Simba hii, ikipata penalti mmekwisha!

ACHANA na matokeo ya mechi za jana ikiwa fungua dimba raundi ya 17 kwa Ligi Kuu Bara, kama hujui ni kwamba Simba ndio timu pekee iliyopata penalti nyingi kuliko yoyote ikiwa nazo saba huku zote ikiweka kambani.

Yaani kwa kifupi kila timu inayocheza na Simba ni lazima iwe na tahadhari ya kufanya madhambi langoni mwake, kwani Mnyama haachi kitu inapotokea adhabu hiyo kulingana na takwimu zilizopo.

Kati ya penalti saba ilizopata Simba, nne zimefungwa na mshambuliaji Leonel Ateba, huku tatu zikiwekwa wavuni na kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua na kuwafanya mastaa hao wawili kufikisha mabao saba ya ligi kila mmoja.

Tabora United inafuatia ikiwa na penalti tano na kati ya hizo imekosa moja ya mshambuliaji Heritier Makambo ilipochapwa mabao 3-1 na Fountain Gate katika mechi iliyopigwa Septemba 20, mwaka jana.

Timu nyingine ni Coastal Union ambayo pia imepata tano na kukosa moja ya mshambuliaji Maabad Maulid iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar – mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Oktoba 29, mwaka jana.

Yanga imepiga penalti tano na ni mbili tu ilizopoteza, zote akikosa za Stephane Aziz KI, akianza na ile ya kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United Novemba 7, mwaka jana na ushindi wa 4-0 mbele ya Kagera Sugar Februari Mosi, mwaka huu.

Azam FC imepata penalti tatu ikifunga zote, huku Namungo FC ikipata tano na kukosa mbili – akianza Moubarack Amza wakati timu hiyo ilipochapwa mabao 2-0 na Fountain Gate Agosti 29, mwaka jana.

Penalti nyingine iliyokoswa ni ya aliyekuwa beki wa timu hiyo, Djuma Shabani wakati kikosi hicho kiliposhinda mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union katika mechi iliyopigwa Septemba 17, mwaka jana.

Fountain Gate imepata penalti tatu na kufunga mbili huku moja ikikosa ambayo ilikuwa ya beki Nicholas Gyan katika mchezo iliochapwa mabao 2-1 na ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo mechi ikipigwa Babati Desemba 25, mwaka jana.

Mashujaa, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons zimepata penalti mbili kila moja na zote imefunga, huku Singida Black Stars ikipata mbili na kukosa moja ya Elvis Rupia wakati timu hiyo ikishinda mabao 2-1, dhidi ya KenGold Desemba 24, mwaka jana. 

Maafande wa JKT Tanzania wamepata mbili na kukosa moja ambayo ilikuwa ni ya nyota wa kikosi hicho, Hassan Dilunga wakati kikosi hicho kikitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Singida Black Stars, mechi ikipigwa Septemba 29, mwaka jana.

KenGold imepata penalti moja na kufunga, huku KMC FC, Pamba Jiji FC na Kagera Sugar zikiwa ndizo timu tatu pekee kati ya 16, zinazoshiriki Ligi Kuu Bara hadi sasa ambazo hazijapata penalti yoyote.

Related Posts