Kibano wanaotumia simu wakiendesha vyombo vya moto

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limependekeza mabadiliko ya sheria kupiga marufuku matumizi ya simu kwa madereva wanapoendesha vyombo vya moto.

Marufuku ya matumizi ya simu na vifaa vingine vya kielektroniki kwa madereva wa magari, pikipiki na bajaji inalenga kudhibiti ajali za barabarani.

Akizungumza na Mwananchi Januari 30, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkaguzi wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Dumu Mwalugenge alisema mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yameshawasilishwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania Desemba 31, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia ajali za barabarani na kuagiza Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati kuzizuia zile zinazosababishwa na makosa ya uzembe.

Alisema mwaka 2024 Tanzania ilikumbwa na jinamizi la ajali za barabarani, akieleza idadi ya watu waliofariki dunia ni 1,715.

“Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba 2024, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715.

“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alisema.

Mwalugenge amelieleza Mwananchi kuwa matumizi ya simu na vifaa kama vile spika za masikioni huathiri uwezo wa dereva kutambua mazingira yake, hali inayoongeza hatari ya ajali.

“Akiwa anatumia vifaa hivyo, anapoteza umakini. Inapotokea ajali au kuna ishara zozote za hatari inaweza kuwa vigumu kwa dereva kusikia au kutambua harufu yoyote inayoweza kuwa ishara ya tatizo,” alisema.

Mwalugenge alisema kikosi cha usalama barabarani kimepeleka mapendekezo mabadiliko katika Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ili kuzuia kabisa matumizi ya vifaa hivyo wakati dereva akiendesha vyombo vya moto.

Mbali na mabadiliko ya sheria, alieleza umuhimu wa kampeni za elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya matumizi ya simu na vifaa vingine vya kielektroniki barabarani.

Amesema katika mazingira ya sasa ya sheria, trafiki wanapowakamata madereva wanaotumia simu na kusababisha ajali, hutumia kifungu cha makosa ya uzembe kuwaadhibu kwa sababu hakuna kifungu mahususi kinachokataza matumizi hayo.

Mwalugenge amesema upungufu huo wa kisheria unasababisha ugumu wa kuchukua hatua kali kwa madereva wanaokiuka kanuni za usalama barabarani.

“Kwa sababu hatuna sheria inayozungumzia matumizi ya simu, tunapomkamata mtu aliyesababisha ajali kwa kutumia kifaa hicho, moja kwa moja tunatumia kifungu kinachozungumzia masuala ya uzembe barabarani,” alisema.

Tanzania haijaweka sheria kali kudhibiti matumizi ya simu barabarani kama ilivyo kwa Kenya na Uganda.

Kenya ina sheria kali zinazowazuia madereva kutumia simu wakiwa barabarani, huku Uganda ikiwa na sheria inayoelekeza adhabu kali kwa wanaokiuka taratibu hizo.

Mjumbe wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani nchini Tanzania, Alpherio Nchimbi aliwahi kupendekeza marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ili kujumuisha changamoto mpya kama vile matumizi ya simu.

“Lengo la dunia lilikuwa kupunguza vifo vya ajali hadi kufikia milioni 50 ifikapo mwaka 2020, lakini hali inaonyesha idadi ya vifo imeongezeka.

“Tanzania haijafanya vibaya, lakini bado kuna hatua za kuchukua, ikiwemo kufanyia marekebisho sheria ya usalama barabarani,” alisema Nchimbi.

Pius Isaya, dereva wa lori mkazi wa jijini Dar es Salaam amesema marekebisho ya sheria hiyo yamechelewa kwani baadhi ya kampuni tayari zimewazuia madereva wake kutumia simu na vifaa vingine vya kielektoniki wawapo barabarani ili kuepusha ajali.

“Siku hizi kampuni zimeamua kuwafungia madereva sehemu ya kuunganisha simu na kuongea bila kushika endapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo, kwani ajali za matumizi ya simu zinatokana na kushikilia mkononi hivyo ni ngumu kuwa makini kwa kutumia mkono mmoja,” amesema.

Ramadhan Selemani, dereva wa daladala linalofanya safari Mbagala amesema marekebisho ya sheria yatasaidia udhibiti kwa safari za mjini kwa sababu madereva wengi huzitumia wanapoendesha vyombo vya moto.

“Sheria itasaidia, wenzetu wenye magari binafsi wanatusumbua wanapoendesha na kuzungumza na simu muda wote bila kujali wakati mwingine wanasababisha ajali. Pia wanajisahau wana-chat bila kuchukua tahadhari,” amesema.

Amesema hata wao wana kasoro zao lakini hawatumii simu muda mwingi kwa sababu ya kuwahi abiria.

Kwa mujibu wa Baraza la Usalama Barabarani nchini Marekani, mwaka 2016 watu takribani 6,000 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani, huku asilimia kubwa ya ajali hizo zikihusishwa na matumizi ya simu.

Hii inaonyesha kuwa tatizo la matumizi ya simu barabarani si la Tanzania pekee, bali ni changamoto ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya vifo kutokana na ajali za barabarani imeongezeka kutoka watu milioni 1.24 mwaka 2016 hadi milioni 1.35 mwaka 2018, kulingana na Ripoti ya Hali ya Usalama Barabarani Duniani.

Pia, ripoti mbalimbali za WHO na utafiti wa ndani zinaonyesha licha ya ajali kuwa na sababu nyingi, matumizi ya simu barabarani ni tishio linaloongezeka kwa kasi.

Madereva na hata watembea kwa miguu wanahusika na shughuli za kidijitali wakiwa barabarani, hali inayosababisha kupungua kwa umakini wao.

Takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha idadi ya wamiliki wa simu za mkononi nchini imeongezeka kutoka milioni 27.62 mwaka 2012 hadi milioni 40 mwaka 2017.

Vivyo hivyo, matumizi ya intaneti yameongezeka kutoka watu milioni 7.52 mwaka 2012 hadi milioni 23 mwaka 2017.

Hali hii inazidisha hatari ya ajali kwani watu wengi hutumia simu hata wakiwa barabarani.

Related Posts