Kesi ya Dk Slaa kutajwa leo Mahakama ya Kisutu

Dar es Salaam. Kesi ya kusambaza taarifa za uongo kwenye Mtandao wa X inayomkabili wanasiasa mkongwe nchini, Dk Willibrod Slaa (76) itatajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Dk Slaa anadaiwa  kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki na imeitwa leo Alhamisi, Februari 6, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wake umekamilika.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo inaitwa, mahakama hiyo imeshafungwa mikono kuendelea na hatua zaidi.

Hali hiyo inatokana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kuwasilisisha kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu, ulioelekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo pamoja na kuanagalia uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili kwa haraka.

Notisi hiyo ya kupinga uamuzi huo ilisajiliwa katika mfumo wa Mahakama ya Rufani Januari 30, 2025 na sasa inasubiriwa kupangiwa jaji.

Katika mazingira hayo, kwa kuwa mshtakiwa yupo rumande kutokana na upande wa mashtaka kuweka zuio la dhamana, kesi hiyo itakuwa inatajwa kila baada ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza hadi hapo suala lake litakapopata ufumbuzi katika Mahakama ya Rufani.

Awali, baada ya DPP kuzuia dhamana yake kwa kiapo, Dk Slaa alifungua mashauri mawili Mahakama Kuu akiiomba mahakama iitishe na kupitia mwenendo wa shauri dogo lililofunguliwa na Jamhuri kupinga dhamana yake na kuangalia kesi ya msingi ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.

Baada ya kusikiliza mashauri hayo, Mahakama Kuu ilitoa maelekezo ya kushughulikia masuala yote mawili haraka pamoja na maelekezo maalumu kwa mahakama zote za chini, kuhusu namna ya kushughulikia dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.

Katika maelekezo hayo, Mahakama Kuu ilizitaka mahakama hizo kuweka kipaumbele cha kwanza kabisa kushughulikia dhamana kuliko masuala yoyote yanayohusiana na kesi hizo, huku ikisisitiza kuwa suala la dhamana linapaswa lishughulikiwe siku ya kwanza mshtakiwa anaposomewa mashtaka.

Licha ya uamuzi huo kutoa mwanga kwa suala la Dk Slaa, matumaini yalifutika baada ya Jamhuri kutangaza uamuzi wa kuweka nitisi ya kukata rufaa kuupinga kwenye Mahakama ya Rufani.

Katika kesi ya msingi, Dk Slaa anakabiliwa na mashtaka ya kusambaza taarifa za uongo katika mtandao ya kijamii wa X Januari 9, 2025.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Dk Slaa kupitia jukwaa la mtandao wa a X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka:

“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya. …na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa, ni dhahili atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake”

Pia, inadaiwa alisema:  “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi, anahangaikia namna ya kurudi ikulu, na namna yake ya kurudi ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe.”

Related Posts