Dar es Salaam. Kama ulidhani kuwa kupika kwa umeme ni ghali, huenda ulikosea. Teknolojia mpya iliyozinduliwa na kampuni inayomilikiwa na Watanzania itawawezesha kutumia Sh500 kulipia umeme utakaotosha kupikia kwa siku nzima.
Teknolojia hiyo inahusisha matumizi ya sufuria za umeme zinazopika kwa haraka (pressure eCookers), ambazo zina uwezo wa kipekee kuhakikisha kuwa chakula kinakuwa tayari kwa matumizi kwa kutumia umeme kidogo zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kiwanda na Mfuko wa Maendeleo wa Nordic (NDF), ambao ni miongoni mwa wafadhili wa mradi huo, Mkurugenzi wa kampuni ya SmartPika, Andron Mendes, alisema kuwa teknolojia hiyo ni rahisi na nafuu, na ilitengenezwa kukabiliana na changamoto ya matumizi makubwa ya umeme ambayo huishia kumgharimu mtumiaji.
“Tumefanya utafiti huu kwa miaka mingi, na mwaka huu tuko tayari kuuzindua kwa soko letu. Ili kuhakikisha Watanzania wengi wanaweza kufikia teknolojia hii, tutatoa mikopo na tumeunda mfumo utakaowawezesha wateja kulipa kiasi kidogo ndani ya mwaka mmoja kupitia simu za mkononi na kisha kuwa wamiliki,” alieleza.
Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, nyumba zote zitakuwa zimeunganishwa na umeme, hivyo ni wakati wa nishati hiyo kutumika kwa matumizi mengine tofauti na kutoa mwangaza.
Mendes alibainisha kuwa kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh2.8 bilioni na sasa inatafuta Sh40 bilioni kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo ili kuwafikia Watanzania milioni 1.5 ndani ya miaka mitatu ijayo.
“Ubunifu mwingine ni kwamba, baada ya kupika, teknolojia yetu hutuma ujumbe unaoonyesha kiasi cha umeme na dakika zilizotumika, pamoja na kulinganisha na gharama ambayo ingekuwa imetumika kwa chanzo kingine cha nishati,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NDF, Satu Santala, alisema shirika hilo limeguswa na ubunifu huo ambao unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Santala aliongeza kuwa mradi huo ni hatua nzuri, na kuongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa, hasa katika kukuza matumizi ya nishati safi, ambayo inalinda mazingira na inahamasisha kampuni kukabiliana na changamoto zinazohusiana na hilo.
Naye kiongozi wa sekta ya nishati wa Shirika la Maendeleo la SNV la Uholanzi, Frances Bishop, alisema mradi huo unalingana na sera ya Serikali ya Tanzania kuhusu kupikia kwa nishati safi na mabadiliko ya kupikia kwa umeme.