dk Nchimbi ambaye ni mgombea mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao mwaka huu, amesema kwa utaratibu wa kawaida wa chama hicho, halimashauri kuu ya CCM iliamua sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwake zifanyike kila baada ya micka mitano kwa ngazi ya kitaifa.

“Sherehe hizi zilitakiwa zifanyike mwaka 2027, lakini Kamati Kuu baada ya kupokea maombi kutoka kote nchini ikieleza uzito wa mwaka huu na kazi zilizofanywa na Serikali ya CCM, Kamati Kuu iliridhia zifanyike mwaka huu,” amesema.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Shiriki uchaguzi kwa uadilifu na kazi iendelee,” na mkutano mkuu wa chama hicho chini ya Mwenyekiti wake na Rais Samia umesisitiza: “Uchaguzi wa uadilifu na kwakweli tungependa wana-CCM wote watuelewe tukisema hivyo.”

“Mwenyekiti anamaanisha, Kamati Kuu inamaanisha na Halimashauri Kuu ya Taifa inamaanisha tunataka Chama kisafi ambacho kiko tayari kuwatumikia wananchi,” amesema.

Balozi Nchimbi katika maelezo yake amesema sherehe hizo zilizinduliwa Januari 28, mwaka huu na kufanyika mikoa mbalimbali na kilele chake kuhitimishwa Jijini Dodoma, kilichotanguliwa na shughuli mbalimbali zilizofanywa na Jumuiya za Chama hicho, ikiwemo Marathoni, Kongamano na Mafunzo.

Amesema wanaposherekea miaka hiyo, wanaangalia nguvu ya chama chao zinazopimwa kwa kuangalia idadi ya wanachama wake kwa kujipanga safu za uongozi wake na alama muhimu za chama hicho.

“Wakati CCM kinaanzishwa kilikuwa na jumla ya matawi 6,424, leo tunavyoongea kina matawi 23,430, na wakati vyama vinaungana vilikuwa na wanachama 103,923, leo CCM kina jumla ya wanachama milioni 12.2,” amesema.

Related Posts