Dar es Salaam. Kuunganisha wabunifu na wawekezaji kumetajwa kuwa suluhisho la kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kupata masoko na teknolojia katika ubunifu wao.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Februari 4,2025 na Mkuu wa Mawasiliano ya Vodacom, Anneth Kanora katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano kati yao na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech).
Ushirikiano huo unalenga kuwashirikisha wabunifu kuelekea wiki ya ubunifu inayotarajia kufanyika Mei 12 hadi 16, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kanora amesema kampuni hiyo, katika misimu mitatu mfulizo imetoa elimu ya teknolojia na ubunifu kwa kuwafikia wanawake zaidi ya 3,000 wenye umriwa kati ya miaka 13 hadi 18.
“Kupitia mpango kazi wetu tumetumia bunifu zenye maidhui mazuri kwa jamiii kwa kuziingiza kwenye mfumo wa huduma za Vodacom, ambapo tunampa faida mbunifu na Mtanzania na kuhamasisha bunifu nyingine,” ameeleza.
“Katika kupeleka tasnia ya ubunifu na teknoljia mbele, tunaziongezea nguvu bunifu mbalimbali, huku tukifanya majadiliano na watu wa mataifa mengine ili kupata ujuzi wa kuinua bunifu zetu zaidi na zaidi,”anaeleza
Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, amesema, dhamira ya UNDP ni kujenga mfumo wa bunifu jumuishi na wenye ustahimilivu.
“Tunatambua kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kushughulikia changamoto za maendeleo endelevu na kuunda fursa shirikishi,” anasema.
Amesema kupitia ushirikiano huo, wamelenga kuwainua Watanzania, vijana na wanawake, kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika sekta ya teknolojia.
“Wiki ya ubunifu Tanzania 2025 imelenga kuonyesha ari ya ubunifu Tanzania, hasa kwenye jukwaa la kimataifa ili kuvutia uhamasishaji na ushirikiano wa mifumo iliyofanikiwa duniani,” anasema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Uhamisho wa Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Athumani Ngumia amesema mchango mkubwa wa ushirikiano huo ni kukuza ubunifu.
“Costech imejizatiti kuwaunganisha wadau kwa lengo la kuchochea utafiti, teknolojia na ubunifu ambao unaendana na vipaumbele vya nchi katika maendeleo na maono ya mwaka 2050.
Amesema, maadhimisho ya wiki ya ubunifu kwa mwaka 2025 ni jukwaa pekee kwa ajili ya sekta binafsi na umma,ili kutekeleza suluhisho kwa ajili ya ukuaji endelevu.