Rais Samia ajitwisha zigo la ajira kwa vijana

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema wanaendelea kushughulikia suala la changamoto ya ajira kwa vijana kwa kubuni vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwakwamua kiuchumi.

Hilo linafanyika wakati wakitambua tatizo la ajira siyo la Tanzania pekee bali dunia nzima lakini wanalishughulikia kwani uelekeo wa miaka mingi ijayo inategemea na kasi ya kubaini changamoto mpya na kunyumbulika kwa wakati katika kuzitatua.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 5, 2025 wakati akitoa hotuba yake katika sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Kauli hii inakuja wakati ambao kumekuwapo na vilio vingi vya kukosekana ajira kwa vijana waliomaliza vyuo kwa nyakati tofauti nchini.

Jambo hilo limefanya fursa kiduchu za ajira zinapotangazwa watu wengi kujitokeza kuwania nafasi hizo jambo ambalo linatafsiriwa na wataalamu mbalimbali kuwa janga ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.

Samia amesema katika siku za usoni ni vyema kuanza kujipanga kwani wananchi watakuwa wakiwapima sera, mipango na kazi nzuri zinazofanyika na namna wanavyoleta matokeo kwa jamii.

“CCM imebaini changamoto ya ajira kwa vijana na inatambua kuwa ni changamoto ya dunia nzima na tumenaza kushughulikia hilo kwa kufanya mageuzi katika sera ya elimu na mafunzo ili iweze kujenga ujuzi na utaalamu vijana,” amesema Rais Samia.

Amesema lengo la Serikali ni kuona elimu inayotolewa kwa watoto vijana inawapa ujuzi wa kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika ameneo yao.

Mbali na mageuzi katika elimu pia Serikali imekuja na programu na mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuvutia mitaji ya uwekezaji ndani na nje ya nchi ili vijana waweze kuajiriwa na kujiajiri kupitia mazingira hayo ya biashara nchini.

“Tunafanya jitihada za makusudi kuwekeza katika sekta ya michezo Sanaa na burudani kwani uzoefu unaonyesha kuwa sekta hizo zinatoa mchango mkubwa katika kutoa ajira rasmi na zisizokuwa rasmi,” amesema Rais Samia.

Jambo lingine linalofanyika ni kukuza ufanisi katika sekta ya utalii na uchumi wa buluu kwa sababu zimeonyesha mchango katika utoaji ajira kwa vijana.

“Pia CCM inabuni programu zinazoweza kufanya wajiajiri wenyewe na kuajiri wengine ikiwemo Jenga kesho iliyo bora (BBT) katika sekta ya kilimo, mifugo na nyuki, vijana wanajengewe uwezo kupewa mitaji na nyenzo za kuweza kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wenzao,” amesema Rais Samia.

Amesema program hizo zina dhamira ya kutafuta majibu ya changamoto za wakati husika ambazo ndiyo zitatoa uhakika wa kesho ya CCM kwa kile alichokisema kuwa uimara wa CCM ijayo unatokana na kuimarisha jumuiya ya umoja wa vijana kwa kuwekeza kwao, kuwajenga kiitikadi ili waielewe siasa ya Tanzania na misingi ya kuanzishwa CCM.

“Kina mzee Jakaya Kikwete, Steven Wasira, Dk Emmauel Nchimbi na mimi mwenyewe (Rais Samia) na wengine wengi tunaojivunia uongozi wao yote hayo ni matokeo ya malezi mazuri waliyoyapata kutoka umoja wa vijana huenda wa Tanu na CCM.

Hivyo kesho salama ya chama chetu na nchi yetu itahakikishwa kwa vijana kujengewa uwezo ndani na nje ya nchi ili waweze kujipanga kitaasisi na kupambana kwa hoja na yeyote mwenye hoja hasi kwetu,” amesema Samia.

Katika kufanikisha hilo amesema ni lazima Umoja wa vijana Chama cha Mapinduzi (UVCCM) uimarishwe kimkakati kwani vijana ni hazina ya chama chao.

Hata hivyo, katika kushughulikia suala la ajira nchini, Serikali imekuwa ikitangaza nafasi za kazi katika kada mbalimbali kwa nyakati tofauti zinazoonekana kuwa na uhitaji mkubwa ikiwemo wataalamu wa afya, elimu.

Hilo lilishuhudiwa siku chache zilizopita baada ya watu 201,707 kujitokeza kuomba ajira kwenye kada ya ualimu kupitia nafasi 14,648 zilizokuwa zimetangazwa.

Kufuatia hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alitangaza kufanyika kwa usaili wa walimu hao Januari 14 hadi Februari 24, 2025.

Alipokuwa akizungumza na wanahabari, Januari 11, 2025 Simbachawene alisema kada hiyo hapo awali walikuwa wakipangwa moja kwa moja kwenye vituo vya kazi baada ya kupata ajira lakini sasa ni lazima wasailiwe ili wapate wenye sifa zinazohitajika kabla ya kupangiwa vituo vya kazi.

“Nafasi zilizotangazwa kujazwa kwenye kada ya ualimu zilikuwa ni 14,648 tu lakini mpaka sasa walioomba ajira kupitia Ajira Portal ni watu 201,707 utaona idadi ilivyo kubwa ya watu wanaohitaji kujaza nafasi hii lakini uhitaji wetu kwa sasa ni huo,” amesema Simbachawene.

Amesema usaili utafanyika kidijitali kwa wasailiwa ambao wamepewa namba maalumu ya usaili kwenye vituo vilivyopo kwenye mikoa waliopo ili kupunguza gharama za usafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya usaili huo.

Related Posts