Mwanza. Mwanafunzi anayesoma kidato cha tano katika moja ya shule ya sekondari iliyopo mkoani Tanga, Benadeta Silvester (21) amefariki dunia baada ya kukabwa koo na mpenzi wake, Adamu Kailanga (30) kisha naye kujinyonga kwa mtandio kisa wivu wa mapenzi.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa iliyotolewa leo Jumatano Februari 5, 2025 imesema baada ya kupata taarifa, Askari walifika eneo la tukio na kukuta mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa sakafuni na wa Adam ukining’inia juu ya paa la nyumba.
Mutafungwa amesema taarifa ya vifo hivyo vilivyotokea Mtaa wa Mkudi wilayani Ilemela jijini Mwanza ilipokewa Februari 4, 2025 saa 8 mchana kutoka kwa majirani ikielezwa chanzo ni Adam kumtuhumu mpenzi wake kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine.
Majirani walimsihi mwanaume huyo atulie kwa kuwa migogoro ya kimapenzi ni mambo ya kawaida kwa watu wengi,” amesema Mtafungwa.
Kamanda huyo amesema: “Ndipo mwanaume huyo alirudi ndani na hakutoka tena hadi majirani walipofungua mlango na kuwakuta wapenzi hao wakiwa wamefariki dunia kisha kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.”
Amesema uchunguzi umefanyika na kubaini Benadeta Silvester, alifariki baada ya kukabwa koo na Adamu Kailanga kifo chake kilisababishwa na kujinyonga kwa kutumia mtandio.
Mutafungwa ameeleza jeshi hilo linaendelea kufuatilia taarifa kuhusu mwanafunzi huyo na shule yake iliyoko mkoani Tanga, huku akiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia wenza wao pale kunapotokea migogoro ya kifamilia.
“Badala yake watumie njia sahihi ya kutatua migogoro hiyo ikiwemo kuwashirikisha wazazi wa pande zote mbili, viongozi wa dini na taasisi zinazoshughulika na utatuzi wa migogoro ya kijamii,” ameongeza Mutafungwa.