Dar es Salaam. Mwana Mfalme Rahim Al-Hussaini ameteuliwa kuwa Imam wa 50 wa madhehebu ya Ismailia kufuatia kifo cha baba yake Mtukufu Aga Khan IV, ambaye alifariki dunia jana, Jumanne Februari 4, 2025, jijini Lisbon, Ureno.
Mwana Mfalme Rahim anayekuwa Imamu wa 50 wa madhehebu ya Shia Ismailia, ametangazwa kurithi nafasi hiyo, baada ya kufunguliwa kwa wosia wa marehemu baba yake.
Katika kipindi cha miaka 1,400 ya historia yao, waumini wa Ismailia wameongozwa na Imamu wa kizazi cha urithi. Waismailia wanaishi kwenye zaidi ya nchi 35 na idadi yao inakadiriwa kuwa kati ya milioni 12 hadi 15.
Rahim alizaliwa Oktoba 12, 1971, na ni mtoto wa kwanza wa Mwana Mfalme Karim Aga Khan na mkewe wa kwanza, Binti Mfalme Salimah.
Mwana Mfalme Rahim alipata elimu yake katika Shule ya Phillips Academy Andover na alihitimu mwaka 1995 katika Chuo Kikuu cha Brown na kutunukiwa Shahada ya Sanaa katika Fasihi Linganishi.
Ana watoto wawili Mwana Mfalme Irfan (aliyezaliwa 2015) na Mwana Mfalme Sinan (aliyezaliwa 2017).
Ni msimamizi katika bodi za mashirika mengi ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) na amekuwa akifuatilia kwa karibu kazi ya Taasisi ya Mafunzo ya Ismailia pamoja na taasisi za kijamii za jamii ya Ismailia.
Mwana Mfalme Rahim amejikita katika kusimamia AKDN ili kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, akihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Tabianchi.
Pia, ameonyesha kujitolea katika kusaidia kazi za AKDN na taasisi za jamii ya Ismailia katika kukabiliana na changamoto za umasikini, elimu, mafunzo na ujasiriamali.
Mwana Mfalme Rahim hukutana mara kwa mara na viongozi wa Serikali, mashirika ya kimataifa, na asasi za kiraia ili kuimarisha mahusiano yao na Imamu wa Ismailia na kuendeleza juhudi za AKDN za kuboresha maisha ya jamii zilizo pembezoni na zilizo hatarini zaidi.