Sababu marufuku ya matumizi ya mkaa Dar kukwaa kisiki

Dar es Salaam. Licha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwapiga marufuku wafanyabiashara wa chakula wakiwamo mama na babalishe kutumia kuni na mkaa kupikia, bei kubwa ya gesi na udogo wa majiko vinatajwa kuwa changamoto kwao kutumia nishati hiyo mbadala.

Tangazo la jiji pia linawahusu wafanyabiashara wa migahawa na hoteli.

Kwa kawaida mama na babalishe hutumia hadi majiko matano kwa wakati mmoja katika mapishi ili kuhudumia idadi kubwa ya wateja.

Mamalishe, Halima Hiza akizungumza na Mwananchi amesema mkaa bado ni nishati rahisi kwao, si tu kwa gharama bali pia kwa urahisi wa matumizi kulingana na ukubwa wa masufuria wanayotumia.

“Tunapika wali, pilau na ugali kwenye sufuria kuanzia kilo tano na kuendelea. Majiko ya gesi ni madogo hayawezi kutimiza mahitaji yetu, ndiyo maana wengi tunarudi kwenye mkaa,” amesema Halima anayefanya shughuli zake katika Soko la Mchikichini.

Dharau Mlungula, mamalishe katika soko hilo, amesema ugumu wa kutumia gesi unatokana na ukweli kwamba hupika vyakula mbalimbali kwa wakati mmoja jambo linalowalazimu kuwa na majiko yasiyopungua matano hadi sita.

“Ikiwa tutalazimika kutumia gesi pekee italazimu kusubiri jiko moja likamilike kupika chakula aina moja kabla ya kuanza kingine, jambo ambalo linatupotezea muda mwingi,” amesema.

Fatma Omar, mamalishe eneo la Soko la Machinga Complex, anasema changamoto nyingine ni gharama kubwa ya gesi.

Ametoa mfano akizungumzia mtungi wa gesi wa uzito wa kilo tano aliopatiwa Agosti, 2023 akieleza hautoshi kwa mahitaji yake.

“Kwa wiki nilitumia Sh46,000 kununua gesi wakati kwa mkaa nilitumia Sh30,000 tu. Hii ni tofauti kubwa kwa mtu mwenye kipato kidogo kama mimi,” amesema.

Mamalishe mwingine, Aisha Omar anasema kwa baadhi ya vyakula kama maharage na njugumawe huwezi kupika kwa urahisi kwa kutumia jiko la gesi.

“Gesi tunaiacha kwa ajili ya kupashia moto maziwa, supu, na mchuzi, lakini vyakula vigumu tunatumia mkaa,” amesema.

Watengenezaji wa majiko ya gesi wanasema hoja kuhusu udogo wa majiko si ya msingi wakieleza wanaweza kuyatengeneza kulingana na mahitaji yao.

Ali Dahal, fundi kutoka Jochata Vocational Centre anasema wamekuwa wakitengeneza majiko yanayotosheleza mapishi ya chakula kingi lakini mamalishe wanapendelea matumizi ya mkaa.

Dahal amesema alishawahi kuwatembelea mamalishe kuwaonyesha jiko linalogharimu Sh45,000 lenye uwezo wa kupika kilo tano za wali au ugali lakini wengi hawakununua.

“Walipendekeza niwakopeshe walipie kidogo-kidogo, lakini kwa kuwa hawakuwa na dhamana, niliogopa kupoteza mtaji,” anasema.

Masoud Kumbakumba kutoka kampuni ya Tamecco Gas Metal anasema taasisi zinazotoa msaada kwa mamalishe zinapaswa kuwa makini na kuwapatia majiko sahihi.

Amesema taasisi hizo zimekuwa zikiwapa majiko ya nyumbani badala ya matumizi ya kati, ndiyo maana wanapomaliza gesi hawanunui tena.

“Wanapewa majiko madogo yasiyotosheleza mahitaji yao. Tunayo majiko yanayouzwa kati ya Sh450,000 na Sh500,000 ambayo yana uwezo wa kupika vyakula vingi kwa wakati mmoja.

“Kama mashirika yatashirikiana nasi kutoa mtungi wa gesi, watakuwa wamepata wateja wa kudumu,” anasema.

Mwenyekiti wa sekta ya baba na mamalishe katika Soko la Mchikichini, Mwanahawa Julu anasema walipewa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, ikiwa ni pamoja na mkaa mbadala.

Hata hivyo, anasema upatikanaji wa mkaa huo bado ni changamoto kwa sababu haupatikani kwa urahisi kama gesi.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na jamii, Oscar Mkude, amesema ni vigumu kutekeleza agizo la kusitisha matumizi ya kuni na mkaa bila uwekezaji mkubwa kwa baba na mamalishe.

“Hawa ni wafanyabiashara wadogo wenye mitaji ya Sh10,000 hadi Sh20,000. Leo ukiwaambia wanunue mtungi wa Sh56,000 wanajiona wamebeba mzigo mkubwa,” amesema.

Mkude ameshauri halmashauri kuwapa baba na mamalishe mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya kununua gesi kupitia vikundi vyao ili walipe kwa pamoja.

Amehimiza benki na kampuni za gesi kuona nishati safi ni fursa ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara hao.

Amesema Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) na watu binafsi wanapaswa kuwekeza katika utengenezaji wa majiko makubwa ya gesi yanayoweza kupika vyakula vingi kwa wakati mmoja ili kuondoa changamoto iliyopo.

Januari 18, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilitangaza marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa kwa wafanyabiashara wa chakula, migahawa na hoteli.

Tangazo hilo lililotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa halmashauri hiyo, Tabu Shaibu likihimiza matumizi ya nishati safi kama gesi, umeme au nishati mbadala.

Tangazo hilo lilisisitiza watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ndogo za afya na uhifadhi wa mazingira za mwaka 2019.

Sheria hizo zinaeleza kuwa yeyote atakayekutwa anatumia nishati inayozalisha hewa chafu atalipa faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo cha miezi 12.

Kampeni hii imebebwa na kaulimbiu ya “Linda afya yako na wengine, tunza mazingira yakutunze, tumia nishati safi.”

Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, endelevu, salama na rahisi kutumika.

Mkakati huu wa miaka 10 uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 2024 unalenga kutoa mwongozo wa namna ya kupunguza athari za kiafya, mazingira na kuboresha maisha ya wananchi, huku ukipunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mpango mkakati huo unataka hadi kufikia asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Related Posts