Wananchi wahamasika kujiandikisha, wataja mfumo ‘kusahau’ vidole vyao

Pemba. Wakati uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura likiendelea, wananchi katika Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamesema wameridhishwa na uandikishaji licha ya kujitokeza kwa changamoto ya baadhi vidole vyao kushindwa kutambulika kwa mfumo.

Hata hivyo, hakuna anayeshindwa kuandikishwa kwani changamoto hiyo inatatuliwa kwa wakati. Awamu ya pili ya uandikishaji imeanza tangu Februari Mosi Wilaya ya Micheweni Mkoani hapa na linatarajiwa kumalizika Machi 17, 2025 Wilaya ya Mjini Unguja huku wakitarajiwa kuandikwa wapigakura wapya 78, 922.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Wilaya ya Chakechake baada ya kushiriki katika kazi hiyo na kupata haki yao ya kujiandikisha katika daftari hilo.

Khadija Khamis Ali mkazi wa Mtambwe amesema hali ni shwari na zoezi lina kwenda vizuri bila ya tatizo lolote.

Amesema katika vituo vya uandikishaji unakwenda kujiandikisha zoezi hilo linakwenda vizuri na hawapati pingamizi.

“Tunashukuru zoezi hili linakwenda vizuri hakuna usumbufu wowote kwenye vituo vya uandikishaji wananchi wanapaswa kuutumia muda huu mfupi,” amesema.

Siti Bakari Abas, mkazi wa Jadida, Wete aliwataka wananchi wasiogope, bali wanatakiwa wajitokeze kwani hakuna tatizo lolote kwenye vituo hivyo. “

“Mimi niwatoe hofu wananchi wajitokeze kujiandikisha hakuna tatizo lolote wala usumbufu ukifika unaandikishwa unarudi nyumbani,” amesema Siti.

Wakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fadhila Abdalla alisema tangu kuanza kwa kazi hiyo wanapata ushirikiano mzuri na hakuna tatizo kwenye vituo vya kujiandikisha.

 Amesema wanakuwa na ushirikiano mzuri na wakuu wa vituo na mawakala wengine jambo linalochangia zoezi hilo kwenda vizuri.

“Tunapata ushirikiano mzuri na wakuu wa vituo watu wetu wanakuja kuandikishwa na tunapongeza zoezi hili tunaomba liendelee hivi hivi mpka mwisho kila mtu apate haki yake,” amesema.

Ali Huseni Khamis ni Mkuu wa kituo cha uandikishaji kwenye zoezi alisema mpaka sasa kwenye vituo hakuna changamoto kubwa isipokuwa ni kasoro ndogo ndogo na zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Hata hivyo amesema baadhi ya wananchi wakati mwingine alama za vidole havisomi lakini wanawasafisha kwenye vidole vyao na baadaye vinakubali kusoma na kupata kuandikishwa.

“Kiufupi zoezi linakwenda vizuri kasoro ndogo zinajitokeza lakini zinapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa baadhi ya watu ambao vidole havi somi na baadaye kukubali na kuandikishwa kwenye daftari hilo,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amesema ameridhishwa na utulivu uliopo katika kazi hiyo huku akiwataka wananchi wenye sifa ya kujiandikisha katika daftari hilo kujitokeza kujiandikisha ili waweze kupata haki yao ya msingi ya demokrasia.

Akielezea kuhusu uendeshaji wa kazi hiyo wilayani humo, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Ayoub Bakar Hamad amesema linakwenda vizuri na kwamba changamoto ni ndogo ikiwemo kutosoma alama za vidole.

“Hata hivyo tatizo hili linapatiwa ufumbuzi kwa haraka na mtu anaendelea kupata huduma inavyotakiwa,” amesema.

Amesema wapo maofisa wao wa Tehama wanalifanyia kazi na muda mfupi linatatuliwa na wananchi wanaendelea kupata kuandikishwa kwa wepesi katika zoezi hilo.

“Tumetembelea vituo mbalimbali vya uandikishaji katika Wilaya ya Wete zoezi linakwenda vizuri tunauliza wakuu wa Vituo na Makarani wa Uandikishaji pamoja na wakala wa vyama vya siasa lakini wanatuambia hakuna changamoto zinazojitokeza,” amesema Hamad.

Related Posts