‘Houseboy’ anayeshtakiwa kwa ubakaji adai ana umri wa mtoto

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kesi ya ubakaji Mashaka Manyama, ameibua utata mahakamani kuhusiana na umri wake pamoja na ushiriki wake katika tukio la shtaka linalomkabili.

Mshtakiwa huyo ameibua utata huo leo Jumatano, Februari 5, 2025 wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo baada ya kusomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni.

Katika maelezo hayo aliyosomewa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Rhoda Maingu, pamoja na mambo mengine mshtakiwa huyo amekana umri wake uliotajwa na upande wa mashtaka kuwa ana umri wa miaka 21, akidai yeye ana umri wa miaka 16.

Kwa kutaja umri huo, mshtakiwa huyo maana yake ameieleza mahakama yeye ni mtoto, kwani kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Mtoto, Namba 11 ya mwaka 2009, mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni mtoto.

Pia mshtakiwa huyo ameibua utata kuhusu mahali alipokuwa siku na wakati wa tukio hilo, kwani awali baada ya kusomewa maelezo na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu na kuulizwa kama ni kweli amejibu kuwa ni kweli.

Lakini baadaye alipoulizwa tena na Hamimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila anayesikiliza kesi hiyo hakutoa majibu ya kueleweka na Hakimu Rugemarila akasema anaandika kuwa mshtakiwa amekana.

Katika kesi hiyo Mashaka anadaiwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka saba, akidaiwa kutenda kosa hilo Septemba 12, 2024, eneo la Mikocheni, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Leo Jumatano Februari 5, kesi hiyo imesikilizwa katika hatua ya awali ambapo mshtakiwa amesomewa maelezo ya muhtasari wa kesi inayomkabili na kisha akatakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo na yale asiyokubaliana nayo.

Akimsomea mshtakiwa maelezo hayo ya awali, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Rhoda Maingu, amedai kuwa mshtakiwa huyo anaitwa Mashaka Manyama ana umri wa miaka 21, Msukuma na dini yake ni Mkristo.

Alipoulizwa kama anakubaliana na maelezo, amejibu kuwa anakubaliana na majina na makazi yake, kabila na dini yake lakini akadai kuwa umri huo si wake huku akibainisha kuwa umri wake ni miaka 16.

Wakili Rhoda amedai mshtakiwa ni mkazi wa Mikocheni B, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kwamba alikuwa mfanyakazi za nyumbani (house boy) nyumbani kwa Bibi Tom, maelezo ambayo alipoulizwa amekiri kuwa ni kweli.

Wakili Rhoda ameendelea kueleza kuwa siku ya tukio, Septemba 12, 2024, mshtakiwa huyo alikuwa Mikocheni B na alipoulizwa kama ni kweli amejibu kuwa ni kweli.

Vile vile Wakili Rhoda amedai kuwa siku hiyo ya tukio, Septemba 12, 2024 saa10 mpaka 11 jioni muathirika alikuwa akicheza na rafiki zake na yeye mshtakiwa alimuita chumbani kwake achukue mzigo ampelekee bibi yake Tom, maelezo ambayo mshtakiwa amekana kuwa si kweli.

Wakili Rhoda ameieleza zaidi kuwa chumbani mshtakiwa huyo alimziba mdomo na kumbaka mtoto wa miaka 7 si kweli, maelezo ambayo pia mshtakiwa amekana kuwa si kweli.

Kutokana na tukio hilo, Wakili Rhoda amesema kuwa mshtakiwa alikamatwa Septemba 14, 2024 na kupelekwa kituo cha Polisi Oysterbay na kuhojiwa, lakini mshtakiwa amekana kuwa si kweli.

Wakili Rhoda amedai kuwa alipohojiwa katika kituo cha Polisi Oysterbay, mshtakiwa alikiri kutenda kosa lakini yeye alipoulizwa kama ni kweli amekana kuwa hakukiri.

Akihitimisha maelezo hayo , Wakili Rhoda amesema kuwa Novemba 5, 2024 mshtakiwa alifikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizi, na mshtakiwa huyo akakubali kuwa ni  kweli.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, Wakili Rhoda ameieleza mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi watano ambo unatarajia kuwaita mahakamani kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa.

Hata hivyo alipoulizwa tena na Hakimu Rugemalira kuhusu baadhi ya maelezo aliyosomewa na mwendesha mashtaka hasa mahali alilokuwa siku ya tukio, hakutoa majibu yaliyoeleweka kwani hakukana wala kukubali wala hakusikika alichokuwa akikijibu.

“Mshtakiwa, kwani hujui kama tarehe hiyo ulikuwa Mikocheni au hukuwepo,” amehoji Hakimu Rugemarila baada ya kumhoji mshtakiwa swali hilo mara mbili bila kupata majibu sahihi kutoka kwa mshtakiwa huyo.

Hivyo Hakimu Rugemarila amesema kuhusu maelezo ya mshtakiwa kuwepo eneo la tukio Kwa tarehe iliyotajwa Mahakama itarekodi kuwa amekana (japo awali alikubali).

“Mshtakiwa baada ya kusomewa maelezo kuna uliyoyakataa na mengine kuyakubali. Haya yote uliyoyakataa upande wa mashtaka utaleta ushahidi kuyathibitisha,” amesema Hakimu Rugemarila na kuahirisha kesi hiyo mpaka Februari 19, 2025 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji ushahidi.

Mshtakiwa amerejeshwa mahabusu kutokana na kukosa wadhamini.

Related Posts