Trump aiondoa Marekani UNHRC, UNRWA

Washington. Rais Donald Trump amesaini amri ya kuiondoa Marekani katika Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHRC), jambo linalohatarisha mchango wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa.

Trump pia ameamuru Marekani kujiondoa katika Mpango wa Umoja wa Mataifa unaotoa Misaada kwa Wapalestina (UNRWA).

Tovuti ya Deutshe Welle (DW) imeripoti leo Jumatano Februari 5, 2025, kuwa Trump pia analenga kupitia upya ushiriki wa taifa hilo katika shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sekta ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Siyo mara ya kwanza Trump kuiondoa Marekani katika UNHRC, aliwahi kuchukua uamuzi huo mwaka 2018.

Hata hivyo, amri hiyo ilitenguliwa na Rais Joe Biden mwaka 2021 na kuirejesha Marekani UNHRC.

Akizungumzia uamuzi huo wa Trump, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema: “Trump amekuwa akifanya kazi bila kuchoka kuongeza ufanisi na ubunifu.”

“Mchango wa Marekani katika UN umekuwa ukisaidia na kupambana masuala ya kiusalama yanayoitesa dunia.

“Katibu Mkuu anatarajia kuona ushirikiano kati ya Serikali ya Trump na UN ukiimarishwa,” ameongeza Dujarric.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu ya White House, Will Scharf ameeleza kuwa ndani ya UN kulikuwa na urasimu katika mamlaka zake.

“Kwa ujumla amri hii ya Rais (Trump) inatoa mwanga kwetu kufanya tathmini juu ya ushiriki wetu katika kufadhili shughuli za UN hususan ni wakati huu ambao kuna kusuasua kwa michango kutoka mataifa mengine wanachama wa umoja huo,” amesema Scharf.

Kuhusu suala hilo, Trump amesema UN inafanya kazi nzuri lakini shughuli zake haziendeshwi inavyohitajika.

“UN inapaswa kuchangiwa na kila taifa, lakini tukifuatilia mwenendo huu ambao tumeona sisi (Marekani) ndiyo wachangiaji wakubwa.

“Mizozo hii ambayo tunachangia fedha nyingi kuishughulikia inapaswa kukoma mara moja. Sisi (Marekani) hatuoni faida wala kusaidiwa na nchi nyingine kuifadhili UN,” ameongeza Trump.

Trump amekuwa akiendesha kampeni ya kuliondoa taifa hilo kwenye ufadhili wa taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa katika awamu yake ya kwanza ya uongozi na awamu hii iliyoanza Januari 20 mwaka huu.

Wajumbe 47 wa UNHRC huchaguliwa na Baraza Kuu la UN kila baada ya miaka mitatu, huku ushiriki wa mwisho wa Marekani katika vikao vya baraza hilo ulikuwa ni Desemba 31, 2024.

Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts