Dar es Salaam. Siku mbili kabla ya mkutano wa marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuhusu mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wadau wa masuala ya usafirishaji wameeleza matumaini waliyonayo ya kupatikana suluhu.
Mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili, kuanzia Ijumaa (Februari 7, 2025) hadi Jumamosi, utatanguliwa na mkutano wa mawaziri, ambapo ajenda kuu itakuwa mapigano yanayoendelea Goma, DRC, kati ya majeshi ya M23 na Serikali ya DRC, huku pia kukiwa na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na yale ya Sadc.
Akizungumza leo Jumatano, Februari 5, 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano mkuu wa tano wa Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania (Tamstoa), Mwenyekiti wa chama hicho, Chuki Shabani, amesema kufanyika kwa mkutano huo kunatoa matumaini ya kutatuliwa mgogoro uliopo DRC.
Shabani amesema wanatamani mkutano huo kuwa hatua muhimu katika kutatua changamoto zinazozuia biashara na usafirishaji katika taifa hilo.
Baadhi ya madereva wa magari ya mizigo, wakiwamo kutoka Tanzania, walikwama mjini Goma kutokana na mapigano hayo. Licha ya madereva hao kurejea nchini, malori 43, baadhi yakiwa na mizigo, inaelezwa kuwa yamebaki Goma.
Kwa mujibu wa Shabani, wanaamini hata magari waliyoyaacha nchini humo watayakuta salama.
“Wasafirishaji wengi wamenunua malori kwa mkopo, hivyo kutatua mgogoro huo kutatuwezesha si tu kuyapata magari, lakini kurejesha mikopo,” amesema.
Shabani amesema kati ya magari yaliyobaki, 41 yalikuwa sehemu moja aliyoitaja Jambo Safari, moja Senene na jingine lilikwama jirani na Uwanja wa Ndege wa Goma.
“Tuliahidi familia za madereva tutahakikisha madereva wetu wangerudi salama licha ya baadhi ya mali kuibwa, lakini tunajua mali zinatafutwa lakini siyo roho, na tuna imani na magari na mizigo yetu iliyosalia itabaki salama,” amesema.
Mwakilishi wa Kampuni ya DP World inayotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam, Elitunu Mallamia, aliyehudhuria mkutano wa Tamstoa, amesema wana imani kufanyika kwa mkutano wa EAC na Sadc kutaleta matumaini katika biashara yao ya upakiaji na upakuaji mizigo.
Mallania amesema tangu kampuni hiyo ianze kazi, biashara imekua kwa asilimia 24, huku nchi jirani zinazopakana na Tanzania, ikiwemo DRC, zikichangia kwa asilimia 47.
“Tumefurahi kusikia wiki hii kwamba viongozi, akiwamo Rais wetu Samia Suluhu Hassan, watazikutanisha pande hizi mbili zinazogombana kutafuta suluhu, jambo litakalosaidia biashara katika nchi hizo na Tanzania ziendelee,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa taasisi inayoshughulikia mahusiano ya kiuchumi na kijamii kati ya Bara la Afrika na China, Profesa Humphrey Moshi, amesema mkutano huo unapaswa kuonyesha dunia kwamba Afrika inaweza kutafuta suluhu za matatizo yake.
“Afrika twende tukaishangaze dunia kwamba tunaweza kumaliza mambo yetu wenyewe, kwani hakuwezi kuwa na maendeleo ya uchumi wa kijamii kama hakuna amani na kwa kuwa DRC na Rwanda ni moja ya nchi zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, waelezwe athari zinazoweza kupatikana katika jumuiya hiyo kwa kuendelea na mgogoro,” amesema.
Profesa Moshi amesema wa kunyooshewa kidole anyooshewe bila kuegemea upande wowote.
Mhadhiri Mwandamizi katika masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUCoM), Dk Balozi Morwa, amesema haoni kama mkutano huo unaenda kuleta suluhu.
Dk Morwa, ambaye pia ni mwanahistoria, amesema anachojua ni kwamba nchi zilizoendelea zipo tayari kutumia gharama zozote kupata taarifa kuhusu mkutano huo.
Awali, wakati wa kufungua mkutano, Shabani amesema pamoja na mafaniko mbalimbali ambayo Tamstoa wametapata, ikiwemo kuchangia uchumi wa nchi, bado wanakumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo foleni za barabarani hasa kutokea bandarini.
Kutokana na hilo, ameomba Serikali kuangalia namna ya kuwatengenezea barabara kwa ajili ya kupita malori, kwani foleni si tu inawaathiri kufikisha mizigo kwa wakati kwa wateja bali pia Serikali inapoteza mapato.
“Kwa foleni zinazoendelea jijini Dar es Salaam, kama mtu alikuwa na safari ya kwenda na kurudi anashindwa, lakini pia tumekuwa tukichelewesha mizigo ya wateja wetu.
“Tunaomba nasi tusikilizwe kilio chetu kwani tumekuwa tukipuuzwa kwa muda mrefu licha ya kuwa sekta ya pili kuchangia uchumi wa nchi hii na huko kwenye barabara tumekuwa tukichangia hela nyingi. Kuletwa kwa DP World hakutakuwa na maana kama barabara zetu hazipitiki,” amesema Shabani.
Mwenyekiti huyo ameomba kushughulikiwa matukio ya kamatakamata ya malori Temeke na Ubungo kwa sababu ya kuegeshwa barabarani. Amesema yote hayo ni kwa kuwa baadhi ya wamiliki hawana maeneo ya maegesho na wala kuingia bandarani hakuna maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya maegesho.
Meneja usalama wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), Geofrey Silanda, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Godius Kahyarara, amesema Serikali itashughulikia changamoto zilizotolewa na Tamstoa.
Kuhusu changamoto ya maegesho, amesema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umeshaelekezwa kutafuta maeneo mbadala, ikiwemo Mbezi ambako gari likipata hitilafu yoyote linapelekwa hapo.
“Vilevile tunaendelea kutafuta maeneo mengine ya kuwekeza ili kuhakikisha changamoto hii ya magari inaondolewa kabisa,” amesema.
Damu Mwalugenge, akimwakilisha Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, amesema wamekuwa wakishirikiana na wadau wa usafirishaji kwa karibu, ikiwemo kushughulikia foleni kwa kukaa hadi saa nne usiku ili kuona wanasafirisha mizigo yao kwa wakati na amani kutoka bandarini hadi Kimara.