Dar es Salaam. Bomba la mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) ni miundombinu muhimu ya nishati inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam, Tanzania na Ndola, Zambia.
Lilijengwa mwaka 1968 kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Zambia, ili kusafirisha mafuta ghafi kutoka Tanzania hadi Zambia, kupunguza utegemezi wa Zambia kwa bandari za Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi.
Tazama ni bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1,710 na lina jukumu kubwa katika usambazaji wa nishati kwa uchumi wa Zambia, huku Tanzania ikinufaika na mapato ya usafirishaji wa mafuta.
Kwa muda mrefu, miundombinu hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uchakavu, uvujaji wa mafuta na mahitaji ya uboreshaji wa miundombinu. Serikali za Tanzania na Zambia zimekuwa zikijadili uwekezaji wa kulifufua ili kuongeza ufanisi wake, na sasa wamefanikiwa.
Januari 30, mwaka huu, uongozi wa miundombinu hiyo ulifanya uzinduzi wa kemikali maalumu iitwayo Drag Reducing Agent (DRA) ambayo iliondoa ulazima wa kupanua bomba hilo, kwani matumizi yake yaliongeza ufanisi wa bomba kutoka kusafirisha lita milioni 2.8 mpaka lita milioni 3.7 kwa siku.
Ongezeko hilo linafanya bomba hilo kuwa na uwezo wa kusafirisha lita za mafuta bilioni moja, tofauti na awali ambapo lilikuwa likisafirisha lita milioni 700 mpaka lita bilioni 1 kwa mwaka, hatua ambayo ni zaidi ya malengo ya kusafirisha lita milioni 900.
DRA inaongeza kasi ya mafuta kupita katika bomba na kupunguza mgandamizo wa mafuta ambao huongeza hatari ya mabomba kupasuka.
Meneja Uendeshaji wa Tazama- Tanzania, Simon Salu, anathibitisha kuwa DRA imeongeza msukumo wa mafuta kwa zaidi ya asilimia 20 na kupunguza msuguano wa bomba na mafuta ambao awali ulikuwa chanzo cha kutofikia makadirio ya Serikali.
“Tulishindwa kufikia makadirio ya Serikali kutokana na spidi ndogo ya mafuta hapo awali na presha kubwa iliyotumika kusukuma mafuta kwa kiwango kidogo,” anaeleza Salu.
Anasema mradi huo wa DRA umegharimu Dola 800,000 (Sh2 bilioni), na kuokoa gharama ambazo zingetumika kupanua bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,710.
“Kupanua bomba kunachukua muda mrefu, na ukarabati huo usingeweza kutatua tatizo hilo kwa wakati, ili kukidhi uhitaji wa mafuta kwa Wazambia,” anasema Salu na kuongeza kuwa Tazama ina vituo saba vya DRA vilivyopo Kigamboni, Morogoro, Mikumi, Iringa, Mbeya, Mikese na Chinsali, Zambia.
“Bomba la mafuta limegawanyika sehemu kuu mbili ambazo ni inchi 8 na inchi 12. Inchi 12 hutumika sehemu tambarare pekee, vituo vya DRA tumevijenga kwenye bomba zenye upana wa inchi 8 ambazo zinatumika kwenye sehemu zenye asili ya milima pekee,” anaeleza.
Anasema matumizi ya DRA yanaongeza kiwango cha mafuta kusafiri kwenda nchi jirani, ambapo huenda yakawa na manufaa mazuri kiuchumi.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Mwinuka Lutengano, anasema ongezeko la usambazaji wa mafuta linakwenda sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli hiyo lakini pia ukuzaji wa uchumi.
“Kutokana na hilo, usambazaji wa mafuta utaongeza pato la Taifa na kusisimua shughuli zote za kiuchumi, ambazo zinategemea mafuta, ikiwemo usafirishaji na uendeshaji wa mitambo. Kwa Zambia, itaongeza ufanisi wake katika mambo yaliyoathiriwa na kiwango kidogo cha mafuta ndani ya nchi,” anasema.
Anaongeza kuwa pato litokanalo na sekta hiyo litatumika kufanya maendeleo mengine kwa kufanya kazi mfululizo na bila changamoto kutokana na vikwazo vya mafuta.
“Kuna wakati usafirishwaji wa mafuta kwa njia ya magari unakwama kutokana na changamoto mbalimbali, ambazo huathiri uchumi wa juu na wa chini. Ila kwa teknolojia hii, uchumi utaimarika kutokana na tatizo hilo kutatuliwa.”
Mtaalamu mwingine wa uchumi, Donath Ulomi, anasema ongezeko la ufanisi wa bomba hilo utaharakisha shughuli za kiuchumi na kusisimua uchumi.
“Biashara zote za Tanzania na Zambia zinategemea mafuta ili shughuli za uzalishaji ziendelee. Kukua kiuchumi kwa tafsiri nyingine ni kuongeza miundombinu ya kuchochea uchumi,” anasema.
Hata hivyo, anasema kukua kwa sekta moja kiuchumi mara nyingi ni anguko kwa sekta nyingine, kwani biashara ya usafirishaji wa mafuta kwa njia ya lori itadidimia kutokana na mafuta mengi kufikishwa kwa njia ya bomba.
Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uhandisi wa Tazama, Deodatus Zege, anasema bomba hilo lililojengwa mwaka 1968 lilishindwa kukidhi mahitaji ya Zambia, hivyo ili kumaliza adha hiyo, walilazimika kutumia usafiri wa lori ili kukidhi mahitaji yao.Anasema teknolojia hiyo iliyoanza kutumika siku za hivi karibuni kabla ya kuzinduliwa rasmi imefanikiwa kukidhi mahitaji ya sasa nchini humo na sasa malori ya kusafirisha mafuta si mengi kama ilivyokuwa.
Zege anasema mradi huo umekamilika na kuanza kutumika ndani ya wiki tatu pekee na sasa matunda yake yanaonekana.
Anasema moja ya matarajio baada ya ufanisi wa bomba hilo kukamilika ni kushuka kwa bei ya nishati hiyo nchini Zambia kutokana na upatikanaji wake.
Waziri wa Nishati wa Zambia, Makozo Chikote, anasema ongezeko hilo la usambazaji wa mafuta litabadili uchumi wa Zambia na Tanzania, na kuwa urafiki huo wa kiuchumi utazidi kuzaa matunda kwa kuendelea kuongeza miradi ya pamoja.
Anasema kilichofanyika sasa ni matokeo ya kile kilichoanzishwa na waasisi wa Tanzania na Zambia katika kujenga urafiki na maendeleo ya kiuchumi baina ya nchi hizo.
“Tutaendelea kuwa familia katika maendeleo kama ilivyo Tazama na Tazara,” anaeleza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, anasema shirika hilo linalomilikiwa kwa ubia baina ya Tanzania na Zambia limezindua kemikali hiyo inayosaidia mafuta kuteleza na kuongeza kiasi cha mafuta yatakayopita kwa siku kwa asilimia 30, tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
“Ongezeko la mafuta yanayopita kwa siku litaongeza faida kwetu na kwa Wazambia,” anaeleza na kusisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa ili kupunguza gharama.
Licha ya ongezeko la mafuta yanayopita kwa siku, bomba hilo limekuwa imara na madhubuti zaidi katika utendaji wake wa kazi.
“Ongezeko la mafuta yanayopita kwa siku litaongeza faida kwetu na kwa Wazambia,” anaeleza na kuongeza kuwa mradi huo unapaswa kuwa somo la kutumia teknolojia za kisasa ili kupunguza gharama.
“Tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha, na tungesema tuongeze ukubwa wa bomba kwa asilimia 30 basi tungetumia mamilioni ya dola, lakini hapa tumetumia gharama ndogo sana. Tuongeze ubunifu na tutumie teknolojia ili kupunguza gharama,” anasisitiza.
Agosti mwaka jana, Serikali ya Tanzania ilieleza kuwa ipo kwenye mazungumzo na wenzao wa Zambia yanayolenga kuongeza uwekezaji katika bomba hilo ili kuliwezesha kuwa na uwezo wa kusafirisha mafuta mengi zaidi kwenda nchini Zambia na nchi nyingine za jirani.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alisema lengo la kufanya uwekezaji huo sasa ni kushusha gharama kwa wamiliki wa vituo vya mafuta katika maeneo ambayo bomba linapita.
“Mbali na upanuzi, pia tunatarajia kuanza ujenzi wa bomba jipya la inchi 24 na hili lipo katika hatua za ununuzi kabla utekelezaji haujaanza,” alisema Dk. Biteko.
Alisema lengo ni kuona utumiaji wa malori katika kusafirisha mafuta unapungua na watu wengi wanahamia katika kutumia bomba kwa kuchukua mafuta katika baadhi ya vituo vitakavyowekwa katika mikoa husika.
“Lengo letu ni mafuta yanayokwenda mikoa ya kusini kwa kutumia malori, yasafirishwe kwa bomba,” alisema Dk. Biteko.
Alisema kufanya hivyo kunalenga kuhakikisha Watanzania wanapata mafuta kwa bei nafuu kwa sababu gharama za usafirishaji ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuongezeka kwa bei ya mafuta ya rejareja.
Pia, kufanya hivyo kutasaidia kulinda barabara zisiharibike haraka kutokana na usafirishaji unaofanywa kwa kutumia malori.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tazama, Davison Thawethe, alisema bomba hilo jipya litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo milioni tano za mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Ndola, Zambia, kwa mwaka.
“Tumeagiza kampuni kufanya upembuzi yakinifu utakaoanza siku yoyote kuanzia sasa ili kubaini bomba hilo litagharimu kiasi gani,” alisema.
Alisema uamuzi wa kujenga bomba jipya ni kuendana na ukuaji wa bidhaa za mafuta unaoongezeka kila mwaka.
Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema shirika la Tazama lilianza miaka 58 iliyopita, na kama ingekuwa ni umri wa mtu, basi amebakiza miaka miwili kabla hajastaafu.
Alisema kipindi hicho mtu huwa ameishiwa nguvu, ila ni tofauti na Tazama, ambao umri huo ndiyo wanaanza kuamka na kupata nguvu kubwa.